Monday, December 23, 2024
spot_img

UTATU WA KIFO CHA KANUMBA – 4

The Trinity of Steven Kanumba’s Death

HAMEES SUBA

0672 86 65 74

ILIPOISHIA

WAKATI tukisubiri andiko hilo unaweza kuingia YouTube kisha search headline hii; Aliyekuwa mwanachama wa Freemason ajisalimisha kwa Kuhani na Mwalimu Musa Mwacha, utajionea jinsi Kairuki na rafiki yake Kuhani Mwacha wanavyoichezea madhabahu ya Mungu.

Matukio ya Kairuki ni mengi sana, hayawezi kuisha hapa hivyo tuhame huko na turejee kwenye mada yetu.

Kwa hiyo basi dhana ya Steven Kanumba kuuawa na Freemason ilitokana na mapitio hayo ambayo kimsingi ni ya kupuuzwa na kukemewa kwa nguvu zote.

SASA TUENDELEE

Dhana ya tatu ya kifo cha Kanumba inajengwa na ukiukwaji wa Mila na Matambiko. Lipo kundi kubwa linaloamini kwamba kilichomuua Kanumba ni kujichanganya katika utekelezaji wa matambiko ya kwao (upande wa baba) kwa maana ya matambiko ya kisukuma. Pia inaelezwa kuwa Kanumba aliegemea kwenye mila za Kihaya (upande wa mama) wakati si asili yake.

Kundi hili si la kubezwa wala kupuuzwa kwa sababu ukifuatilia hoja zao na matukio ya mwisho ya siku za Kanumba unaweza ukapata kitu cha kutia mfukoni.

Ikoje sasa? Kabla sijakupa hoja na sababu za msingi za waamini wa kundi hili ngoja nikupe kisa kimoja cha nyongeza ili twende vizuri. Mwezi Februari, 2012 ikiwa ni miezi miwili tu kablà ya kifo cha Kanumba, nilikutana na Kanumba katika ofisi yake iliyokuwa Sinza Mori jirani na baa ya Meeda jijini Dar es Salaam.

Nilikuwa nimeongozana na rafiki yangu aitwaye Kessa Mwambeleko aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Sani. Madhumuni ya safari hii ilikuwa kwenda kumaliza tofauti baina yangu na Kanumba ambazo zilidumu kwa takribani miaka mitatu.

Kablà ya uwepo wa tofauti hizo Kanumba alikuwa rafiki yangu sana. Siwezi kuelezea ni namna gani urafiki wetu ulivyokuwa lakini yatosha kusema alikiwa mtu wangu sana. Ukaribu wetu ndio ikawa sababu ya kumfanyia promosheni nyingi sana kupitia magazeti yetu la Kiu ya jibu.

Aliyesababisha mimi na Kanumba kuwa marafiki wa karibu ni mdau mmoja wa filamu anayejulikana kwa jina la McDonald Mwakamele. Kipindi hicho McDonald alikuwa katika mgogoro mkubwa sana na waigizaji wawili wa filamu, Blandina Chagula maarufu kama Johari na Vincent Kigosi almaarufu kama Ray.

Mgogoro wao ulitokana na mapenzi kwa upande mmoja na upande mwingine ulisababishwa na wizi wa filamu ya Revenge iliyoigizwa na wasanii hao wawili kwa mfuko wa McDonald. Hivyo basi kutokana na mgogoro huo ndipo McDonald akaona amalizie hasira zake kwa kuwekeza fedha nyingi ‘kumpromoti’ Kanumba wakati huo huo ‘kum-demoti’ Ray.

Hapa ndipo urafiki baina yangu na Kanumba ukawa kama ule wa suruali na mkanda kwani jukumu la kumpromoti Kanumba nikakabidhiwa mimi na Mhariri mwenzangu Oscar Ndauka. Tuyaache hayo.

Kessa Mwambeleko ndiye aliyekuwa kiunganishi cha kutuunganisha upya mimi na Kanumba. Sababu ya kuingia katika mgogoro wangu na Kanumba ilitokana na habari tatu nilizoziandika na kuchapishwa katika gazeti la Kiu ya Jibu kumuhusu Kanumba.

Habari ya kwanza ilihusu safari yake ya Marekani mwaka 2008 ambapo akiwa huko alituma picha kwenye baadhi ya magazeti (sio Kiu) zikimuonyesha ameshika tuzo. Gazeti moja likaandika kichwa cha habari kisemacho; ‘Kanumba apewa tuzo Marekani.’

Habari ya pili ilihusu picha nyingine alizotuma Kanumba akiwa huko huko Marekani zikimuonyesha akiwa ndani ya Helikopta. Gazeti jingine likaandika habari yenye kichwa kisemacho; ‘Kanumba aendesha helikopta Marekani.’

Picha aliyopiga marehemu Steven Kanumba akipewa tuzo nchini Marekani

Wakati habari hizo zinatoka sisi marafiki zake (Kiu ya Jibu) hatukupewa habari yoyote kuhusiana na kinachoendelea kuhusu Kanumba huko Marekani. Ilikuwa nadra sana kwa gazeti letu kutopata ‘updates’ za msanii kama Kanumba ambaye alikuwa haishi kuandikwa kwenye magazeti yetu, tena kwa mambo mazuri tu.

Baada na habari hizo kutoka bila sisi kuwa na ‘updates’ zozote kuhusu Kanumba ilileta mshtuko mkubwa ‘newsroom’ na kusababisha sisi wenye ukaribu na Kanumba kuulizwa maswali. Nakumbuka moja ya swali nililoulizwa kwenye kikao cha newsroom (post Moterm) ni hili; “Kiongozi hata wewe mtu wake umeshindwa kupata taarifa zozote kuhusu kinachoendelea Marekani?” Ukweli sikuwa na jibu zaidi ya kuona aibu.

Lakini baada ya kutafakari kwa sekunde chache nikapata cha kujitetea. Nikakiambia kikao hivi; ‘Kuna uwezekano hizi taarifa zimetumwa kwenye e-mail yangu lakini sijaingia kwenye e-mail takribani wiki sasa, password yangu ina shida ila nitajaribu kuiweka sawa ili niweze kuifungua na kuangalia kama kuna taarifa zozote kisha nitawajulisha.’

Walioamini waliamini, waliobaki na yao moyoni nao walibaki nayo lakini kilikuwa kikao kilichonisumbua sana. Kikao kilifanyika kwa sababu kulikuwa na ushindani wa kisoko kwenye magazeti ya udaku, habari mpya za wasanii wakubwa ndio zilikuwa msingi mkubwa wa mauzo katika soko. Wasanii wa filamu walikuwa juu kuliko wanamuziki na habari zao ndizo zilikuwa zinauza zaidi.

Baada ya kumalizika kwa kikao hicho sikuwa na haja ya kwenda kuchungulia kwenye e-mail yangu kwa sababu ni asubuhi tu nilishaitazama na hakukuwa na chochote kipya. Nilikuwa na uhakika Kanumba hakunitumia taarifa yoyote kuhusiana na mambo yake huko Marekani.

Kama rafiki, kama mtu niliyekuwa nikimpambania wakati wote nilijikuta moyo ukisema; ‘Rafiki leo kanivua nguo.’ Ukweli iliniuma! Lakini mwisho wa yote nikajiambia moyoni kwamba nitaandika habari kupitia habari hizo hizo zilizokwishatoka kwa ‘engo’ yangu binafsi.

Mchana ulifika, baadaye jua likazama, siku ikapita. Asubuhi ya siku iliyofuata niliwahi sana ofisini kwa ajili ya kuyapitia yale magazeti yaliyotoa habari za Kanumba akiwa Marekani ili niweze kujua nini ninachoweza kukiongeza katika habari hizo walau na sisi tuonekane tuko na wakati.

Lakini kabla sijagusa gazeti lolote wazo lingine likanijia kwamba niingie kwenye e-mail yangu ‘niperuzi’ kuona labda kuna chochote kipya kimetumwa. Nilipofungua tu e-mail nikakutana na ‘dodo’, sina maana ya embe, nazungumzia mkeka lakini sio ule wa ‘kubeti’.

Ilikuwa ni ripoti mpya iliyotumwa na mtu aliyejitambulisha kama msomaji wa magazeti yetu akielezea kusikitishwa na zile habari zote zilizoandikwa na magazeti kuhusu Kanumba na kinachoendelea Marekani.

Taarifa hiyo iliambatana na zile picha zilizotoka kwenye magazeti mengine na nyongeza ya picha ambazo hazikutumwa kwenye magazeti hayo kama vielelezo vya taarifa hiyo mpya.

Kikubwa ni kwamba mtumaji wa ripoti hiyo alisema habari zote zilizotoka kwenye magazeti hazikuwa za kweli kwa maana kwamba Kanumba hakupewa tuzo yoyote nchini Marekani wala hakuwahi kuendesha Helikopta.

Ripoti hiyo ikabainisha kuwa alichofanya Kanumba ni kununua kinyago (trophy) mtaani kisha akamuomba mzungu mmoja apige naye picha huku akimkabidhi. Maelezo yake yalikwenda sambamba na picha za ushahidi alizotutumia. Maana yake ni kwamba Kanumba alinunua ile ‘trophy’ na kutengeneza tukio hilo kwa makusudi ili kutengeneza ‘kick’ akijua watu hawataweza kujua ukweli.

Tuzo ya Marehemu Steven Kanumba

Mtu huyo akataka Kanumba aulizwe tuzo aliyopewa inaitwaje, ni ya nini? waliompa ni akina nani? Alishindanishwa na wasanii gani na hapa nchini filamu gani iliyomfanya awanie tuzo hiyo? Maswali yote hayo hayakuwa na majibu.

Kuhusu kuendesha Helikopta Marekani mtu huyo alisema jambo hilo halipo kabisa na kilichofanyika ni kile kile cha kuomba kupiga picha ndani ya Helikopta na kutuma picha nchini kwa ajili ya habari.

Mwisho, mtu huyo akaomba gazeti letu litumie maelezo yake na picha alizotumaa ili jamii ipate kujua ukweli wa taarifa hizo. Kwa kuzingatia maombi ya mtu huyo na vithibitisho alivyovitoa ndipo tukaandika habari yenye kichwa kisemacho; ‘Kanumba aumbuka. *Adai kupewa tuzo Marekani kumbe ni kinyago alichonunua mtaani.

Kuhusu habari ya Helikopta tukaandika; ‘Dunia yamshangaa kanumba. *Ni kwa kujifunza kuendesha Helikopta kwa sekunde mbili.’

Habari zikatoka, mjini pakawa pazito, taarifa zikamfikia Kanumba akiwa bado Marekani. Nikaanza kupata taarifa mbaya kutoka kwa watu waliokuwa wakiwasiliana na Kanumba toka Marekani kwamba akitua Bongo ama zake ama zangu. Tayari nikawa adui rasmi, urafiki wetu wa kama suruali na mkanda ukaingia doa. Ukweli ukanipomza, ningefanya nini? sikuwa na cha kufanya.

Kanumba aliporejea kila nilipompigia simu zangu hakupokei, nikaona isiwe tabu nami nikaazimia kumchunia. Kama mbwai na iwe mbwai.

Mwaka uliofuta 2009 Kanumba akapata zari jingine la kualikwa Big Brother msimu wa nne, (BBA Season IV) nchini Afrika Kusini. Alialikwa kama mkaazi nyota (housemate) wa jumba hilo. Akiwa huko akapata nafasi ya kuhojiwa ‘live’ kwenye Televisheni ya BBA, mahojiano ambayo yalifanyika kwa Lugha ya Kiingereza.

Katika mahojiano hayo Kanumba aliboronga mambo mengi sana kwa kile kilichoonekana ni kutojua vema kuzungumza Lugha ya Kiingereza, yaani aliongea ‘broken english’ ya kutosha katika mahojiano hayo.

Kama unavyojua kosa dogo kwa staa kihabari ni jambo kubwa, Gazeti la Kiu ya Jibu likaona hiyo ni habari ya kuandikwa na ikibidi kujadiliwa. Mantiki haikuwa kwanini ameshindwa kuongea Kingereza kizuri kwenye mahojiano hayo bali ilikuwa kwanini alilazimisha kuongea Kingereza ambacho hakifahamu vizuri wakati alikuwa na fursa ya kuomba mkalimani kama mastaa wengine wanavyofanya.

Hasara za kulazimisha lugha usiyoifahamu ni kujinyima fursa ya kueleza hisia zako kwa mapana unayoyataka. Pia kukunyima fursa kujua kwa usahihi kile unachoulizwa. Hicho ndicho kilichotokea kwa Kanumba kwani swali aliloulizwa alijibu vitu tofauti kabisa na alivyoulizwa.

Habari ya tatu kunikosanisha na Kanumba ikatoka hapa. Je, ilikuwa habari gani?ITAENDELEA KESHO, HAKIKISHA UNAFUNGUA tanzaniapanorama.co.tz KUENDELEA KUSOMA DHANA YA TATU YA KIFO CHA KANUMBA

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya