RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imeeleza masikitiko yake dhidi ya madai ya ukatili anaofanyiwa Mohamed Ally Rwambo ambaye ni mfanyakazi wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha Colourful Industry Limited, kilichopo Mbagala jijini Dar es Salaam.
Pia imempa pole Rwambo kwa kueleza kuwa malalamiko yake yanaumiza na ni uvunjifu wa sheria lakini imetoa angalizo kuwa siyo busara kuhukumu bila kusikiliza pande zote mbili na kuchambua hoja na ushahidi kisheria ili kutoa uamuzi wa haki.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Wizara Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi alipokuwa akizungumzia madai ya Rwambo anayemlalamikia mwajiri wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Colourful Industry Limited, Fu He, maarufu zaidi kwa jina la Lina kwa kumfanyia vitendo vya kikatili baada ya kuumia akiwa kazini.
“Hii taarifa ndiyo unanipa wewe sasa hivi, si busara kuhukumu bila kusikiliza pande zote mbili na kuchambua hoja na ushahidi kisheria ili kutoa uamuzi wa haki ila nampa pole sana kama ndivyo, imeniumiza sana pia na kuvunja sheria.
“Ili haki itendeke pande zote kwa kuwa siko huko, aende kumuona afisa kazi mkoa na huko atapata msaada wa kiofisi na kisheria. Anaweza kutumia chama chake cha wafanyakazi kufungua malalamiko CMA au yeye mwenyewe kwenda tume ya usuluhishi na uamuzi CMA. Afike Ofisi za WCF pia kwa fidia watamuongoza kisheria,” amesema Naibu Waziri Katambi.
Katika madai yake, Rwambo anamtuhumu mwajiri wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Colourful, Lina kwa kumdhulumu haki zake alizopaswa kulipwa baada ya kupata ajali iliyosababisha kukatika vidole vyake viwili na kimoja kupoteza uwezo wa kufanyakazi vya mkono wa kushoto, kumlazimisha kusaini barua ya kuacha kazi kwa hiari kabla ya mkataba wake wa ajira kuisha na kumfungulia kesi polisi akimtuhumu kwa wizi.
Rwambo anadai alianza kufanyakazi Kiwanda cha Colourful mwaka 2014 kama ‘Operator’ wa mashine na ilipofika mwaka 2016 alipata ajali iliyosababisha kukatika vidole viwili na kimoja kukosa uwezo wa kufanya kazi ambapo alitibiwa na kupona lakini alipoanza kudai malipo yake ya kuumia akiwa kazini ndipo uhasama baina yake na bosi wake Lina ulipoanza.
Rwambo anadai zaidi kuwa amebambikiwa kesi ya kuvamia Kiwanda cha Colourful, kuwateka na kuwafunga kamba walinzi wawili kisha kuiba Shilingi 200,000 na mashine ya kuosha magari na kwamba kesi hiyo iliyofunguliwa mwezi Agosti, 2022 hadi sasa upelelezi wake haujakamilika kwa madai kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi na wakati huo huo mwajiri wake amesitisha kumlipa mshahara wake akidai kuwa ni jambazi.
Anaeleza kushangazwa na kukawia kwa upelelezi huo wakati kiwandani hapo kuna kamera zinazoweza kuonyesha ukweli wa kilichotokea siku anayotuhumiwa kutenda uhalifu kiwandani hapo na kwamba kitendo cha mwajiri wake kumuhukumu kuwa ni jambazi wakati kesi yake haijafikishwa mahakamani na yeye kutia hatia ni cha kikatili na uonevu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Richard Michael Ngoye alipoulizwa kuhusu kuchelewa kwa upelelezi wa kesi hiyo alisema mwenye mamlaka ya kuzungumzia mambo ya kipolisi kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo na alipotafutwa Kamanda Murilo kuzungumzia hilo, simu yake haikuweza kupatikana mara moja.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Coroulful, Lina alipoulizwa kuhusu madai ya Rwambo alisema si ya kweli na alimtuhumu kwa kusema uongo kwa kile alichoeleza kuwa jeraha alilopata ni la miaka mingi na alilipwa fidia. Alisema polisi walimkamata kwa sababu alihusika na wizi kwenye tukio lililowahusisha watu sita.
Akizungumzia kuhusu kusitisha kumlipa mshahara Rwambo akingali mfanyakazi wake, alisema yeye hana deni lolote naye na kwamba alikuwa akiiba lakini anamsamehe kisha alieleza mshangao wake kuwa ni kwa namna gani majambazi wanajiamini hivyo.
Alipoulizwa Lina iwapo ana uthibitisho kuwa Rwambo ni jambazi na iwapo kesi yake imekwishafikishwa mahakamani na kutolewa hukumu alisema maswali hayo aulizwe wakili wake kisha akatoa namba za simu za wakili wake huyo.
Alipotafutwa wakili wa Lina ambaye hakutaja jina lake wakati akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, alisema yupo polisi atafutwe Jumatatu ya Disemba 19 na alipotafutwa tena siku hiyo alisema hakumbuki alichozungumza na PANORAMA na alipokumbushwa alitaka atumiwe kwa maandishi kile kinachoulizwa ili ajibu kwa maandishi pia; jambo ambalo lilitekelezwa lakini licha ya kusoma alichoulizwa, hakujibu.
TANZANIA PANORAMA INAENDELEA KURIPOTI KWA UFASAHA SAKATA HILI