Tuesday, December 24, 2024
spot_img

JINSI SERIKALI ILIVYOPORWA MALI ZA UMMA (2)

RIPOTI MAALUMU (2)


SKANDALI ya kuporwa kwa mali za umma kisha kutumiwa kuchukua mkopo wa mabilioni ya fedha kwenye Benki ya NBC; na Serikali kukiri kuwepo kwa skandali hiyo huku ikieleza jitihada ilizochukua na inazoendelea kuchukua kukabiliana na uhalifu huo; ni moja ya mambo ambayo Tanzania PANORAMA Blog iliyaripoti kwa kina mwaka 2022.

Hatma ya skandali hiyo bado ipo kwenye kiza kinene kwa sababu kampuni inayohusika na kashfa hiyo, SISI Construction Company Limited (SISICOL) ambayo Agosti 30, 2001 ilinunua hisa asilimia 75 za Serikali kwa Shilingi milioni 287.03 katika Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Company Limited (MECCO) inaendelea kupumua.

Kauli ya Serikali kuhusu skandali hiyo ilieleza kuwa imekwama kukamilisha urejeshaji wa mali za umma kwenye mikono yake ambazo zimeporwa na SISICOL kwa sababu SISICOL haikutoa ushirikiano uliohitajika kwa Mamlaka ya Mapato (TRA); na kwa sababu ya ukaidi huo wa SISICOL, skandali hiyo ingejadiliwa kwa mapana na marefu kwenye mkutano wa wanahisa wa Kampuni ya MECCO uliopangwa kufanyika mwaka jana, mkutano ambao hata hivyo haukufanyika.

Wanasheria waliozungumzia skandali hiyo walisema ni skandali kubwa inayoangukia kwenye makosa ya jinai na kwamba SISICOL na Meneja wa Benki ya NBC aliyehusika kuidhinisha mabilioni ya mkopo kwa kampuni ya SISICOL kwa kutumia mali za umma wanapaswa kushtakiwa mahakamani.

Kwa upande mwingine, mwanahisa mkubwa wa MECCO ambaye ni SISICOL alipoizungumzia skandali hiyo mwaka jana, alisema atajibu mapigo dhidi ya shutuma na madai yote aliyoelekezewa kwenye mkutano na waandishi wa Habari; mkutano ambao hadi leo haujafanyika. 

Hii ni sehemu ya pili ya ripoti maalumu inayoeleza kinaga ubaga skandali hiyo.

Mmiliki wa Kampuni ya SISICOL, Abdulkadir Mohammed

Sehemu ya kwanza ripoti hii inaonyesha mtaji wa Kampuni ya MECCO ulionekana kuongezeka kutoka Shilingi milioni 207.83 mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi bilioni 42.76 mwaka 2019. 

Ripoti ya uchunguzi wa skandali hii ambayo ilionwa na Tanzania PANORAMA Blog inaonyesha ongezeko hilo lilitokana na kufanyika kwa uthaminishaji ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 43.75 kiliingizwa kwenye vitabu kama Revalutaion Surplus.

Aidha, mwaka 2019 mkopo wa mwanahisa mkubwa wenye thamani ya Shilingi bilioni 3.8 uliokuwa umegeuzwa kuwa hisa ulirejeshwa kwenye vitabu lakini bado kulikuwa  na kutofautiana juu ya suala hili kwa jinsi mkopo huo ulivyoingizwa kwenye vitabu.

Uchunguzi uliofanyika unaonyesha umiliki wa Serikali kwenye Kampuni ya MECCO ulipunguzwa kutoka asilimia 25 hadi kufikia asilimia 2.6. Hisa hizi zilipunguzwa baada ya mwanahisa mkubwa, Kampuni ya SISICOL ambaye ndiye anayesimamia uendeshaji wa kila siku wa Kampuni ya MECCO kuingiza deni kwenye vitabu lililodaiwa kutokana na kuingiza fedha kwenye uendeshaji wa shughuli za kampuni na baadaye kuiomba Bodi kuidhinisha deni hilo kubadilishwa kuwa hisa zake.

Wakati yote haya yanafanyika mwanahisa mwenza ambaye ni Serikali hakushirikishwa.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alibainisha madudu yote haya kwenye uchunguzi maalumu alioufanya kwenye Kampuni ya MECCO, ndipo Serikali ikaanza kupambana kurejesha hisa zake zilizokuwa zimeporwa na SISICOL.

Serikali ilifanikiwa kurejesha deni linalodaiwa na SISICOL kwenye vitabu vya Kampuni ya MECCO na hivyo kurejesha umiliki wake (re-instate) hadi kufikia asilimia 25 ya hisa ilizokuwa nazo tangu awali.

Hili linathibitishwa pia kwenye taarifa za Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA) ambako hivi sasa rekodi zilizoko zinaonyesha kuwa Serikali inamiliki asilimia 25 ya hisa katika Kampuni ya MECCO.

Rekodi kuhusu makubaliano ya uendeshaji wa Kampuni ya MECCO baina ya Serikali ya Kampuni ya SISICOL zinaonyesha kuwa wakati SISICOL inanunua hisa kwenye Kampuni ya MECCO ilikubali masharti ya ununuzi ikiwemo kuhakikisha inaongeza mtaji wa uendeshaji na kufanya uwekezaji wakati Serikali ikiwa haiwajibiki kufanya uwekezaji wowote kutokana na hisa ilizobaki nazo.

Jengo la Makao Makuu ya NBC

Katika ripoti yake, CAG anaonyesha kuwa Kampuni ya MECCO chini ya uendeshaji wa SISICOL ilikuwa imehamisha umiliki wa baadhi ya mali zake kwenda kwa mwanahisa mkubwa ambaye ndiye SISICOL kama sehemu ya malipo ya deni la mwanahisa huyo lililoingizwa kwenye vitabu mwaka 2008.

Baada ya deni hilo kurejeshwa kwenye kampuni, ilikubalika pia kuwa mali hizo ambazo zilikuwa tayari zimefanyiwa mabadiliko ya hatimiliki na kusomeka jina la MAS Holding and Container Depot Limited (kampuni dada ya SISICOL) zirejeshwe katika umiliki wa MECCO.

Lakini wakati hilo likiamriwa hivyo, kuliibuka utata mwingine baada ya kubainika kuwa hati za mali hizo zilikuwa tayari zimetumika kama dhamana ya mkopo katika Benki ya NBC, ndipo Serikali ikamuomba Msajili wa Hazina awasiliane na uongozi wa Benki ya NBC ili hati hizo ziweze kubadilishwa wakati zikiendelea kuwa katika uhifadhi wa benki hiyo.

INAENDELEA…..

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya