ABBAS MWALIMU
Wakati leo Zanzibar ikiadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi, si vibaya kupata picha ya hali ya Mapinduzi ya visiwa hivyo ilivyokuwa.
Changamoto ilianza kwenye uchaguzi wa mwisho wa Julai 1963. Aidha, kwa mara ya kwanza wanawake waliruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi huo.
Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa kama ifuatavyo; Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilipata kura 47,943 na kushinda viti 12, Afro Shiriz Party (ASP) kilipata kura 87,402 na kushinda viti 12 huku Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) ikipata kura 25,610 na kushinda viti sita (Mapuri, 1996)
Kwa ujumla ni kwamba ASP kilipata asilimia 54.2 ya kura zote au kura 13,849 zaidi ya kura za ZNP na ZPPP kwa pamoja. Licha ya ASP kupata kura hizo lakini hakikutangazwa mshindi badala yake ZNP na ZPPP vikaungana kuunda Serikali.
Baadaye Disemba 10, 1963 Zanzibar ilitangazwa kupata uhuru. Kwa bahati mbaya sana uhuru wa mwaka 1963 haukuakisi kujikomboa kwa Mzanzibari kutoka kwenye makucha ya ukoloni wa Waingereza na utawala wa Sultani.
Hili lilitokana na ukweli kwamba Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1963 ilianzisha mfumo wa usultani wa kikatiba ambao ulimpa Sultani ukuu wa nchi. Vilevile Katiba hiyo ilimpa Sultani na “warithi wake” uongozi wa Zanzibar usio na ukomo wa muda (Rejea ibara ya 32,33,34,35 na viapo First Schedule, Part II vya Katiba ya mwaka 1963).
Ikumbukwe kuwa, Sheikh Abeid Amani Karume akiwa kwenye mkutano wa hadhara huko Raha Leo
mwezi Disemba, 1959 alitamka kwamba, ‘ASP ilitaka Zanzibar iwe Jamhuri, kauli ambayo Serikali ya kikoloni haikukubaliana nayo’ (ASP, 1973).
Hivyo kitendo cha Katiba ya mwaka 1963 kuipa Zanzibar uhuru wa kisultani ilikuwa ni sawa na kuendeleza ukoloni visiwani humo.
Kutokana na hali hiyo, ASP iliona kuwa milango yote ya kidemokrasia kwa upande wa Waafrika ilikuwa imefungwa na Waingereza na Waarabu hivyo ASP iliiona kuna njia moja tu ya kuleta uhuru wa kweli Zanzibar, nayo ni kupitia Mapinduzi ya Umma.
Ndipo Mapinduzi Matukufu yakafanyika Januari 12, 1964. Mapinduzi hayo yaliitwa Matukufu kwa sababu hayakuhusisha jeshi kupindua nchi (Coup d’etat.)
Januari 13, 1964 kulitokea tukio nadra kufanyika duniani, lakini tukio hilo lilifanyika Zanzibar. Sheikh Abeid Amani Karume akiwa amefuatana na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Sultani na kiongozi wa ZPPP, Mohammed Shamte Hamad na kiongozi wa ZNP, Ali Muhsin Barwan walienda
Redio Zanzibar kutangaza rasmi kwamba Mapinduzi yamefanikiwa na kwamba Zanzibar ni Jamhuri yenye Serikali mpya.
Sheikh Karume akahimiza utulivu na amani na kuahidi kwamba Serikali mpya itaendeshwa na watu, kwa ajili ya watu na kwa kuzingatia matakwa ya watu.
Sheikh Karume akatumia muda huo kuuelezea umma wa Wazanzibari kuwa mbali na Mohammed Shamte na Ali Muhsin Barwan aliokuwa amefuatana nao, viongozi wengine katika Serikali iliyopinduliwa kama vile Sheikh Idarusi, Sheikh Ibuni Salehe, Sheikh Juma Alley na mawaziri, walikuwa mikononi mwa Serikali mpya na akaahidi kuwalinda mpaka hali itakapotulia.
Mohammed Shamte Hamad kwa upande wake, akawasihi wanachama na wapenzi wa ZPPP kuacha malumbano na mapambano na kusalimisha silaha zao kwa utaratibu uliowekwa. Aidha, Mohammed Shamte aliwataka wanachama wa ZPPP kuitii Serikali mpya.
Kwa msisitizo Mohammed Shamte alisema, ‘Serikali iliyoundwa jana ndiyo Serikali ya nchi na wanachama wetu wote hawana budi kuitii Serikali mpya.’
Naye Sheikh Ali Muhsin akatoa wito kwa wananchi kuacha mapambano na kusalimisha silaha zao na kuitii Serikali, akisema; ‘Tukio limetokea, utake usitake. Kinachohitajika sasa ni kuijenga Zanzibar mpya na sote hatuna budi kushiriki’ (ASP, 1974)
Tukio hilo la kihistoria lipo tofauti na taarifa nyingi za kwenye magazeti, vitabu, mitandao, majarida na kauli za baadhi ya watu kuwa Sultani Jamshid aliikimbia nchi akiwa na Waziri Mkuu Shamte na mawaziri wake.
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse)
+255 719 258 484
Marejeo:
(1) ASP (1973) Afro-Shirazi–A Liberatin Movement, ZPPC
(2) ASP (1974) The Afro-Shirazi Revolution 1964-1974, Printpak Tanzania Ltd, Dar es Salaam.
(3) Mapuri, O.R., (1996) The 1964 Revolution: Achievements & Prospects, TEMA Pubishers Company Ltd, Dar es Salaam.