Wednesday, June 18, 2025
spot_img

UTATU WA KIFO CHA KANUMBA – 8

The Trinity of Steven Kanumba’s Death

HAMEES SUBA

0672 86 65 74

ILIPOISHIA

MAJIRA ya saa sita usiku nilimpigia simu muigizaji Jacob Stephen, maarufu kwa jina la JB nikiwa na taarifa kuwa yeye na Vicent Kigosi, anayefahamika kwa jina la kisanii kama Ray, ndiyo walioupeleka mwili wa marehemu Steven Kanumba Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhiwa.

JB alinithibitishia kwamba ni kweli marehemu Kanumba amefariki na wao wako Hospitali ya Taifa Muhimbili wakishughulika kuuingiza mwili wa nguli huyo wa filamu mochwari. Nikawa sasa nina jeuri ya kuwasambazia wenzangu taarifa za uthibitisho wa kifo cha marehemu Kanumba.

SASA TUUNGANE NAYO

Tukiweka pembeni suala zima la mazishi na mwitiko wa watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa namna walivyopokea taarifa za kifo hicho, jambo jipya liliibuka kutoka kwa baba yake Kanumba, mzee Charles Kusekwa Kanumba.

Licha ya kifo cha marehemu Kanumba kuwagusa watu wengi wakiwemo watu kutoka mataifa ya jirani, Mzee Charles Kusekwa hakuonekana kuguswa sana na kifo hicho hasa pale aliposusa kushiriki kwenye mazishi ya mwanaye.

Kwa mujibu wa mama Kanumba, walimtumia Mzee Charles Kusekwa usafiri wa kutoka Shinyanga hadi Mwanza na tiketi ya ndege kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam lakini mzee huyo aligoma kunyanyua mguu wake kwenda kumzika mwanaye

Jitihada mbalimbali zilifanyika kumshawishi mzee huyo kushiriki kwenye mazishi ya mwanaye lakini hazikufua dafu kwani msimamo wake ulibaki pale pale kwamba hatoshiriki.

Mwisho wa siku ukoo akamteua aliyekuwa Mbunge wa Maswa, John Shibuda kumwakilisha mzee Charles Kusekwa kwa niaba ya familia katika mazishi hayo. Taarifa za ndani zilieleza kwamba Mzee Kanumba aligoma kuhudhuria kwenye mazishi hayo kutokana na mambo makuu matatu.

Mosi; Kitendo cha Kanumba kumdhalilisha hadharani kwa kuieleza jamii kuwa alikuwa akinyanyasika mbele ya macho yake na yeye kama mzazi au kiongozi wa familia hakuchukua hatua zozote kumlinda.

Pili; kitendo cha Kanumba kuongozana na watu wasiokuwa wa ukoo wake kwenda kutambika kwenye kaburi la babu yake bila kuzingatia mila na taratibu za kisukuma.

Tatu; nadhiri aliyokuwa ameweka mzee Kanumba kutokana na kitendo cha Kanumba ‘kumfumua’ hadharani, jambo ambalo lilihesabiwa kama chukizo kwenye ukoo. Tuchambue hoja moja baada ya nyingine.

Siku za hivi karibuni kumekuwepo tabia ya vijana wanaopata umaarufu wakiwa chini ya malezi ya upande mmoja, hasa upande wa mama kujitokeza hadharani na ‘kuwabutua’ wazazi wao wa kiume kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwalea au kuwahudumia walipokuwa wadogo.

Zamani tabia hii haikuwepo na ilichukuliwa kwamba kumsema vibaya mzazi wako awe baba au mama yako kwa namna yoyote ile hata kama hakukusaidia chochote katika maisha ni sawa na kujitafutia laana.

Tamaduni nyingi za kiafrika ziliamini katika mfumo huo wa kuheshimu wazazi hata kama walikukosea. Lakini kwa sasa mambo ni tofauti, hakuna mtoto anayejali tena laana ya mzazi ambaye hakumuwajibikia.

Kinachoaminika ni kwamba kila mtu atakula kwa jasho lake. Usiposhiriki msimu wa kilimo hupaswi kushiriki msimu wa mavuno. Waliolima pamoja ndiyo watakaokula pamoja.

Ukweli ni kwamba marehemu Kanumba baada ya kumsema vibaya baba yake aliumia moyoni, jambo hilo lilimuuma sana mzee huyo. Inaelezwa kuwa amewahi kusikika akisema anatamani siku zirudi nyuma wakati ule Flora Mtegoa alipokuwa na ujauzito wa marehemu Kanumba ili aiharibu mimba iliyokuwa tumboni mwake asijezaliwa mtoto wa aina ya Kanumba.

Marehemu Steven Kanumba akiwa na msanii maarufu wa Nigeria Ramsey Noah

Kingine alichokuwa akilalamika mzee huyo ni kitendo cha kudhalilishwa mke wake wa ndoa wakati marehemu Kanumba alikuwa mtoto wa nje ya ndoa. Hata kitendo cha marehemu Kanumba kumuita mke wa baba yake mama wa kambo, mzee Charles Kusekwa hakukipenda kabisa na alisikika akilalamika juu ya jambo hilo huku akisema kilidhamiria kuhalalisha madai yake kwamba alikuwa akiteswa na mama huyo.

Ikumbukwe kuwa mama yake marehemu Kanumba ndiye alikuwa mchepuko wa Mzee Charles Kusekwa kwani mzee huyo wakati anakutana na mama Kanumba, tayari alikuwa na mke wa ndoa na watoto.

Kwa tafsiri nyingine ni kwamba mama Kanumba ndiye ‘aliyeintafia,’ aliyeingilia mapenzi ya mke halali wa mzee Charles Kusekwa. Mama Kanumba amewahi kukiri kwamba alikuwa mchepuko wa mzee Charles Kusekwa na hakuwahi kuolewa naye.

Pia kitendo cha marehemu Kanumba kueleza kwamba baba yake na mama yake walitengana wakati akiwa darasa la nne kilichukuliwa na mzee Charles Kusekwa kama kutaka kuwalaghai watu na kumhalalisha mama yake kuwa alikuwa mke halali wa mzee huyo.

Mara kadhaa wazee wa kisukuma wenye ukaribu na mzee Charles Kusekwa walikuwa wakielezea kitendo alichokifanya marehemu Kanumba kwa baba yake kuwa ni cha fedheha na utovu wa nidhamu uliopitiliza. Kwa hiyo kutokana na mazingira hayo, mzee Kanumba alihuzunika, alifedheheka, alipatwa na aibu na kubaki na donge moyoni.

Hoja ya pili; marehamu Kanumba kwenda kutambika kwenye kaburi la babu yake bila kuzingatia taratibu za kimila za wasumuma. Kama mtakumbuka kule nyuma marehemu Kanumba alisema anajua ugumu uliopo katika safari yake ya kwenda kuaga kwao lakini atafanya kila awezalo kutekeleza jambo hilo.

Haikuwa safari ya kuaga tu bali ilihusu kwenda kutambika pia. Sasa alichokifanya marehemu Kanumba kwa kuwa hakuwa na maelewano mazuri na baba yake akaamua kuunda msafara wake uliowahusisha watu hawa; mdogo wake aliyeitwa Seth Bosco (hivi sasa naye ni marehemu), mjomba wake na shemeji yake.

Alipofika Shinyanga akamtafuta ndugu mmoja wa upande wa baba akampa mshiko ndiyo akakubali kuwapeleka lilipo kaburi la babu yake marehemu Kanumba, kwenda kutambika.

Kwa haraka ukiangalia hiyo ‘listi’ aliyoongozana nayo marehemu Kanumba utaona kwamba imeegemea zaidi upande wa mama kuliko upande wa baba. Tukianza na mjomba ambaye ni kaka wa mama, Seth Bosco ambaye ni mdogo wake marehemu Kanumba (mtoto wa mdogo wake mama Kanumba na shemeji ambaye ni mume wa dada yake marehemu Kanumba.

Ndugu toka upande wa baba aliyekuwepo naye alikuwa wa mchongo kwa maana hakuwa na kibali wala ridhaa ya ukoo wa mzee Kanumba kwenda kwenye kaburi la baba yake mzee Charles Kusekwa ambaye ndiye babu yake marehemu Kanumba. Kwa mtaji huo lolote lingeweza kutokea.

Hebu tumuangalie babu yake marehemu Kanumba alikuwa na uzito gani kwa marehemu Kanumba; Taarifa za kiukoo zinaeleza kuwa zamani marehemu Kanumba alipokuwa mdogo kulitokea kutoelewana kati ya mama Kanumba na Mzee Charles Kusekwa, hali iliyosababisha kutikisika kwa ndoa ya mzee Charles Kusekwa.

Baada ya mzee Charles Kusekwa kuona ndoa yake iko mashakani alimshauri mama Kanumba kumchua mwanae na kuondoka kabisa Shinyanga. Mama Kanumba kwa shingo upande alichukua mbeleko na kujitwisha mwanae mgongoni kisha akasafiri toka Shinyanga hadi kwao Bukoba na kuanzisha makazi mapya.

Akiwa huko, mtoto (Kanumba) alianza kuumwa, aliugua sana, mama Kanumba alijaribu tiba za hospitali zikadunda, akaingia kwenye mitishamba nako akachemka, ikabidi awasogelee wazee wa jadi, walipotizama ‘satelite’ zao wakagundua shida ipo Shinyanga kwa baba wa mtoto.

Ikabidi ‘wamchane’ mama Kanumba kuwa mtoto hawezi kutibika popote zaidi ya kwao, yaani kwa baba yake. Hivyo anapaswa kurudi alikotoka kumrejesha mtoto kwa baba, yeye ndiye anayejua pa kwenda kumtibu.

Presha ikampanda Flora lakini akaona akipuuzia maneno ya watu wazima atamkosa mwanaye. Hakupenda jambo hilo litokee, haraka akaandaa safari na kurudi Shinyanga.

Alipofika Shinyanga akamsimulia mzee Charles Kusekwa yote yaliyomfika. Mzee Kusekwa bila hiyana akampokea mwanaye, marehemu Kanumba na kumruhusu mama Kanumba kwenda. Hapo ndipo mzee Charles Kusekwa akamchukua Kanumba mpaka kwa baba yake, yaani babu yake Kanumba.

Babu alipomshika mtoto akamtazama tangu unyayoni hadi utosini kisha akagundua kinachomsumbua na namna ya kumtibu. Ikafungwa safari ya mbali na mji hadi katikati ya msitu mkubwa, huko kikajengwa kibanda kwa ajili ya tiba. Kanumba akaingizwa ndani ya kibanda hicho na kukaa kwa siku kadhaa akifanyiwa tiba.

Ndani ya kibanda hiki ndipo asili ya jina Kanumba lilipoanzia. Inaelezwa kuwa kwa lugha ya kisukuma Kanumba maana yake ni kajumba, yaani kile kibanda tiba kilimoofanyiwa kazi ys kumtibu marehemu Kanumba.  Kwa maana kuwa kile kibanda kilichotumika kufanyia Tina ya Kanumba.

Hapa tunapata kufahamu kuwa Kanumba halikuwa jina halisi la ukoo wao bali ni jina lililotokana na tiba hiyo. Baada ya kumalizika kwa tiba hiyo, ndipo Steven Charles Kusekwa akabatizwa jina jipya la Kanumba; Tangu hapo mzee Charles Kusekwa naye akaongeza urefu wa jina lake na kuwa Charles Kusekwa Kanumba.

Hoja ya tatu; Nadhiri aliyokuwa amejiwekea mzee Charles Kusekwa Kanumba. Hii ni sababu ya tatu inayotajwa kusababisha mzee Charles Kusekwa kushindwa kuhudhuria mazishi ya mwanaye.

Inaelezwa kuwa baada ya kuhitilafiana na marehemu Kanumba kutokana na ile ‘intavyuu’ aliyofanya na Zamaradi, mzee Charles Kusekwa alijiapiza kutoshiriki katika jambo lolote litakalomuhusu marehemu Kanumba. Kwa hiyo mpaka siku marehemu Kanumba anakufa alikuwa hajaitoa nadhiri hiyo.

Kwanini wazee wa kisukuma na baadhi ya watu wanahusisha kifo cha marehemu Kanumba na ukiukwaji wa mila na tamaduni?

Jambo la kwanza wazee wa mila za kisukuma wanaamini kuwa marehemu Kanumba alikufa akiwa hana radhi ya baba yake. Hii inatokana na mapito yote niliyoyaelezea tangu kuruka kwa mahojiano ya marehemu Kanumba na Zamaradi yaliyolenga kumdhalilisha mzee Charles Kusekwa.

Jambo la pili, marehemu Kanumba asingemjua babu yake bila uwepo wa baba yake. Tiba aliyofanyiwa marehemu Kanumba kule msituni ilikiwa ya jadi na ilitokana na mkono wa baba yake. Kitendo cha kumruka baba yake na kuunda msafara wa ‘kihuni’ kwenda kuchukua baraka kwenye kaburi la babu ni ukiukwaji wa mila za kisukuma.

Wazee wa mila wanasema kuwa huwezi kupata baraka za ukoo kwa kumdharau baba yako aliyekuingiza katika ukoo. Wako wanaoamini kwamba kama marehemu Kanumba angelifuata taratibu sahihi za kimila, ikiwemo kumuheshimu baba yake, basi kifo kisingemchukua.

Marehemu Steven Kanumba akiwa Hollywood, Marekani

Wengine wanasema kwamba ni heri angelisafiri ‘kavu kavu’ bila kwenda kutambika angeweza kuyanusuru maisha yake kuliko alichokifanya.

“Mila zipo na zina nguvu sana, lakini pia kaburini si sehemu ya kuchezea. Tambiko lina utaratibu wake na kama utakosea lazima madhara yawepo, huwezi kwenda kutambika kihuni ukatoka salama hata siku moja,” anasema Mzee Bubinza ambaye ni msukuma wa Katoro, Geita.

Ukweli ni kwamba wazo la marehemu Kanumba kwenda kutambika kwenye kaburi la babu yake sijui alilitoa kwa nani? Sina maana kuwa ni wazo baya kwa sababu kila mtu ana mila za kwao lakini kwanini alifanya mambo ya hatari kirahisi sana? Hili ndio swali la kujiuliza.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya