Tuesday, December 24, 2024
spot_img

UTATU WA KIFO CHA KANUMBA – 3

The Trinity of Steven Kanumba’s Death – 3

HAMEES SUBA

0672 86 65 74

ILIPOISHIA

MIONGONI mwa matukio ya hatari aliyowahi kuyafanya Kairuki ni pamoja na kujisingizia kifo kwa minajili ya kujipatia pesa na umaarufu.

Tukio lenyewe lilikuwa hivi; Alipiga picha akiwa ndani ya jeneza mithili ya mtu aliyekufa na kuwatuma washirika wake wazisambaze kwenye vyombo vya habari na kudai kuwa Freemason wamemuua. Lengo lilikuwa taarifa hizo zikishasambaa, baadaye ajitokeza hadharani na kuilaghai jamii kwa mara nyingine kuwa ameyashinda mauti.

Tukio hili alilifanya mwaka 2013 akiwa na dhamira ya kuanzisha kanisa endapo ‘dili’ lake ‘lingetiki’ lakini kwa bahati mbaya janja yake ilibainika kutokana na upungufu uliokuwemo ndani ya picha za maiti yake.

TUENDELEE

Wataalamu wa picha waliweza kubaini upungufu mwingi katika picha iliyokuwa ikimuonyesha Kairuki akiwa ndani ya jeneza kama marehemu. Miongoni mwa upungufu huo ni kukosekana kwa pamba za pua na masikioni kama ambavyo maiti nyingi huonekana zikiwa na pamba katika maeneo hayo.

Lakini pia sura ya marehemu Kairuki ilionekana ikiwa na tabasamu tena la kupendeza tofauti na ilivyozoeleka kwenye muonekano wa maiti nyingi, sura hupoteza tabasamu na mvuto. Jambo lingine ni mdomo kutofunga vizuri kama maiti nyingi zinavyoonekanaga zikiwa zimefumba mdomo kisawasawa lakini kama hiyo haitoshi, hata ukaaji wa mwili wa Kairuki ndani ya jeneza ulitia shaka.

Ukaaji wake ndani ya jeneza ulionekana ni wa kuigiza na sio halisi kama maiti inavyokuwa ndani ya jeneza. Kimsingi ni kwamba picha hazikukidhi viwango vya uhalisia wa maiti katika jeneza.

Tukio hili la kifo cha Kairuki lilisambaa kwenye vyombo vingi vya habari na kuripotiwa. Hapa nitavitaja baadhi vilivyoripoti tukio hili la kushangaza na kustaajabisha kuwahi kutokea hapa nchini Tanzania.

Jamii Forum iliripoti tukio hili baada ya mtumiaji mmoja wa mtandao huo kutaka kujua kama kweli Nabii Kairuki alifariki dunia au la. Uki-google na ‘kusechi’ maneno haya; “Ni kweli mchungaji aliyetoa siri za Kanumba alishafariki?”

Utaunganishwa na mtandao wa Jamii Forum na kukutana na taarifa hizo na majibu yake. ‘Post’ hiyo iliwekwa tarehe 31 Agosti, 2013 na mtu aliyeuliza swali hilo akitaka kupata ufafanuzi.

Lakini pia ukiingia kwenye blogu iitwayo Irene Mwamfupe Jamii Blog tukio hili liliripotiwa kwa kupewa kichwa cha habari kisemacho; ‘aliyedai Kanumba freemason adaiwa kufa ghafla.’

Stori yao iliripoti tukio hilo kama ifuatavyo; “Kifo chake kilifanana na kifo cha Kanumba na kwa mujibu wa chanzo cha habari hiyo, siku ya tukio zilisikika kelele ndani ya chumba alichokuwa akiishi na baada ya muda alitoka mwanamke na kutokomea kusikojulikana.

“Hatukujua kilichotokea, tulipoingia ndani tukakuta George amekufa, ndipo taratibu za mazishi zilipofanyika.”

Yaani Kairuki aliiga mpaka staili ya kufa kama Kanumba alivyokufa. Eti, zilisikika kelele halafu mwanamke akatoka ‘nduki’ na kutokomea kusikojulikana.

Washirika wa George Kairuki wakiwa wamebeba jeneza lake

Ikumbukwe kuwa mara baada ya Kanumba kufariki, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu alichoropoka nyumbani kwa Kanumba na kutokomea kusikojulika ndiyo maana naye akapitia njia ile ile ya kusema baada ya kusikika kelele za umauti alitoka mwanamke ndani ya kile chumba na kutokomea kusikojulika.

Blogu nyingine iitwayo tumsifu-thegreat.blogspot iliripoti tukio hili kama ilivyoripotiwa kwenye blogu Irene Mwamfupe lakini wao wakibadili kichwa cha habari na kusema; ‘aliyepigilia msumari Kanumba Freemason afariki ghafla.’

Hata hivyo, pamoja na kuripotiwa kote huko kuhusu kifo cha Kairuki, siku chache baadaye siri ilifichuka na habari zikaanza kuwa kinyume zikimuumbua na kumsuta Kairuki kuhusu udanganyifu wake.

Baada ya Kairuki kuona ‘kimenuka’ akabadili ajenda na kuibuka tena na utetezi kwamba picha hizo zilipigwa wakati akiigiza filamu yake kuhusu Freemason.

Swali la kujiuliza ni hili? Tangu mwaka 2013 lilipotokea tukio hilo hadi leo ni miaka tisa imepita, nani aliyewahi kuiona filamu aliyoigiza Kairuki kuhusu maisha yake na Freemason? Jibu; haikawahi kuwepo filamu kama hiyo hapa duniani.

Pamoja na yote hayo Kairuki bado aliendelea kumsakama marehemu Kanumba kuwa alikufa akiwa mwanachama wa Freemason na ili kujiwekea ulinzi akajisingizia kuwa walikuwa pamoja katika chama hicho. Ujasiri wa kusema uongo wote huu ni kwa sababu Kanumba hayupo nasi tena, hakuna awezaye kuurejesha uhai wake ili aje kujitetea.

Hali hii ilisababisha Blogu ya Swahili Cinema News kushindwa kulivumilia jambo hilo na kuamua kulikemea hadharani. Februari 19, 2013 blogu hiyo iliandika habari yenye kichwa kisemacho; ‘mchungaji bado amwandama Kanumba.’ Iliripotiwa kama ifuatavyo;

‘Kitendo cha baadhi ya wananchi kutumia jina la msanii aliyefariki kujipatia kipato au umaarufu ni kitu kibaya, kinachotakiwa kupigwa marufuku na kuwakamata wahusika na kufikisha mbele ya vyombo vya sheria.

‘Swahili Cinema News imeshuhudia mtu anayejiita Mchungaji George Kairuki akitumia jina la marehemu Steven Kanumba kujipatia umaarufu katika kiwanja kilichokuwa Buguruni Chama, karibu na shule ya msingi, pamoja na kituo cha basi.

‘Mchungaji huyo aliibuka mara baada ya kifo cha Marehemu Kanumba na kueleza kuwa marehemu alikuwa muumini wa Freemasons, madai ambayo hakuna aliyekuwa na uhakika nayo.

‘Hata hivyo, kwa akili za kawaida madai hayo kwa sasa hayana umuhimu wowote, hakuna anayetaka kufahamu kama alikuwa muumuni wa Freemasons kwa sababu haisaidi chochote hata watu wakifahamu.

‘Kikubwa anachofanya mchungaji huyo ni kujitafutia umaarufu kupitia mgongo wa marehemu Kanumba, taarifa ambazo kwa upande mwingine zinaonyesha kumjenga kwa kumpatia umaarufu ili watu wajiunge na kanisa lake.

‘Kama lengo ni kutoa taarifa za marehamu Kanumba kujiunga na Freemasons, alikwishatoa baada ya kifo chake, vyombo vya habari viliandika na kutangaza.

‘Kwa hiyo hana sababu ya kuendelea kueleza taarifa hizo kwenye viwanja vya wazi. Ukifuatilia matukio ya mchungaji huyo utagundua anachofanya ni kujitafutia umaarufu, mwaka jana alijisingizia kifo kilichofanana na kifo cha Marehemu Kanumba, magazeti ya udaku yaliandika taarifa zake na kuonyesha picha aliyokuwa kwenye jeneza.

‘Baada ya muda mfupi aliibuka kiwanja cha Buguruni akitoa maelezo ya namna marehamu Kanumba alivyokufa. Mchungaji huyu ni hatari anayestahili kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

‘Wadua, shirikisho, familia na marafiki wa marehemu jitokezeni kumtia adabu mtu huyo anayeendelea kujipatia umaarufu sambamba na kipato kupitia jina la marehemu Kanumba, kwani hawezi kuzungumzia Freemasons bila ya kutaja jina la marehemu Kanumba.

‘Ikiwa nia yake ni safi, angeelezea imani ya Freemasons kwa kumtaja aliyekuwa kiongozi wa Afrika Mashariki, Sir. Andy Chande, sio vizuri kumtaja mtu aliyekufa ambaye hawezi kujitetea.

‘Kwa mujibu wa maelezo yake anadai alikuwa anajua kama marehemu Kanumba ni muumini wa Freemasons kabla hajafa. Kama ni kweli kwanini alikaa kimya mpaka alivyokufa ndipo akaibuka kuanza kuzungumza mambo ambayo hayana faida kwa jamii, badala yake ni kuhamasisha jamii ya vijana kutaka kujiunga na imani. Sisi wana Swahili Cinema News tunasikitishwa na tabia ya mchungaji huyo.’ Mwisho wa kunukuu.

Kama hiyo haitoshi, mwaka jana ikiwa ni miaka tisa tangu kutokea kwa kifo cha marehemu Kanumba, Nabii Kairuki aliibuka tena kwenye madhabahu ya mtumishi wa Mungu mwenye umaarufu mkubwa nchini, Musa Richard Mwacha maarufu kama Kuhani Mwacha na kutoa ushuhuda mwingine wa uongo kuhusu Freemason huku waamini wa kanisa hilo wakimsikiliza na kumshangalia.

George Kairuki

Kifupi ni kwamba hata tukio hilo lililotendeka kwenye madhabahu ya kuhani Mwacha ni la uongo, na hata Kuhani Mwacha anahusika na tukio hili la kupangwa, (ushahidi upo) na  malengo yakiwa yale yale ya kujitafutia umaarufu na pesa kwa waumini anaowangoza.

Kwa kuwa tukio hilo siyo mada yangu ya leo nitaliandalia andiko maalumu kwa faida ya jamii na kuweka bayana mpango mzima ulivyokwenda.

Wakati tukisubiri andiko hilo unaweza kuingia YouTube kisha ‘search headline’ hii; ‘aliyekuwa mwanachama wa Freemason ajisalimisha kwa Kuhani na Mwalimu Musa Mwacha,’ utajionea jinsi Kairuki na rafiki yake Kuhani Mwacha wanavyoichezea madhabahu ya Mungu.

Matukio ya Kairuki ni mengi sana, hayawezi kuisha hapa hivyo tuhame huko na turejee kwenye mada yetu.

Kwa hiyo basi dhana ya Kanumba kuuawa na Fremason ilitokana na mapitio hayo ambayo kimsingi ni ya kupuuzwa na kukemewa kwa nguvu zote.

ITAENDELEA KESHO, HAKIKISHA UNAFUNGUA tanzaniapanorama.co.tz KUSOMA DHANA YA TATU YA KIFO CHA KANUMBA

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya