Wampa siku 14 kulipa, akikaidi kuburuzwa mahakamani
RIPOTA PANORAMA
MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amepewa siku 14 kuwalipa Shilingi milioni 10.1 wahariri wa waandishi wa habari waliokuwa wakifanya kazi katika gazeti lake la LAJIJI.
Kwa mujibu wa barua ya madai iliyoandikwa na Kampuni ya Mawakili ya Haki Kwanza na kusainiwa na Wakili Kiongozi wa kampuni hiyo, Aloyce Komba, Jaji Mutungi amepewa siku 14 kuwalipa waliokuwa wahariri na waandishi wa habari wa gazeti lake hilo kiasi hicho cha fedha ambazo ni malimbikizo ya mishahara yao wanayomdai.
Barua hiyo ya Disemba 2, 2022 ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeoina ina Kumb. Na. HKA/JIJI/ ECHO/MSHAHARA, 2022/1 na inawataja wahariri na waandishi wa habari wanaodai malimbikizo ya mishahara yao kwa Jaji Mutungi kuwa ni Eckland Mwaffisi, Zahoro Mlanzi, Salha Mohamed, Sarah Mazengo, Bright Mduma na Penford Wangeleja.
Wakili Komba anaandika katika barua hiyo kuwa Jaji Mutungi amekataa kulilipa deni hilo bila sababu zozote za msingi wa kisheria akitambua kuwa anavunja sheria za ajira na nchi kwa makusudi wakati yeye ni mwanasheria mwenye hadhi ya ujaji.
Kwamba Jaji Mutungi ni kiongozi ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye kiapo cha viongozi wakuu wa taasisi za umma, uaminifu kwa Katiba ya nchi, utii na maadili ya uongozi wa umma.
“Iwapo hutalipa fedha yote kwa mkupuo ndani ya muda tuliokupatia, tumeagizwa na wateja wetu tukuchukulie hatua za kisheria hususan kukushtaki mahakamani kwa kesi ya madai ambayo utalipa fedha nyingi zaidi.
“Fedha hiyo itajumuisha riba ya kimahakama, usumbufu uliowafanyia wateja wangu kiasi cha wao wenyewe na familia zao kukosa mahitaji muhimu, gharama za kesi, nafuu nyingine ambazo mahakama itaona inafaa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Akizungumzia na Tanzania PABORAMA Blog leo kuhusu madai hayo, Mwaffisi amesema yeye binafsi alianza kumkumbusha Jaji Mutungi juu ya deni hilo kuanzia Agosti 28, 2021. “Nilianza kazi Gazeti la LAJIJI Mei, 2019 na kuacha kazi Septemba, 2021 baada ya Jaji Mutungi kushindwa kunilipa mshahara wangu kuanzia Novemba, 2020.
“Ilipofika Novemba, 2021 alipunguza deni la Novemba-Disemba, 2020 kwa wafanyakazi wote baada ya baadhi ya wafanyakazi kulalamikia malimbikizo ya mshahara wao kwenye Mtandao wa Jamii Forum.”
Mwaffisi amesema baada ya Jaji Mutungi kupunguza deni hilo, aliendelea kumkumbusha ili aweze kumalizia pesa wanazomdai kupitia simu yake ya mkononi (WhatsApp). “Awali Jaji Mutungi alikuwa akionyesha ushirikiano kwa kutoa ahadi ya kulipa deni letu lakini baadaye aliamua kukaa kimya kila nilipomkumbusha.
“Kutokana na usumbufu huo, ilipofika Februari 10, 2022 niliuandikia barua uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na barua yangu niliielekeza kwa Waziri na Katibu Mkuu ili waingilie kati jambo hilo.
“Uongozi wa wizara uliahidi kufuatilia jambo hilo na ilipofika Juni 4, 2022, wizara ilisema malalamiko hayo ni madai hivyo ilishauri jambo hilo lifikishwe mahakamani ili wafanyakazi waweze kupata stahiki zao ndiyo maana kupitia mwanasheria wetu, amemuandikia barua Jaji Mutungi na kumpa siku 14 awe ametulipa pesa zetu, asipotulipa tutakwenda mbele zaidi,” amesema.
Aidha, Mwaffisi amesema wakati yeye na wenzeke wakiendelea kudai malimbikizo ya mishahara yao, Jaji Mutungi aliendelea kuchapa Gazeti la LAJIJI zaidi ya miezi mitatu mfululizo bila kujali deni alilokuwa akidaiwa na wafanyakazi.
Amesema gharama za uchapaji zilikuwa sh. 1,050,000 kwa kopi 3,000 mbali na gharama za usafirishaji gazeti mikoani.