RIPOTA PANORAMA- DODOMA
MAADHIMISHO ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambayo yangegharimu Shilingi milioni 960 yamefutwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza fedha hizo kupelekwa Wizara ya Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Uamuzi huo wa Rais Samia umetangazwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene alipokutana na waandishi wa habari na kueleza kuwa fedha za maadhimisho hayo zilizoelekezwa kwenye wizara hiyo na Rais Samia zilitengwa na wizara na taasisi mbalimbali.
Waziri Simbachawene amesema Rais Samia ameelekeza fedha hizo kutumika kujenga mabweni katika shule nane za msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambazo alizitaja kuwa ni Shule za Msingi Buhangija iliyoko Mkoa wa Shinyanga, Goweko ya mkoani Tabora, Darajani ya mkoani Singida, Mtanga na Songambele zilizoko Mkoa wa Lindi, Msanzi ya mkoani Rukwa, Idofi ya Mkoa wa Njombe na Longido ya mkoani Arusha.
“Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu 2022 yatafanyika kwa midahalo na makongamano katika wilaya zote hapa nchini kujadili na kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulikotoka, tulipo na tunakoelekea kuhusu maendeleo endelevu ambayo nchi yetu adhimu ya Tanzania imeyafikia.
“Siku hiyo hakutakuwa na gwaride na shughuli nyingine za kitaifa. Kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru ni amani na umoja ni nguzo ya maendeleo yetu.
“Makongamano hayo yatatanguliwa na ratiba mbalimbali kwa viongozi wa mikoa na wilaya kufanya shughuli za kijamii kama vile usafi katika maeneo ya hospitali, shule, nyumba za wazee na makundi yenye mahitaji maalum,” amesema Simbachawene.