Monday, December 23, 2024
spot_img

UTATU WA KIFO CHA KANUMBA – 5

The Trinity of Steven Kanumba’s Death

HAMEES SUBA

0672 86 65 74

ILIPOISHIA

HASARA za kulazimisha lugha usiyoifahamu ni kujinyima fursa ya kueleza hisia zako kwa mapana unayoyataka. Pia, hukunyima fursa ya kujua kwa usahihi kile unachoulizwa. Hicho ndicho kilichotokea kwa Kanumba kwani swali aliloulizwa alilijibu tofauti kabisa.

Habari ya tatu kunikosanisha na Kanumba ikatoka hapa. Je, ilikuwa habari gani?

TUUNGANE NAYO

GAZETI la Kiu ya Jibu likaandika habari yenye kichwa kisemacho; “Big Brother yamuumbua ‘BOGASI KANUMBA!’” ashindwa kuongea Kiingereza cha darasa la nne.

Baada ya kutoka kwa habari hiyo mgogoro wangu na Kanumba ukaongezeka maradufu. Aliporejea nchini tu, siku ya pili yake akawasiliana na mwanasheria wake wakaleta ‘demand notes’ ya kuishtaki Kampuni ya Kiu Investment iliyokuwa ikichapisha magazeti ya Kiu ya Jibu na sambamba na hilo, ilikuwa kunishtaki mimi binafsi.

Kesi ilikwenda mahakamani lakini Kanumba hakupata kuhudhuria hata mara moja. Ikafika kipindi na sisi kama Kiu ya Jibu tukawa hatuhudhurii mahakamani hivyo kesi ikawa inatajwa tu bila mlalamikaji wala mlalamikiwa kuwepo mahakamani.

Ukapita mwaka wa kwanza, wa pili ukaingia kisha mwaka wa tatu bila kusikikizwa kwa kesi hiyo. Ndipo siku moja Kessa akanifuta na kuniambia ameongea na Kanumba amesema hana nia tena ya kuendelea na kesi ile na hata wakili wake ameshamweleza.

Pia akaniambia Kanumba anataka tukutane kwa ajili ya kuondoa tofauti zetu na kurejesha urafiki wetu kama mwanzo. Hiyo ndiyo sababu ya mimi kwenda ofisini kwa Kanumba nikiwa nimeongozana na Kessa siku hiyo.

Turudi kwenye mada sasa.

Tukiwa ofisini hapo tulipiga stori nyingi sana na kukumbushana mambo yaliyopita. Baada ya muda kidogo Kanumba akatutaka tutoke nje ya ofisi yake tukakae kwenye gari lake alilokuwa akilitumia kwa ajili matangazo na kazi za ‘lokesheni’ aina ya Hiace Super Custom. Tulifanya hivyo.

Tukiwa ndani ya gari hilo, Kanumba akasema; “Ogaa kuna jambo nataka niwaambie ndio maana nimewatoa pale ofisini ili nanyi mnipe ushauri.” Nikamuuliza; “jambo gani?” akasema; “Unajua mimi nimepitia mateso mengi sana udogoni kwangu.”

Nikamuuliza; “Kivipi?” akaanza kutiririka akisema; “Maisha yangu ya utotoni yalikuwa ya mateso baada ya wazazi wangu kutengana, nilionja joto ya jiwe kwenda kuishi kwa baba aliyekuwa na mke mwingine jambo hilo lilinikosesha furaha na amani ya utotoni.”

Alisema kuwa wazazi wake walitengana akiwa anasoma darasa la nne ndiyo sababu ya yeye kuishi na mama bila baba.“Nilikuwa naishi na mama, nilitamani sana kumjua baba yangu, nilimsumbua mama mpaka akanionyesha baba yangu ndipo nikaenda kuishi naye, wakati huo nilikuwa nampenda sana baba yangu.

“Mwanzo tuliishi kwa furaha na baba yangu pamoja na mama wa kambo lakini kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele ndipo kibao kilianza kunigeukia na kujikuta nikiingia kwenye ukurasa mpya wa mateso.

“Nilikuwa nikiamshwa asubuhi na mapema na kutumwa kuchota maji, nikirudi naambiwa niwatoe mbuzi kwenda kuwafunga kwenye malisho, nikitoka huko natakiwa kuosha vyombo.

Nikimaliza kazi hizo ndipo nijiandae kwenda shule, sisi tumesoma kipindi cha viboko, ukifika shule unakutana na mwalimu wa zamu unachapwa bakora, mwalimu wa darasa naye anakupa adhabu kwa kuchelewa kipindi chake.

“Unajua Shinyanga kuna shida kubwa sana ya maji, niliporudi nyumbani kutoka shuleni nilitakiwa kwenda kuchota tena maji. Nilipewa toroli na madumu kibao kwenda kuchota maji. Mateso yote hayo niliyapata huku baba akishuhudia lakini hakuchukua hatua zozote kuninusuru.

“Pale nyumbani tulikuwa na jalala la kutupia taka, siku moja mama aliniambia niwapelekee mbuzi maganda ya viazi lakini kwa kuona kuwa mbuzi wale walikuwa wameshiba na ilikuwa usiku nikaona bora niyatupe kwenye jalala la pale nyumbani.

“Mama alipogundua nimefanya hivyo hakujali kama ni usiku, akanishurutisha niingie shimoni na kuyatoa yale maganda ya viazi na kuwapelekea mbuzi, nilitumbukia mle jalalani kukiwa na giza na kuanza kuyakusanya maganda yote ingawa nilikuwa sioni kutokana na giza.

“Baba alipita pale aliposikia minong’ono alidhani ni paka akataka kunirushia jiwe lakini kabla ya kurusha, aliwasha tochi akaniona, aliniuliza nilikuwa nafanya nini nikamweleza lakini hakuchukua hatua zozote.”

Kanumba aliendelea kusimulia kuwa baada ya mama yake kupata taarifa za mateso yote anayoyapitia ndipo ikamlazimu kumchukua na kwenda kuishi naye. “Siku moja mama alikuwa anakwenda harusini na wenzake akaniona nikichunga mbuzi mchana wa jua kali, alijisikia vibaya sana, baada ya kuona mateso yamezidi ndipo akaamua kunichukua moja kwa moja.”

Akasema baada ya kuondoka kwa mama wa kambo alijitahidi sana kumshawishi mama yake awasiliane na baba yake ili wasaidiane kumsomesha lakini baba yake aliendelea kuwa kichwa ngumu. “Ilifika hatua mama aliamua kumshtaki baba Ustawi wa Jamii lakini walipotoka kwenye shauri, hakuniambia nini kilichokuwa kinaendelea.

“Nilijitahidi kutaka kujua lakini mama hakuthubutu kuniambia zaidi ya kusisitiza kwamba atanisomesha mwenyewe. Nilishindwa kuelewa lakini siku nikiwa nacheza nje nilimsikia mama kupitia dirishani akiongea na wanawake wenzake kwamba baba yangu amesema kuwa hawezi kumsomesha jambazi, yaani mimi aliniita jambazi.

“Akadai kuwa mimi nilikuwa nikimuibia mama yangu wa kambo fedha lakini yote hayo najua alikuwa akijazwa upepo na mama yangu kambo.”

Marehemu Steven Kanumba

Baada ya Kanumba kueleza hayo nilimuuliza maswali mawili. Stori yake ilinisikitisha kwa namna fulani lakini kwa kuwa vitu vingi alivyovizungumza havikuwa vigeni sana hasa kwa mtoto aliyeishi na mzazi ambaye si wake.

Nikamuuliza maswali haya. Swali la kwanza; “Kwanini umefikiria kuyasema mambo haya sasa na hukuwahi kuyasema huko nyuma?” Swali la pili; “Unahisi ukiyaweka hadharani mambo haya utapata faida gani na ukiyapotezea utapata hasara gani?”

Akajibu; “Ogaa unajua sasa hivi mimi ni mtu wa tofauti sana, nimekuwa mtu wa kusoma sana vitabu lakini vitabu vya watu wenye fikra pevu (great thinkers), kwa hiyo nimebadikika sana ndiyo maana hata wewe nimekuita ili tumalize tofauti zetu kwa sababu najua wewe ni miongini mwa watu wenye mchango mkubwa sana katika mafanikio yangu, sasa kugombana na watu waliokusaidia ni sawa na kugombana na mafanikio yako, sipendi kuwa mtovu wa fadhila kwako.”

Nilimuelewa kuhusu alichoongea juu yangu lakini bado sikumwelewa kuhusu dhamira yake ya kutaka ‘kumfumua’ baba yake mzazi. Nikarudia kumuuliza kuhusu faida na hasara za kutaka kuyaweka mambo yale hadharani.

Akasema; “Katika vitabu nilivyosoma pia nimesoma kitabu cha Martin Luther King, kuna mahali anasema ‘only truth shall set you free’ (kweli itakuweka huru) kwa hiyo na mimi naamini kabisa katika hicho alichokisema, nataka kuwa mkweli.

“Kitendo cha baba yangu kufumbia macho mateso niliyokuwa nayapata kwa mama wa kambo kimekuwa kikinisumbua moyoni kwa muda mrefu kwa hiyo ili niwe huru ni lazima nitoe moyoni kile kinachonisumbia.”

Nikamwambia hilo neno unalolizungumza hata kwenye Biblia Takatifu lipo, ukitazama Yohana 8:31-32 utakutana na hilo neno lakini kumbuka yule ni mzazi wako hata kama amekukosea bado ni mzazi tu pia usisahau kuwa wewe sasa hivi ni staa, jambo dogo tu litageuka kuwa kubwa, huoni kama itakuletea shida kwenye ukoo wako?”

Kanumba akajibu; “Ogaa umezungumza vizuri sana, tena kumbe hata Biblia imezungumza habari hiyo sasa kwanini nihofie kuzungumza ukweli wakati ni agizo la Mungu hata kama ukoo utanikasirikia?”

Nikamwambia; “Kuna neno pia linasema ‘si kila neno husemwa popote’ tafakari kwa kina juu ya jambo hilo.” Akasema; “Hilo neno limeandikwa wapi Ogaa maana sasa unataka kujichanganya?”

Nikamwambia; “Ni katika vitabu hivyo hivyo vya dini japo sikumbuki ni kitabu gani nilisoma neno hilo?” Akaniuliza; “Ogaa kumbe na wewe unapenda kusoma vitabu, umewahi kumsoma mwanafalsafa yeyote au great thinker yeyote?”

Nikamwambia kuhusu wanafalsafa nimewahi kusoma baadhi ya ‘do trine’ zao hasa wanafalsafa kama Plato, Aristotle, Karl Max. Heraclitus, Zeno of Elea n.k.

Akacheka sana kisha akasema; “Basi uko vizuri Ogaa, mimi mbali na kumsoma Martin Luther King nimemsoma kidogo Malcolm X na Mahatma Gadhi, lakini Plato na Aristotle nimewasikia ila sijawahi kuwasoma nataka nijitahidi kadri nitakavyoweza niwasome wote hao.”

Tuliendelea kupiga stori mbili tatu lakini mwisho wa yote nilimsisitiza sana kuachana na dhamira ya kumuanika baba yake kwa yale mambo aliyoyaeleza. Nikamsisitiza kuwa kusamehe ni bora zaidi kuliko kulipa kisasi na hasa ukizingatia yeye alishatoka kwenye shida na tayari Mungu alishamjalia kipaji cha uigizaji kilichokuwa kinamuendeshea maisha.

Mwisho wa siku Kanumba alituelewa na kukubali kuachana na dhamira ya ‘kumchana live’ baba yake kwenye vyombo vya habari. Tulifunga kikao chetu rasmi lakini kablà hatujaachana akaniambia alikuwa na ratiba mbili za kwenda kutoa misaada kwa wasiojiweza, moja kwenye kituo cha kulea watoto yatima pale pale Sinza Mori jirani na ofisi yake na nyingine kwenye kituo cha walemavu wenye ukoma kule Vijibweni Kigamboni. Akaniomba nishiriki kwenye matukio hayo yaliyokuwa chini ya uratibu wa Steps Entertaiment.

Sikuwa na jinsi zaidi ya kumkubalia hivyo tuliaanza na kile kituo cha watoto yatima pale Sinza kisha tukaelekea Kigamboni kwenye kituo cha pili cha watu wenye ukoma.

Urafiki wangu na Kanumba ukawa umerejea upya na wakati tunakwenda Kigamboni alipanda kwenye gari yangu. Shughuli zote mbili zilikwenda vizuri na kumalizika kama zilivyopangwa ndipo tukaachana.

Lakini katika hali ya kushangaza, jioni ya siku hiyo hiyo nilikuwa naangalia Televisheni ya Clouds FM, kipindi cha Take One kinachoendeshwa na Zamaradi Mketema nikastaabu kuoma mahojiano ya Kanumba na Zamaradi ambapo Kanumba alikuwa ‘akimchana live’ baba yake kwa mistari ile ile aliyokuwa akitueleza. Nilishtuka sana, muda huo huo nikachukua simu na kumpigia Kaanumba.

Simu yangu haikupokelewa. Nikarudia tena na tena lakini bado simu haikupokelewa. Nikajua hapokei kwa sababu anajua nitakuwa natazama kipindi hicho na kushuhudia yale yote tuliyomkataza akiyangurumisha hewani.

Nikajisemea; “Atajua mwenyewe kwani uamuzi wa kusuka au kunyoa ni wake, sisi ni washauri tu.” Nilikitazama kipindi hicho mwanzo mpaka mwisho ambapo nilimsikia Kanumba akifunguka bila aibu wala woga akimchana baba yake. Kuna sehemu alikiri waziwazi kumpenda mama yake kuliko baba yake.

Nanukuu; “Samahani sana najua hata baba anaweza kuwa anaangalia kipindi hiki lakini ukweli ni kwamba nampenda mama kuliko baba yangu.”

Kama hiyo haitoshi akaongeza; “Baba yangu alianza kunitafuta baada ya kuwa maarufu, lakini mimi nilishawasamehe yeye pamoja na mama yangu wa kambo, kwani hadi sasa huwa nawasiliana nao kwa simu, nawasaidia panapowezekana.”

Sikuwa na jinsi ya kuzuia tena jambo hilo kwani lilishatekelezeka. Siku ya tatu tangu kurushwa kwa kipindi hicho ndipo nikipokuja kumpata Kanumba baada ya kumpigia simu na kupokea. Licha ya kuwa mimi ndiye mpigaji wa simu lakini alipopokea tu yeye ndiye akawa mzungumzaji wa kwanza.

Akaanimbia; “Ogaa samahani sana kwa kutopokea simu zako lakini najua uliona intrerview yangu na Zamaradi ndiyo maana ukawa unanipigia, kifupi ni kwamba wakati nakusimulia yale mambo siku zile nilikuwa tayari nimesharekodi kipindi na Zamaradi kwa hiyo hakukuwa na namna ya kuzuia kipindi kisirushwe wakati walishapoteza muda na kipindi kilishaingizwa kwenye ratiba ya kurushwa siku hiyo.”

Alitoa maelezo mengi ya kujitetea kuhusu jambo hilo lakini kwangu hayakuwa na maana yoyote kwani yalikuwa masuala yake na familia yake. Mimi nikamuuliza; “Vipi mrejesho wa watazamaji baada ya kutazama mahojiano hayo?”

Akajibu; “Ukweli mashabiki na watu wengi wamenipigia simu na kunipongeza sana, wameniambia ni kitendo cha kijasiri nilichokifanya na wamefurahishwa kwa mimi kuwa muwazi na mkweli, kwa hiyo mrejesho ni mzuri kabisa.”

Nikamuuliza; “Kwa upande wa baba yako mrejesho ukoje?” Akasema; “Sijapata simu toka upande huo najua watakuwa wamenuna lakini potelea mbali, mimi jambo langu limetimia.”

Je, Nini kilifuatia usikose kufuatilia makala hii ya UTATU WA KIFO CHA KANUMBA ikiwa inaelekea ukingoni.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya