Monday, December 23, 2024
spot_img

KETE ZA CCM UCHAGUZI MKUU 2025

SIMBA GEMBAGU NGW’ANA NJAMITI

HEKAHEKA za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 zimeanza. Wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo ya siasa wanabashiri kuwa iwapo mwenendo wa sasa wa siasa za Tanzania utaendelea kama ulivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kukabiliwa na ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani.

Sababu zinazotolewa za CCM kukabiliwa na ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao ni nyingi na wapo wanaokwenda mbali zaidi kimtazamo na pengine ‘kiimani’ wakiongozwa na ‘kudhani’ kuwa ushindani mkali utakuwa ndani ya CCM chenyewe; hata hivyo hayo siyo sehemu ya makala haya, yana nafasi yake pana zaidi kuyajadili huko tuendeko. Hapa najielekeza kwenye kete za CCM katika uchaguzi mkuu wa 2025.

CCM kinaelekea kwenye uchaguzi huo kikiwa na nguvu kubwa ya umaarufu wa kisiasa kuliko vyama vingine vya siasa na pia kina mtaji mkubwa wa kuhodhi nafasi za uongozi wa kisiasa. Hizi ni kete za kutosha zinazokipa matumaini ya kuingia kwenye ushindani wa kuwania ukuu wa Dola na nafasi za uwakilishi dhidi ya vyama vya upinzani.

Lakini sambamba na hayo, CCM pia kina kete nyingine muhimu kitakayoiweka mezani wakati wa uchaguzi mkuu huo ambayo ni utekelezaji wenye mafanikio wa Ilani yake ya uchaguzi wa mwaka 2020 iliyobeba dira ya Taifa ya maendeleo ya 2020 hadi 2025.

Haina shaka kuwa mafanikio ya utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ndiyo kete muhimu zaidi ya CCM kitakayosimama nayo kwa wapigakura kuomba ridhaa ya kuendelea kushika ukuu wa Dola na tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekwishaiweka mezani kete hiyo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2022 kwenye mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho ulioketi kwa siku mbili katika ukumbi Jakaya Kikwete jijini Dodoma, hivi karibuni.

Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwa katika mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Katika wasilisho lake hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alianza na mafanikio katika ukusanyaji mapato kwa kuwaeleza wana CCM wenzake kuwa, ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa Shilingi trilioni 1.46 kwa mwezi, katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi kufikia wastani wa Shilingi trilioni1.74 kwa mwezi, katika kipindi cha mwaka 2021/2022.

Alizungumzia pia uwekezaji na viwanda ambapo aliwaeleza makada wenzake kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia uwekezaji katika viwanda vitakavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini ili kukuza pato la mwananchi, kupunguza umasikini na kuongeza ajira.

Kwamba baadhi ya viwanda vilivyozinduliwa hivi karibuni ni kiwanda cha kuzalisha sukari cha Bagamoyo, kiwanda cha kusafishia madini ya dhahabu cha Geita na kiwanda cha kuchambua pamba cha NGS, Ifukutwa kilichopo Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi.

Kuhusu ajira alisema; “moja ya ahadi ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020 ni kuzalisha ajira zipatazo milioni nane katika kipindi cha miaka mitano. Katika kutekeleza programu ya kukuza ajira kwa vijana ambayo ni jumuishi katika sekta zote, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kutekeleza miradi ya kimkakati, kutoa mafunzo ya ujuzi na kutoa mikopo yenye masharti nafuu, ajira 1,381,618 zimezalishwa kwa watanzania kupitia sekta ya umma na binafsi.

“Vile vile, Serikali imehakikisha miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini inatoa ajira, kuwanufaisha wazawa na kuwajengea uwezo ili kukidhi vigezo vya ajira hizo. Jitihada hizo zimewezesha miradi ya kimkakati kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana 97,832 na zisizo za moja kwa moja 377,000 kwa vijana wenye ujuzi mahiri, ujuzi wa kati na wasio na ujuzi.”

Mafanikio mengine yaliyotangazwa na Waziri Mkuu Majaliwa yalihusu sekta ya miundombinu ambapo alisema Serikali imeendelea kuboresha barabara na ujenzi wa madaraja makubwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji.

Kwa maneno yake mwenyewe alisema; “Kipindi cha Novemba, 2020 hadi Oktoba, 2022 Serikali imejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilometa 950.29, Aidha.

“Serikali iliendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara mijini na vijijinizenye urefu wakilometa 50,373.23 ambapo barabara za kiwango cha changarawe ni kilometa 9,989.36 na matengenezo ya kawaida na sehemu korofi ni kilometa 22,045.68.

Darala la Tanzanite.

“Vile vile, Serikali inaendelea na ujenzi wa madaraja makubwa ya Kitengule lililopo Mkoa wa Kagera, Daraja Jipya la Wami la mkoani Pwani, Daraja la Msingi lililopo Mkoa wa Singida na Daraja la Kigongo – Busisi la mkoani Mwanza. Ujenzi wa Daraja la Tanzanite lililopo Mkoa wa Dar es Salaam na Daraja la Kiyegeya lililopo Mkoa wa Morogoro umekamilika.”

Mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) nao aliutaja katika mafanikio hayo, alisema; “Hadi kufikia Novemba, 2022 kipande cha Dar es Salaam hadi  Morogoro chenye urefu wa kilometa 300 kimefikia asilimia 97.49 na Morogoro hadi Makutopora chenye urefu wa kilometa 422 ujenzi wake umefikia asilimia 90.07, Mwanza hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 341, ujenzi umefikia asilimia 14.2 na Makutopora hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368 ujenzi wake umefikia asilimia 1.92 ilhali ujenzi wa kipande cha Tabora hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 165, umeanza.

“Utengenezaji wa mabehewa unaendelea vizuri. Kati ya mabehewa 81, mabehewa 36 yamekamilika na 14 kati ya hayo yaliwasili Bandari ya Dar es Salaam tarehe 22, Novemba 2022, mabehewa 45 yaliyobakia yanategemewa kukamilika Machi, 2023.”

Kisha aliigeukia Bandari na kuwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu huo kuwa Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam na Tanga na pia katika Ziwa Tanganyika kwenye Bandari za Kibirizi mkoani Kigoma, Karema mkaoni Katavi na Kabwe mkoani Rukwa ili kuongeza ufanisi katika huduma.

Kwamba hadi Oktoba, 2022 ujenzi wa gati namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam unaohusisha kuongeza kina, kujenga gati maalumu (RoRo berth) ya kuhudumia meli za magari na kujenga yadi ya kuhudumia makasha (container yard) umekamilika na vile vile, Serikali imeboresha Bandari ya Tanga kwa kuongeza kina cha lango la kuingilia na kugeuzia meli.

Akifafanua zaidi kuhusu bandari alisema; “Serikali imeendelea na upanuzi wa Bandari ya Kibirizi, Kigoma ili kuchochea biashara na nchi jirani za Congo (DRC), Zambia na Burundi. Pia ujenzi wa Bandari ya Kabwe mkoani Rukwa umekamilika na utakuwa kivutio kikubwa cha biashara baina ya Wilaya ya Nkasi na eneo la Moba nchini Congo.

“Pia ujenzi wa Bandari ya Karema iliyopo mkoani Katavi umekamilika na imeanza kutumika. Ujenzi wake umegharimu Shilingi bilioni 47.9, ukihusisha ujenzi wa kivunja mawimbi, mlango bandari na gati ya meta 150 zenye uwezo wa kulaza meli zenye urefu wa mita 75 na upana wa meta 15, uchimbaji na uwekaji wa kina wa mlango wa bandari, jengo la ofisi, jengo la abiria na shehena ya jumla.”

Bandari la Karema iliyopo Mkoa wa Katavi.

Waziri Mkuu Majaliwa aliutaja usafiri wa anga kuwa miongoni mwa sekta zilizoguswa kimafanikio na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Alisema Serikali imeendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Songea mkoani Ruvuma na Nduli mkoani Iringa.

‘Kwa uwanja wa ndege wa Songea, ujenzi na ukarabati wa jengo la kuongozea ndege upo katika hatua za mwisho na wanakamilisha uwekaji wa taa ili kuwezesha ndege kutua usiku. Katika kiwanja cha ndege cha Nduli upanuzi wa kiwanja hicho unahusisha ujenzi wa barabara za kutua na kurukia ndege.

“Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili liweze kutoa huduma bora za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi. Hivi sasa limefanikiwa kuanza safari za Arusha, Geita na kurejesha safari za Mtwara na Songea.

“Pia limerudisha safari za kikanda katika vituo vya Bujumbura, Entebbe, Harare, Lusaka na Hahaya pamoja na kuanzisha vituo vipya vitatu katika miji ya Lubumbashi, Nairobi na Ndola. Vile vile, Shirika limerejesha safari ya kimataifa kwenda Mumbai, India pamoja na kuanzisha safari za mizigo na abiria kuelekea Guangzhou – China.”

Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATLC)

Na kuhusu usafiri wa majini alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu ambao umefikia asilimia 73. Pia ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika na meli mpya ya kubeba mabehewa (wagon ferry) katika Ziwa Victoria unaendelea.

Kwenye sekta ya nishati alisema pamoja na miradi mingine inayoendelea katika sekta hiyo ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project – JNHPP) unatarajiwa kuzalisha MW 2,115, umefikia asilimia 77.15.

Sekta ya utalii nayo ni moja ya sekta ambazo zinakibeba zaidi CCM kwa wananchi kutokana na kukua kwake kwa kasi na mchango wake kwa uchumi wa Taifa na kwa mtu mmoja mmoja kama alivyoainisha Waziri Mkuu Majaliwa alipowaeleza wajumbe wa mkutano mkuu wa 10 wa CCM kuwa, “utalii ni sekta muhimu kwa uchumi yenye mchango mkubwa katika pato la Taifa.

“Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kulinda na kuhifadhi rasilimali na kuendeleza utalii nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza na kutangaza vivutio vya utalii.

“Takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa sekta ya utalii inazidi kuimarika zaidi hususan baada ya uzinduzi rasmi wa programu maalumu yaThe Royal Tour uliofanyika tarehe 19 Aprili, 2022 nchini Marekani.

“Hadi kufikia Septemba 2022, takwimu zinaonesha kuwa watalii wanaokuja nchini Tanzania wameongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 na kufikia 1,034,180. Pia, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 ambazo ni sawa na Shilingi trilioni 1.6 kwa mwaka 2020 na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na Shilingi trilioni 3, katika mwaka 2021.

“Novemba 2022, Tanzania ilipokea meli kubwa ya kitalii ya Zaandam kutoka Florida, Marekani ikiwa na watalii 1,060 kutoka mataifa ya Marekani na Ulaya na wafanyakazi 520 kutoka mataifa 35 duniani.

Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiandaa sinema ya Royal Tour

“Vivutio vya utalii tulivyonavyo vimeifanya sekta hii kuwa mhimili muhimu wa uchumi na sasa Tanzania imeanza kuwa kitovu cha utalii wa mikutano (conference tourism) ambapo hivi karibuni tumeweza kuwa wenyeji wa mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani – Kamisheni ya Afrika. Pia tulikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Mikutano hii ilifanyika jijini Arusha.

Serikali itaendelea kuongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa na kuibua masoko mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini hadi kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.

“Ili kulinda ikolojia na uoto wa asili katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), Serikali imefanikiwa kuwaratibu wakazi wanaohama kwa hiari katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga.

“Utaratibu wa kuandikisha wakazi wanaoomba kuhama kwa hiari unaendelea vizuri. Aidha, hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2022 jumla ya kaya 1,524 zenye watu 8,715 na mifugo 32,842 zilikuwa zimekwishajiandikisha.

“Aidha, kati ya tarehe 16 Juni, 2022 na tarehe 15 Novemba, 2022 makundi 16 yenye kaya 489 zenye watu 2,629 na mifugo 14,132 zilikuwa zimeshahamia katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni. Katika maeneo ambayo wakazi hao wamehama kwa hiari, uoto umeanza kurejea katika hali ya awali huku wanyama wakiongezeka na watalii wanaotembelea eneo hilo pia wameongezeka.”

CCM pia kinabebwa na utekelezaji wa miradi mikubwa mitano ya maji ambayo Waziri Mkuu Majaliwa aliiweka bayana mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM aliposema; “Katika kuimarisha sekta ya maji nchini, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama.

“Hadi kufikia Oktoba 2022, ujenzi wa miradi mikubwa mitano ya Tabora, Igunga, Nzega; Orkesumet; Kagongwa, Isaka; Longido na Misungwi imekamilika. Aidha, vijiji 171 vilivyopo kandokando ya miradi hiyo, vimeunganishwa na huduma ya maji.

Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiongoza mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikweye, jijini Dodoma hivi karibuni

“Juni 6, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji ya miji 28. Miji itakayonufaika na miradi hiyo ni Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa-Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Chunya, Rujewa, Wangingo’mbe, Makambako, Njombe, Kiomboi, Singida, Manyoni na Chemba.

“Miji mingine ni Chamwino, Mugumu, Kasulu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga pamoja na ukanda wa Makonde.

“Utekelezaji wa miradi hiyo ni mojawapo ya mikakati ya Serikali ya kusambaza maji safi na salama maeneo ya mijini na vijijini. Aidha, kiwango cha upatikanaji wa majisafi na salama mijini kimeongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2020 hadi asilimia 86 mwaka 2022 na vijijini kutoka asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 74.5 mwaka 2022.”

Katika hili, Waziri Mkuu Majaliwa alimalizia kwa kummwangia sifa Rais Samia kwa kuridhia zitolewe Shilingi bilioni 100 kati ya Shilingi bilioni 329ili kuanza utekelezaji wa mradi wa maji unaotarajiwa kuchukua miezi 36 hadi kukamilika na kwamba sambamba na mradi huo, Serikali inaendelea na taratibu za awali za ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 292 ili kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma na miji ya Bahi, Chemba na Chamwino.

Utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya Serikali kuhamia Dodoma nao ni ajenda muhimu iliyomo kwenye kete za CCM. Hili Waziri Mkuu Majaliwa alilieleza hivi. “Serikali ilifanya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani Dodoma. Ili kutimiza azma hiyo, Shilingi bilioni 300 zilitolewa kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa Mji wa Serikali unaohusisha majengo ya ofisi yenye urefu wa ghorofa kuanzia sita hadi 11 ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya CCM kuhakikisha Serikali inahamishia shughuli zake makao makuu ya nchi, jijini Dodoma.

Ujenzi huo ambao umefikia asilimia kati ya 50 na 70 unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2023 na utaenda sambamba na uwekaji wa miundombinu ya maji, umeme, mawasiliano, usalama, gesi, TEHAMA, zimamoto na uokoaji na programu za upandaji miti.

Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

“Lengo ni kuwa na Mji wa Serikali wa kisasa utakaozingatia dhana ya mji wa kijani na mji rafiki ili kudhibiti gharama za uendeshaji. Ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 51.2 katika eneo hilo umekamilika kwa asilimia 99.

“Sambamba na hatua hizo, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji yenye urefu wa kilometa 112.3 ambapo sehemu ya Nala, Veyula, Mtumba, Ihumwa, Dry Port ni kilometa 52.3na sehemu ya Ihumwa Dry Port, Matumbulu, Nala nikilometa60. Ujenzi huu utakapokamilika, utakuwa umegharimu Shilingi bilioni 230.4.

“Ili kuboresha Jiji la Dodoma kwa mawasiliano ya anga, Serikali imeanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambapo barabara ya kuruka na kutua ndege imeanza kujengwa na ili kuhakikisha shughuli zote za Serikali zinafanyika makao makuu ya nchi, kwa dhamira ya dhati kabisa, Serikali iliamua kujenga Ikulu mpya ya Chamwino, Dodoma. Na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.”

Sensa ya watu na makazi inabebwa na CCM kwa sura mbili, ya kwanza kama moja ya mafanikio kiliyoyafikia katika utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi na pili kama jambo la kihistoria kililolifanikisha ambalo litabaki kwenye kumbukumbu za mambo muhimu ya nchi kwa miaka mingi ijayo.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Sensa ya Watu na Makazi, Oktoba 31, 2022.

Historia ya Tanzania sasa inasomeka kuwa mwaka 2022, Tanzania ilifanya Sensa ya watu na makazi ambayo ilizinduliwa Oktoba 31, 2022 na Rais wa Awamu ya Sita na pia Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan ambayo matokeo yake yalionyesha kuwa idadi ya watu Tanzania ni 61,741,120, kati ya hao watu 59,851,347 wapo Tanzania Bara na watu 1,889,773 wapo Zanzibar. Kwa upande wa majengo yapo 14,348,372, kati ya hayo, 13,907,951 yapo Tanzania Bara na 440,421 yapo Zanzibar.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya