RIPOTI MAALUMU
RIPOTA PANORAMA
SKANDALI ya kuporwa kwa mali za umma kisha kutumiwa kuchukua mkopo wa mabilioni ya fedha kwenye Benki ya NBC; na Serikali kukiri kuwepo kwa skandali hiyo huku ikieleza jitihada ilizochukua na inazoendelea kuchukua kukabiliana na uhalifu huo; ni moja ya mambo ambayo Tanzania PANORAMA Blog iliyaripoti kwa kina mwaka 2022.
Hatma ya skandali hiyo bado ipo kwenye kiza kinene kwa sababu kampuni inayohusika na kashfa hiyo, SISI Construction Company Limited (SISICOL) ambayo Agosti 30, 2001 ilinunua hisa asilimia 75 za Serikali kwa Shilingi milioni 287.03 katika Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Company Limited (MECCO) inaendelea kupumua.
Kauli ya Serikali kuhusu skandali hiyo ilieleza kuwa imekwama kukamilisha urejeshaji wa mali za umma kwenye mikono yake ambazo zimeporwa na SISICOL kwa sababu SISICOL haikutoa ushirikiano uliohitajika kwa Mamlaka ya Mapato (TRA); na kwa sababu ya ukaidi huo wa SISICOL, skandali hiyo ingejadiliwa kwa mapana na marefu kwenye mkutano wa wanahisa wa Kampuni ya MECCO uliopangwa kufanyika mwaka jana, mkutano ambao hata hivyo haukufanyika.
Wanasheria waliozungumzia skandali hiyo walisema ni skandali kubwa inayoangukia kwenye makosa ya jinai na kwamba SISICOL na Meneja wa Benki ya NBC aliyehusika kuidhinisha mabilioni ya mkopo kwa kampuni ya SISICOL kwa kutumia mali za umma wanapaswa kushtakiwa mahakamani.
Kwa upande mwingine, mwanahisa mkubwa wa MECCO anayetokea SISICOL alipoizungumzia skandali hiyo mwaka jana, alisema atajibu mapigo dhidi ya shutuma na madai yote aliyoelekezewa kwenye mkutano na waandishi wa habari, mkutano ambao hadi leo haujafanyika.
Hii ni ripoti maalumu inayoeleza kinaga ubaga skandali hiyo.
Historia ya Kampuni ya Umma ya Mwananchi Engineering and Contracting Company Limited (MECCO) inaonyesha kuwa ilisajiliwa Februari 10,1964 ikiwa inamilikiwa na Serikali baada ya Chama cha Tanganyika African Union (TANU) kununua hisa za Kampuni ya Tanganyika Engineering kupitia Shirika la Maendeleo la Mwananchi (Mwananchi Development Corporation-MDC) ambalo lilikuwa shirika la chama hicho.
Kampuni hiyo ilibinafsishwa Agosti 30, 2001 baada ya Serikali kuuza asilimia 75 ya hisa zake na ilisajiliwa Aprili, 2007 kupitia Sheria ya Makampuni (The Companies Act 2002). Fedha za ubinafsishaji wa MECCO zilipelekwa kwenye akaunti ya ubinafsishaji iliyokuwa chini ya PSRC.
Kazi kubwa ya Kampuni ya MECCO ni ujenzi wa majengo, barabara, madaraja na kazi nyingine zinazohusiana na ujenzi na kwa mujibu wa hesabu za mwisho za kampuni kabla ya kubinafsishwa, ilikuwa ikimiliki mali zenye thamani ya Shilingi bilioni 54.39.
Kati ya mali hizo, Shilingi bilioni 42.76 zilikuwa mali za muda mrefu zinazojumuisha ardhi yenye thamani ya Shilingi bilioni 35.46, majengo yenye thamani ya Shilingi bilioni 5.07 na mitambo yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.22. Mali za muda mfupi za Kampuni ya MECCO zilikuwa na jumla ya Shilingi bilioni 11.63, sehemu kubwa ikiwa ni madeni ya wateja yaliyokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 5.69.
Aidha, wakati inabinafsihwa ilikuwa na kazi zinazoendelea zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.86, fedha taslimu kiasi cha Shilingi bilioni 1.97, kodi ya zuio yenye thamani ya Shilingi bilioni 0.5 na kodi inayojulikana kwa jina la kimombo kama Tax Advance yenye thamani ya Shilingi bilioni 0.2.
Kampuni ya MECCO ilikuwa na madeni yenye thamani ya Shilingi bilioni 12.26. Sehemu kubwa ya madeni hayo yakiwa ya wazabuni yenye thamani ya Shilingi bilioni 5.88, malipo ya awali ya wateja yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.92, deni la mwanahisa mkubwa lenye thamani ya Shilingi bilioni 1.39, deni la Shilingi milioni 70.37 la kodi ya mapato na Shilingi milioni 8.76 ya overdraft ya benki.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Setrikali (CAG), deni la mwanahisa mkubwa limetokana na malimbikizo ya riba yaliyotokana na mkopo wa fedha za uendeshaji zilizotolewa na mwanahisa mkubwa baada ya ubinafsishaji ambazo hazikuweza kuthibitishwa wakati wa ukaguzi maalum uliofanywa na CAG.
Wakati wa ukaguzi wa CAG, Kampuni ya MECCO ilikutwa na hisa zenye thamani ya Shilingi milioni 443.73 ambazo hata hivyo zilikuwa zimepungua ikilinganishwa na mwaka uliotangulia kabla ya ukaguzi wa CAG ambapo hisa hizo zilikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 4.24.
CAG alibaini kuwa mabadiliko hayo yalitokana na kurejeshwa kwa mkopo wa mwanahisa kwenye vitabu uliokuwa umebadilishwa na kuwa hisa hapo awali na hivyo kupunguza umiliki wa Serikali kwenye MECCO.
Mtaji wa Kampuni ya MECCO ulionekana kuongezeka kutoka mwaka 2018 hadi mwaka 2019. Ongezeko hili lilitokana na kufanyika kwa uthaminishaji ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 43.75 kiliingizwa kwenye vitabu kama Revalutaion Surplus.
Aidha, mwaka huo pia, mkopo wa mwanahisa mkubwa wenye thamani ya Shilingi bilioni 3.8 uliokuwa umegeuzwa kuwa hisa ulirejeshwa kwenye vitabu. Hata hivyo, bado kumekuwa na kutofautiana juu ya suala hili kwa jinsi mkopo huu ulivyoingizwa kwenye vitabu.
INAENDELEA….