RIPOTA PANORAMA
MAMBO ni magumu kwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kipindi hiki linapokabiliwa na madai ya kutumia ‘njia za panya’ kuipatia Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited, leseni ya kufanya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena.
TASAC ni mdhibiti wa masuala yahusuyo shughuli na biashara za usafirishaji baharini, na moja ya majukumu yake ni kukagua eneo na vifaa vya biashara linaloombewa leseni kabla ya kutoa leseni.
Pia kuhakikisha eneo husika na wahusika wana vigezo vilivyowekwa na kuhakikisha muombaji anavyo vifaa kama vile vya kupokea na kupakia kontena kabla ya kutoa leseni.
Katika skandali hii, TASAC inadaiwa kutoa leseni ya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena kwa Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited huku ikiwa haina vifaa vya kupokea na kupakia kontena na aidha;
Inadaiwa, TASAC ilitoa leseni hiyo bila kufanya ukaguzi kwenye eneo ambalo Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited iliomba kufanyia biashara; aneo ambalo kuna biashara nyingine ya uhifadhi wa kontena tupu za wenye meli.
Novemba 28, 2022 Tanzania PANORAMA Blog ilifika ofisini kwa Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Abdul Mkeyenge ikiwa imefumbata maswali mawili mkono kuhusu ukiukwaji huo wa uratatibu wa utoaji leseni uliofanywa na ofisi yake kwa ajili ya kumuuliza naye ayajibu na kukutana na Katibu Muhtasi wake ambaye alieleza kuwa bosi wake hayupo lakini mwenye dhamana ya kujibu maswali ya waandishi wa habari kwa niaba ya bosi huyo ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Habari na Mawasiliano, Josephine Bujimu.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Bujimu alisema ni vizuri akatumiwa maswali hayo kwenye simu yake ya kiganjani ili atakapomaliza kikao ayajibu; “Nimetoka kwenye kikao kuja kuwasikiliza kwa sababu bosi hayupo na idara yangu ndiyo yenye dhamana ya kushughulika na ninyi kwa niaba ya bosi.
“Mimi ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Habari na Mawasiliano, niwaombe mnitumie hayo maswali kwenye simu yangu nikimaliza tu kikao nitayajibu kwa sababu sasa sina muda kwa kweli bado nipo kwenye kikao cha menejimenti,” alisema Bujimu.
Tanzania PANORAMA Blog ilimtumia maswali Bujimu kama alivyoomba, maswali hayo yalisomeka hivi; Salamu Josephine. Rejea mazungumzo yetu ya leo mchana ofisini kwako. Hapa tunawasilisha kwako maswali machache ambayo majibu na au ufafanuzi wake utatumika kihabari.
Tanzania PANORAMA Blog inatambua kuwa moja ya majukumu ya TASAC ni kukagua na kutoa leseni kwa kampuni zinazotaka kufanya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena. 1) zipo taarifa kuwa TASAC imetoa leseni kwa Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited ikiiruhusu kufanya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena katika eneo ambalo kuna biashara nyingine inayoendelea. Taarifa hizi zina ukweli kiasi gani?
Swali la pili lilisomeka; Moja ya mahitaji muhimu ambayo TASAC walipaswa wahakikishe Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited imeyatimiza kabla ya kuwapatia leseni ni kuwa na vifaa vya kupakia na kupokelea kontena ambavyo kampuni hiyo haina, Je? TASAC ilizingatia hilo kabla ya kutoa leseni hiyo?
Novemba 29, 2022 mapema saa 1.26 asubuhi, Bujimu aliandika kukiri kupokea maswali hayo. Aliandika hivi; “Nimepokea. Asante sana …. Good morning.” Baada ya kutuma ujumbe huo hakupatikana tena licha ya kukumbushwa mara kadhaa kujibu, lakini kila simu yake ilipoita, haikupokelewa.
Machi 30, 2022 Tanzania PANORAMA Blog iliendelea kumtafuta Bujimu bila mafanikio kwani licha ya simu yake kuita lakini haikupokelewa na Disemba Mosi, 2022 alipopigiwa kwa namba nyingine ya mtandao wa tigo alipokea kwa bashasha lakini baada ya kuelezwa kuwa anazungumza na Tanzaniaa PANORAMA Blog, alipunguza sauti na kuwa ya chini sana kisha akasema yupo kwenye kikao hawezi kuongea lakini majibu yapo tayari hivyo baada tu ya kikao atayatuma.
Bujimu hakutuma majibu kama alivyoahidi na tangu siku hayo hajapokea tena simu ya Tanzania PANORAMA Blog wala kujibu ujumbe alioandikiwa.

Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited ni Kampuni dada ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) yenye ubia na Serikali wa kuendesha Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Company Limited (MECCO.) Katika ubia huo, SISICOL ina hisa asilimia 75 na Serikali ina hisa asiimia 25.
SISICOL ambayo ina jukumu la uendeshaji wa shughuli za kila siku za MECCO ilifanya hila ikapoka sehemu kubwa ya hisa za Serikali na kuibakiza hisa asilimia 2.6 pekee kabla ya hila hizo kujulikana na Serikali kuchukua hatua ya kuzirejesha hisa zake.
Mbali na hila hiyo, mbia huyo wa Serikali alipora ardhi na mali za umma katika MECCO ambapo abadilisha umiliki wa hati za viwanja vya MECCO, kiwanja namba 2 na kiwanja namba 3B ambavyo alivihamishia kwenye umiliki wake kisha akaenda Benki kuchukua mkopo wa mabilioni ya shilingi ambao inadaiwa kuwa haujalipwa mpaka sasa.
Kampuni ya SISICOL inamilikiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya kisomali, Abdulkadir Mohamed anayedaiwa kutumia majina ya baadhi wa viongozi wa Serikali na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutekeleza hila mbalimbali zenye lengo la kumnufaisha binafsi na inaelezwa kuwa kwenye uendeshaji wa MECCO ameweka watu ambao wamekuwa wakichukua maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwake ya kutekeleza hila mbalimbali ikiwemo hii inayoihusisha TASAC.
Mwenyekiti wa MECCO, Kwabhi Maungo katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni alisema wanajiandaa kujibu mapigo mbele ya mkutano mkubwa wa waandishi wa habari dhidi ya yale yaliyoelezwa na Serikali kuhusu hila ambazo wamekuwa wakizifanya dhidi ya mali za umma wa Watanzania. Hata hivyo hakusema mkutano uo utafanyika lini.