RIPOTA PANORAMA
RAIS Samia Suluhu Hassan ametangaza kuondolewa kwa zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Akizungumza leo na viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu Ikulu, Dar es Salaam Rais Samia amesema mikutano ya hadhara ni haki ya kisheria na ni haki ya vyama vya siasa.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na kilio kutoka kwa wanasiasa na jamii za kimataifa kuhusu haki ya kufanya siasa hasa mikutano ya siasa kuruhusiwa, haki ambayo ipo kisheria na kwamba uwepo wake mbele ha wanasiasa hao ulikuwa kutangaza kuondolewa kwa zuio la kufanya mikutano hiyo.
Hata hivyo, Rais Samia alitoa rai kwa wanasiasa hao kutimiza wajibu wao kwa kufanya siasa za kistaarabu wakifuata sheria na kanuni wakati wa kufanya mikutano ya hadhara na wanapotekeleza majukumu yao ya kisiasa.
“Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka.
“Lakini ndugu zangu tuna wajibu, wajibu wetu Serikali ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema. Twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, tukafanye siasa za kupevuka, tukafanye siasa za kujenga sio za kubomoa, si kurudi nyuma hapa tulipofika, sisi ndani ya CCM tunaamini katika kukosolewa na kujikosoa.
“Wakati mnanikabidhi kuongoza nchi hii busara zilinituma kwamba jinsi nilivyolipokea taifa hili kuna haja ya kufanya taifa liwe kitu kitu kimoja, wote tuzungumze lugha moja, ili taifa liwe moja lazima tuwe na maridhiano. Nikasema kwanza tuwe na mazungumzo kwenye vyama vya siasa,’” amesema Rais Samia.
Mkutano huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wenyeviti, makamu wenyeviti, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu kutoka vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu.