Thursday, July 17, 2025
spot_img

TANROADS YATEKELEZA VIPAUMBELE VYA 2022/2023


KAZI ya utekelezaji wa vipaumbele na majukumu ya Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 inaendelea kwa kasi kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mpango wa Taifa wa maendeleo wa mwaka 2020/2025.

Kuelekea mwisho wa mwaka wa fedha wa 2022/2023, tayari TANROADS imekamilisha kikamilifu utekelezaji wa miradi 14 ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 883; ikiwa ni kuanzia Aprili 2021 hadi Oktoba 2022.

TANROADS ambayo imekasimiwa jukumu la kuratibu na kusimamia, ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara kuu na za mikoa; kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ilikuwa na jukumu la utekelezaji wa kazi hizo kwenye kilometa 36,362 za barabara ikiwa ni kazi za mwaka wa kwanza wa bajeti ya kazi ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Ielewele kuwa TANROADS ilianzishwa kwa waraka wa Serikali uliotolewa kwenye gazeti la Serikali nambari 293 la Agosti 25, 2000 kwa mujibu wa sheria ya wakala wa Serikali nambari 30 ya mwaka 1977 na lengo la kuanzishwa kwake ni kuleta ufanisi zaidi katika majukumu yaliyokuwa chini ya Idara ya Barabara katika Wizara ya Ujenzi.

TANROADS ilianza kufanya kazi Julai 1, 2000 na utekelezaji wa vipaumbele na majukumu yake kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ni wa 22 sasa toka kuanzishwa kwake na; katika bajeti ya mwaka huu miradi iliyoitekeleza ni ya jumla ya Shilingi trilioni 1.37.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Rogatus Mativila

Taarifa ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Rogatus Mativila kwa umma kuhusu utekelezaji wa vipaumbele na majukumu ya taasisi yake inaeleza kuwa wakala ina jukumu la kufanya utafiti kuhusu vifaa vya ujenzi wa barabara kupitia Kitengo cha Maabara Kuu ya Vifaa (Central Materials Laboratory) na maabara ndogo zilizopo kila mkoa hapa nchini.

Katika taarifa yake hiyo, Mativila anayataja majukumu mengine ya  TANROADS kuwa ni kudhibiti uzito wa magari barabarani na kulinda maeneo ya hifadhi ya barabara na kwa sasa TANROADS ina mizani 70 ya kudumu na mizani 22 ya kuhamishika.

Mizani hiyo ya kuhamishika, Vigwaza ipo miwili, Mikese mmoja, Dakawa miwili, Njuki miwili, Nala miwili, Mpemba miwili, Wenda miwili na Kimokouwa miwili  ambayo kazi yake ni kupima uzito wakati gari linatembea (Weight in Motion) na kwamba TANROADS pia inasimamia usanifu wa ujenzi wa viwanja vya ndege nchini.  

Mativila anaeleza katika taarifa yake ya utekelezaji wa vipaumbele na majukumu ya taasisi anayoiongoza kwa bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwa mpango ulikuwa kujenga kilometa 12,216 kwa barabara kuu na kwa barabara za mikoa ilipangwa kujengwa kilometa 24,146 na kwamba jumla ya kilometa za lami zilizojengwa ni 11,513.

Katika taarifa yake, Mativila anafafanua kuwa; “Jumla ya miradi 14 yenye urefu wa kilometa 883 imekamilika kati ya Aprili 2021 hadi sasa, yaani ndani ya kipindi cha Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ya Shilingi trilioni 1.37.

“Miradi hiyo ni Barabara ya Kidahwe hadi Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 iliyopo Mkoa wa Kigoma, Barabara ya Nyakanazi hadi Kibondo (Kabingo) yenye urefu wa kilometa 50 nayo ya mkoani Kigoma na Barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66 ya mkoani Ruvuma.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua barabara ya Njombe Makete hivi karibuni

“Barabara nyingine zilizokamilika ni ile ya Njombe hadi Moronga Section, hii ina kilometa 53.9 na ipo Mkoa wa Njombe na katika mkoa huo huo wa Njombe kuna barabara ya kutoka Moronga hadi Makete Section, yenye urefu wa kilometa 53.30 nayo ipo tayari. Katika Mkoa wa Mara kuna barabara ya Makutano hadi Natta (Sanzate) Section, hii ina urefu wa kilometa 50 na barabara nyingine ni ya Waso hadi Sale Jct Section yenye urefu wa kilometa 49, hii ipo mkoani Arusha.

“Pia kuna barabara ya Kikusya, Ipinda hadi Matema yenye kilometa 39.10 ya mkoani Mbeya, pia hapo hapo Mbeya kuna barabara nyingine ya Chunya hadi Makongolosi yenye urefu wa kilometa 39. Katika Mkoa wa Tabora kuna Lot 1, Usesula hadi Komanga Section and Sikonge Spur Road kwa urefu wa kilometa 115.50.

“Katika Mkoa wa Katavi kuna Lot 2, Komanga hadi Kasinde Section na Iyonga Spur Road kwa urefu wa kilometa 112.80 na Lot 3, Kasinde hadi Mpanda Section na Urwira Town Section kwa urefu wa kilometa 108.00. Katika Mkoa wa Songwe kuna barabara ya Mpemba hadi Isongole yenye urefu wa kilometa 50.30 na aidha, ile ya Mpanda, Kibo hadi Usimbili yenye kilometa 37.65 nayo imekamilika.”

Taarifa ya Mrendaji Mkuu huyo inazungumzia pia miradi ya madaraja makubwa yaliyokamilika kujengwa ambapo anasema yapo manne. Anayataja madaraja hayo kuwa ni daraja la Tanzanite lililopo Mkoa wa Dar es Salaam ambalo lina urefu wa kilometa 1.03, daraja la Ruhuhu lililo katika barabara ya Kitai kwenda Lituhi mkoani Ruvuma lenye urefu wa meta 98.

Daraja la Tanzanite lililojengwa mkoani Dar es Salaam

“Mkoa wa Manyara, daraja la Magara lenye urefu wa meta 84 limekamilika kujengwa; kwingineko ni mkoani Mara ambako daraja Mara lenye meta 940 liko tayari. Katika Mkoa wa Singida daraja la Msingi lenye meta 100 na daraja la Sibiti lenye meta 82 yamekamilika na pia kuna daraja la Wami lenye meta 514 nalo kazi imekamilika.”

Mativila katika taarifa yake anaitaja miradi ya madaraja makubwa matatu ambayo ujenzi wake unaendelea kuwa ni daraja la Magufuli (Kigongo hadi Busisi) la mkoani Mwanza ambalo lina urefu wa kilometa 3.2, daraja la Pangani lenye meta 520 na daraja la Kitengule lenye urefu wa meta 140; Gharama za ujenzi wa madaraja hayo ni Shilingi bil 701.

Taarifa inaeleza zaidi kuwa, “miradi ya madaraja makubwa sita ambayo usanifu wa kina umekamilika ni daraja la Simiyu lililopo barabara ya Mwanza kwenda Musoma, daraja la Bwawa la Mtera lililo barabara ya Iringa kwenda Dodoma, daraja la Mzinga katika barabara ya Dar es Salaam kwenda Kibiti, daraja Mitomoni la mkoani Ruvuma, daraja la Mkenda la mkoani Ruvuma na daraja la Jangwani mkoani Dar es Salaam.”

Kuhusu miradi ya barabara inayoendelea na ujenzi, taarifa hiyo ya Mativila inaeleza; “Jumla ya miradi 44 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,523 ikiwa na gharama yaShilingi trilioni 3.8ipo katika hatua mbalimbali ya ujenzi nchi nzima.

‘Miradi hii inahusisha miradi inayogharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani na inayogharamiwa kupitia washirika mbalimbali wa maendeleo. Aidha, mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege na majengo ya abiria unaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi bil 360.

‘Ipo pia miradi 62 ya barabara ambayo iko katika hatua mbalimbali za manunuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami ambayo inajumuisha miradi inayogharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani pamoja na fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Daraja jipya la Wami lililopo Mkoa wa Pwani.

‘Lakini pia Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS imeanza utekelezaji wa Miradi ya EPC + F yenye urefu wa kilometa 2,533. Kampuni zilizokuwa “shortlisted’ zilialikwa tarehe 22 Septemba, 2022 kuwasilisha zabuni tarehe 22 Novemba, 2022.

‘Miradi hiyo ni barabara ya Kibaha, Mlandizi, Chalinze hadi Morogoro yenye kilometa 205. Hii ni Expressway. Pia barabara ya Kidatu, Ifakara, Lupiro, Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo hadi Lumecha mkoani Songea yenye urefu wa kilometa 512 na barabara ya Arusha, Kibaya hadi Kongwa yenye urefu wa kilometa 493.

‘Nyingine ni barabara ya Handeni, Kiberashi, Kijingu, Njoro, Olboroti, Mrijo Chini, Dalai, Bicha, Chambolo, Chemba, Kwa Mtoro hadi Singida yenye kilometa 460 na pia kuna barabara ya Igawa, Songwe hadi Tunduma ina kilometa 218 na barabara ya Masasi, Nachingwea hadi Liwale yenye urefu wa kilometa 175.

‘Kwenye miradi hiyo ya EPC + F pia kuna barabara ya Karatu, Mbulu, Hydom, Sibiti River, Lalago hadi Maswa ambayo ni ya kilometa 389 na barabara ya Mafinga hadi Mtwango, hii ina urefu wa kilometa 81.’

Taarifa ya Mativila pia inaeleza kuwa ipo miradi 43 ya barabara ambayo ipo katika hatua mbalimbali za upembuzi yakinifu yenye urefu wa kilometa 2,021.04ambayo ujenzi wake utagharimu Shilingi Bil 9.6

Mativila anahitimisha taarifa yake hiyo kwa kueleza kuwa ‘katika mwaka wa fedha 2021/22, kati ya Julai 2021 hadi Mei 2022, jumla ya mikataba 20 inayohusisha miradi ya ujenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege inayogharimiwa moja kwa moja na fedha za ndani na mingine fedha za washirika wa maendeleo ilisainiwa.

‘Mikataba ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilometa 582.455 imesainiwa na mikataba ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Msalato na kumalizia jengo la kiwanja cha ndege Songwe pamoja na mizani ya Rubana nayo imekwishasainiwa ambapo gharma ya miradi yote 20 ni Shilingi Bil 1,460.84.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya