VATICAN
MWILI wa Papa Mstaafu Benedikto XVI, aliyefariki dunia Disemba 31, 2022 umelazwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro huko Vatican ambako watu kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatoa heshima zao mwisho.
Vyombo vya habari mbalimbali vya Italia na Vatican leo vimeripoti kuwa mwili wa Papa Mstaafu Joseph Ratzinger, ambaye ndiye Papa Mstaafu Benedikto XVI uliondolewa katika Monasteri ya Mater Ecclesiae na kuwekwa katika Altare ya Maungamo iliyopo Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Jumatatu ya Januari 2. 2023 kwa ajili ya watu kutoa heshima zao za mwisho.
Mtandao wa habari za Vatican, Vatican News umeripoti kuwa baada ya mwili wa Papa Benedikto XVI kuwekwa Altare ya Maungamo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro ambalo lilikuwa limefungwa kwa muda; wa kwanza kuingia kanisani humo kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho alikuwa Rais wa Jamhuri ya Italia, Sergio Mattarella akiwa ameambatana na binti yake Laura ambao walisimama wakisali wakiwa wameshikana mikono.
Aliyefuatia alikuwa Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni akiwa ameambatana na Katibu wake, Alfredo Mantovano na Waziri wa Kilimo, Francesco Lollobrigida ambao kwa pamoja walipiga magoti na kusali mbele ya mwili wa Papa Mstaafu Benedikto XVI huku wakishuhudiwa na Kardinali Michael Harvey na Kardinali Mauro Gambetti ambaye ni msimamizi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Kardinali Gambeti aliongoza ibada fupi ya kumuombea Papa Mstaafu Benedikto XVI Jumatatu ya Januari 2, 2023 iliyoanza saa 7.15 hadi 7.40, baada ya kuhamishwa kwa mwili wa Papa huyo kutoka nyumba ya Mater Ecclesiae iliyo katika bustani ya Vatican ambapo alikuwa akiishi baada ya kung’atuka kwenye wadhfa wa upapa mwaka 2013.
Ukiwa katika Altare ya Maungamo kwenye Kanisa Kuu la Mtakarifu Petro, mwili wa Papa Mstaafu Benedikto XVI umezungukwa na Askofu Gänswein Memores Domini ambaye alikuwa msaidizi wake wa kila siku kwa miaka mingi pamoja wasaidizi wake wa zamani.