SIMBA GEMBAGU NGW’ANA NJAMITI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza mwisho wa safari yake ngumu ya miaka mitano. Safari hiyo ya jasho na damu ilianza mwaka 2020 ikiwa inaelekea mwaka 2025.
Tangazo la kufika mwisho wa safari hiyo ngumu ya utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025 ambayo CCM kilianza kuitekeleza katika Ilani yake ya mwaka 2020, limetolewa mwishoni mwa wiki hii na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, uliopo jijini Dodoma.
Katika dira ya Taifa ya maendeleo ya 2020 hadi 2025, CCM kimeielekeza Serikali kutekeleza maeneo makuu sita ya kipaumbele. Maeneo hayo ni kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa, kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.
Pia kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu maendeleo ya uchumi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini.
Maeneo mengine ni kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi na kutengeneza ajira zisizopungua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.
Katika taarifa yake ya kuelekea mwisho wa safari ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa inayoisha mwaka 2025 ambayo Waziri Mkuu Majaliwa aliitoa kwenye mkutano mkuu huo wa 10 wa CCM, anataja maeneo yote sita ambayo CCM kiliielekeza Serikali kuyatekeleza kikamilifu kuwa utekelezaji wa maagizo hayo umekuwa na mafanikio makubwa, akianza na ukusanyaji wa mapato kisha elimu, kilimo na huduma za ugani, kukuza demokrasia na uhusuano wa kimataifa.
Kuhusu ukusanyaji mapato, anasema Serikali ilianza utekelezaji wa mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026) ukiwa na dhima ya kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu.
Anasema uamuzi wa Serikali kutoa uhuru wa ulipaji kodi kwa hiari umewezesha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali uliofikia wastani wa Shilingi trilioni 1.74 kwa mwezi ikilinganishwa na Shilingi trilioni 1.46 kwa mwezi mwaka 2020/2021 na kuhusu mfumiko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kubaki kwenye tarakimu moja.
Eneo la pili analolizungumzia ni elimu ambako Serikali inaendelea na mpango wa kutoa elimu ya msingi na sekondari bila ada, ikiwemo ada za mitihani lakini pia kuimarisha uandikishaji na uhitimu wa wanafunzi shuleni.
Katika elimu, jitihada za Serikali kutekeleza maelekezo ya CCM zimewesha kupatikana fedha za kujenga vyumba vya madarasa 12,000 katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa3,000 na kufanya wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa saba mwaka 2021 kupata nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza Januari, 2022 bila kuwa na chaguo la pili.

Taarifa ya Waziri Mkuu Majaliwa inaeleza zaidi kuwa mafanikio yaliyofikiwa na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu ni ujenzi wa shule za wasichana katika mikoa yote 26 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,200 wa mchepuo wa sayansi na kwanmba huo ni mpango mkakati wa Serikali inapotekeleza dira ya Taifa ya maendeleo ya 2020 hadi 2025 wa kuongeza fursa kwa watoto wa kike.
Katika mpango mkakati huo, Waziri Mkuu Majaiwa anamtaja kwa shukrani Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutenga Shilingi bilioni nne kwa kila shule kwa mikoa 10 ya kwanza nchini katika bajeti ya mwaka huu na sasa ujenzi wa shule hizo unaendelea.
Na kuhusu elimu ya juu, anasema Serikali imeendelea kugharamia elimu hiyo ambapo katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2022, imetoa mikopo ya Shilingi trilioni 1.03 kwa wanafunzi 327,175 wa vyuo vya elimu ya juu.
Kilimo na huduma za ugani ni eneo la tatu alilotaja kuwa na mafanikio makubwa ambako kumefanyika maamuzi ya kimapinduzi kwa kuridhia ongezeko la bajeti ya kilimo kutoka Shilingi bilioni 294mwaka 2021/2022 hadi Shilingi bilioni 954kwamwaka 2022/2023.
Kuthibitisha usahihi wa ripoti yake hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa anawageukia wajumbe wa mkutano mkuu huo na kuwakumbusha kuwa Aprili 4, 2022 mkoani Dodoma, Rais Samia alikabidhi vitendea kazi kwa maafisa ugani zikiwemo pikipiki 2,000, vifaa vya kupima afya ya udongo 143, simujanja 384 na visanduku vya ufundi 3,400 na aidha, ili kuhakikisha upatikanaji wa mbolea na kuongeza tija katika uzalishaji kwa wakulima, ruzuku ya Shilingi bilioni 150 imetolewa kwa lengo la kushusha bei ya mbolea.
Eneo la nne alilolitaja ni kukuza demekrasia ambapo alieleza kuwa demokrasia ina misingi na taratibu ambazo Taifa husika limejiwekea na kwa hapa nchini mazingira mazuri ya demokrasia na siasa yaliyowekwa na Serikali yanajidhihirisha kupitia sera ya upatanishi, kuvumiliana, kuishi pamoja na kujenga nchi ambayo Rais Samia ameipa jina la R4; maani yake kwa kimombo ni Reconciliation, Resiliency, Reforms and Rebuilding of the nation.

Na mwisho, Waziri Mkuu Majaliwa alizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ya 2020 hadi 2025 kuwa ni kuimarishwa kwa uhusiano na mataifa ya nje yakiwemo mataifa jirani na hasa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kuimarika kwa uhusiano kuliwafanya baadhi ya marais na wakuu wa nchi kutembelea Tanzania na anataja Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuwa wa kwanza katika orodha hiyo.
Wengine aliowataja ni Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri Kidemokrasia ya Congo, Rais Filippe Nyusi wa Msumbiji, Rais Evariste Ndayishimye wa Burundi, Rais Hakainde Hichilema wa Zambia) na Rais William Ruto wa Kenya.
Katika hilo, alisema Rais Samia naye amefanya ziara katika nchi za Marekani, Ubelgiji, Ufaransa, Qatar, Uganda, Ghana, Uingereza, Msumbiji, China, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Scotland, Malawi, Rwanda na Burundi.