RIPOTA PANORAMA
DARAJA la Tanzanite linaloanzia kando kidogo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi na kwenda hadi eneo la Oysterbay linatarajiwa kufungwa kwa muda wa siku saba kwa ajili ya kuwekewa nembo ya Tanzanite.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam wa Wakala wa Barabara (Tanroad), barabara hiyo itafungwa kuanzia Januari 2, 2023 majira ya saa 12 asubuhi na kufunguliwa Jumatatu ya Januari 9, 2023 saa 12 asubuhi.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa katika muda wote wa maboresho hayo ya uwekaji nembo ya Tanzanite, daraja hilo halitatumika kwa sababu za kiusalama na watumiaji wake wanashauriwa kutumia Barabara ya Kaunda na Ali Hassan Mwinyi.
Daraja la Tanzanite lilizinduliwa Machi 24, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye baada tu ya kulizindua aliwaagiza Tanroads kuiondoa nembo ya Mwenge wa Uhuru iliyokuwepo na kuweka nembo ya Tanzanite ambayo italeta maana halisi ya jina na kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa la kisasa na kufungua fursa za kiuchumi na biashara.
Daraja hilo lenye utefu wa kilometa 1.03 lilijengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 243 na Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Korea Kusini.