Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MENEJA NBC, SISICOL WAWEZA KUSHTAKIWA KWA UHUJUMU UCHUMI

RIPOTA PANORAMA

SERIKALI inaweza kuwashtaki mahakamani Meneja wa Benki ya NBC na Kampuni ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Hayo yameelezwa na wanasheria waliozungumzia na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu skandali ya kuporwa kwa ardhi na mali za umma na kutumika kuchukua mkopo wa mabilioni ya Shilingi benki, ukiwemo mkopo usiokuwa na ukomo.

Katika skandali hiyo, Kampuni ya SISICOL inadaiwa kupora kwa kiwango kikubwa hisa za Serikali asilimia 25 inazomiliki kwenye Kampuni ya Mwananchi Engeenering and Contracting Company Limited (MECCO) na kuhamisha umiliki wa mali za kampuni hiyo ya umma na kuzitumia kuchukua mkopo mkubwa benki ambao haujalipwa.

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekwishakiri kuifahamu skandali hiyo kwa kueleza kuwa ilibaini Kampuni ya SISICOL kupora kwa kiwango kikubwa hisa zake asilimia 25 inazomiliki kwenye MECCO baada ya kuwekwa bayana na ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambaye katika ripoti yake alionyesha kuwa mwanahisa mwenye hisa nyingi, asilimia 75 katika kampuni ya MECCO alikuwa amechukua kinyemele hisa za mwanahisa mdogo ambaye ni Serikali, kutoka asilimia 25 na kumbakiza hisa asilimia 2,6 tu.

Akizungumzia skandali hiyo, Mwanasheria Kiongozi wa Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba alisema kuna vitendo vya kijinai vilivyofanyika ambavyo vinapaswa kuripotiwa polisi.

Alivitaja vitendo hivyo kuwa ni kughushi, udanganyifu, kula njama, kutumia nyaraka za huo udanganyifu na uhujumu uchumi unaohusisha pia utakatishaji fedha ambapo wahusika wakikamatwa wanaweza kufikishwa mahakamani kwa makosa hayo yasiyo na dhamana.

“Kuna vitendo vya kijinai vimefanyika ambavyo vinapaswa kuripotiwa polisi. Vitendo hivyo ni vya kughushi, udanganyifu, kula njama, kutumia nyaraka za huo udanganyifu na uhujumu uchumi unaohusisha pia utakatishaji fedha ambapo wahusika wakikamatwa wanaweza kufikishwa mahakamani kwa makosa hayo yasiyo na dhamana.

“Uhamishaji hisa isivyo halali na kuzitumia kuchukua mkopo ni kosa la jinai. Hapo ndipo uhujumu uchumi kwa kosa la utakatishaji fedha hutokea. Sheria za Makosa ya Jinai, Sura ya 16 na Uhujumu Uchumi Sura ya 200 na Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai Sura ya 20 zitatumika.

Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba.

“Hata benki haitakiwi kutoa mkopo bila kuchunguza uhalali wa kampuni husika, mali za kuchukulia mkopo, nk. Ikifanya hivyo nayo itakosea. Maafisa wa benki hiyo hasa meneja wake nao wanaweza kuunganishwa katika kesi ya jinai ya uhujumu uchumi,” alisema Wakili Komba.

Mwanasheria mwingine aliyezungumzia skandali hiyo kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa, yeye alisema katika skandali hiyo kilichofanyika ni kughushi kwa kudanganya Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela) na Mamlaka ya Mapato (TRA).

“Uamuzi wa kupeana au kuuziana hisa upya haukufuata utaratibu. Wanahisa wakiwemo wawakilishi wa Serikali hawakufanya mkutano wa maamuzi hayo kwa hiyo maamuzi kama yapo ni ya kughushi kwa kuidanganya Brela na TRA.

“Hivyo inabidi upande wa wanahisa waliohujumiwa (Serikali) kufungua kesi ya madai Mahakama Kuu kudai hisa ilizoporwa isivyo halali. Sheria ya Makampuni, Sura ya 212 vifungu vya kuanzia 200 na kuendelea hueleza hivyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Eric Mkuti katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni, Serikali ilifanya ufuatiliaji na kubaini kuwa ni kweli mbia wake, Kampuni SISICOL alikuwa amepunguza hisa za Serikali kinyemela.

Alisema kubainika kwa jambo hilo kuliwekwa bayana na ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG ambaye katika ripoti yake alionyesha kuwa mwanahisa mwenye hisa nyingi, asilimia 75 katika Kampuni ya MECCO alikuwa amechukua kinyemele hisa za mwanahisa mdogo ambaye ni Serikali kutoka asilimia 25 na kumbakiza hisa asilimia 2,6 tu.

Alisema Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifuatilia hila hiyo iliyokuwa imefanywa na SISICOL na kufanikiwa kurejesha hisa zake zote.

Akizungumzia hila nyingine iliyofanywa na Kampuni Mas Holding and Container Depot Limited ambayo ni kampuni dada ya SISICOL ya kubadilisha kinyemela hati za viwanja viwili, kiwanja namba mbili na kiwanja namba 3B vilivyopo Barabara ya Nyerere, Manispaa ya Temeke, ambavyo ni mali ya MECCO, kutoka MECCO kwenda kwenye umiliki wa Mas Holding and Container Depot Limited, Mkuti alisema hata hilo Serikali inalifahamu na imekwishachukua hatua.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

“Hata hilo Serikali inalifahamu, inafahamu hila iliyofanyika na imekwishachukua hatua ingawa kulitokea mkwamo kidogo lakini umma uelewe kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu sana jambo hilo.

“Kwenye ule ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG ilibainika kuwa mwanahisa mkubwa alihamisha umiliki wa baadhi ya mali za MECCO kwenda kwenye umiliki wa kampuni yake ya SISICOL kama sehemu ya malipo ya deni la mwanahisa huyo lililoingizwa kwenye vitabu mwaka 2008.

“Kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa uendeshaji wa Kampuni ya MECCO baina Serikali ya mbia wake huyo, yeye ndiye mwenye jukumu la kusimamia shughuli za kila siku za kampuni lakini hilo siyo ruhusa kwake kuhamisha mali.

“Serikali baada ya kulibaini hilo kama nilivyokwambia baada ya kufanyika kwa ukaguzi, iliamriwa mali za MECCO ambazo zilikuwa tayari zimefanyiwa mabadiliko ya hatimiliki na kusomeka jina la MAS Holding and Container Depot Limited zirejeshwe katika umiliki wa MECCO.

“Msajili wa Hazina alisimamia kazi hiyo ya utekelezaji wa uamuzi huo na hatua za kubadilisha umiliki wa hati ya mali hizo kurudishwa kwenye umiliki wa MECCO zilianza hadi kufika hatua ya kufanya malipo ya stamp duty na capital gain ili kukamilisha taratibu za kubadilisha umiliki.

“Katika hilo MECCO ilifanya malipo ya stamp duty kisha ikaomba kupatiwa msamaha wa capital gain tax lakini Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitoa maelekezo kuwa hesabu za Kampuni ya MECCO na zile za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited ni lazima ziwasilishwe kwa mamlaka hiyo ili ifanye makadirio ya kodi kabla ya kuangalia huo msamaha.

“Hao jamaa hawakufanya kilichosemwa na TRA na badala yake wakakimbilia kwa Waziri wa Fedha na Mipango ambako nako walirudishwa TRA kwani aliwaambia watekeleze walichoambiwa na TRA. Hapa nikwambie tu kuwa hawajatekeleza hayo maagizo ndiyo maana kuna mkwamo lakini Serikali inafuatilia kwa karibu sana,” alisema Mkuti.

Mkuti pia alikiri Serikali kufahamu hila zilizofaanywa na mwanahisa wake huyo kutumia hati za viwanja namba 2 na kiwanja namba 3B vilivyopo barabara ya Nyerere, Manispaa ya Temeke ambavyo ni mali ya MECCO kuchukua mkopo mkubwa katika moja ya benki hapa nchini pasipo kuihusisha Serikali ambayo ni mbia wake na hadi sasa mkopo huo haujarejeshwa.

Alisema, “Hata hilo Serikali inalifahamu na imeishachukua hatua. Msajili wa Hazina alifanya mawasiliano na Benki ya NBC na hatua za kurejesha umiliki wa hati hizo zilianza lakini kama nilivyoeleza kulitokea mkwamo kidogo baada ya hawa jamaa kutowasilisha hesabu zao TRA.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ambaye jina lake ni mioja ya majina viongozi wa Serikali na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanayodaiwa kutumiwa vibaya na mmiliki wa Kampuni ya SISICOL, Abdulkadir Mohammed katika harakati zake za kibiashara alipohojiwa na Tanzania PANORAMA Blog alijitenga mbali na mfanyabiasha huyo kisha akaitupia ‘mzigo’ Ofisi ya Msajili wa Hazina kuizungumzia skandali kuporwa kwa ardhi na mali za umma na kutumika kuchukua mkopo wa mabilioni benki.

Mwenyekiti wa Kampuni ya MECCO, Kwabhi Maungo.

Mwenyekiti wa Kampuni MECCO, Kwabhi Maungo alipohojiwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu skandali hiyo alisema atajibu hoja zote ambazo menejimenti ya MECCO imeelekezewa kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao hata hivyo hakusema utafanyika lini.

“Tumetuhumiwa sana, tumechafuliwa sana na ninyi mkaandika hayo waliyoyasema. Sasa siwezi kusema lolote kwa sasa, siwezi kusema kama kuna mkutano wa wana hisa au vinginevyo. Tunachokifanya sasa tunajipanga kujibu yote hayo yaliyosemwa, na wewe siwezi kukwambia lolote kwa sababu ndiyo walikwambia ukaandika, nitaitisha mkutano mkubwa wa waandishi wa habari wote ndiyo ntasema hapo kila kitu,” alisema Maungo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya