Tuesday, December 24, 2024
spot_img

NINI KINAKWAMISHA AMANI YA KUDUMU DRC?

ABBAS MWALIMU

0719 25 84 84

WANAJESHI wapatao 900 kutoka Kenya wapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Democratic Republic of Congo – DRC kwa ajili ya mapambano dhidi ya waasi wa tarehe 23 Machi – M23.

Wanajeshi hawa ni sehemu ya Jeshi la Afrika Mashariki – East Africa standby forces/military force (EACSF/MF) litakalokuwapo DRC kwa ajili ya kuleta amani. Aidha, wanajeshi hawa ni sehemu ya makubaliano ya kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Juni 2022.

Licha ya mikakati hiyo ya EAC bado kuna nchi zinahisiwa kutoa misaada kwa makundi ya waasi DRC. Makundi ya waasi yanayodhaniwa kupata misaada kutoka kwa baadhi ya nchi ni kama vile M23, muungano wa majeshi ya kidemokrasia – alliance democratic forces (ADF) na majeshi ya kidemokrasia kwa ukombozi wa Rwanda – Fonds départemental de revitalisation du loiret (FDRL.)

Hivyo basi, wakati huu Afrika Mashariki ikipeleka majeshi yake kuna haja ya kujiuliza kwa kina: nini kinakwamisha amani ya kudumu DRC?

Kwa kuzingatia swali hilo, makala hii itaangalia mambo kadhaa yanayokwamisha kufikiwa kwa amani ya kudumu DRC. Mambo hayo ni kama yafuatayo: (i) Kukosekana kwa utashi wa dhati kutoka Umoja wa Mataifa – United Nations (UN), (ii) ufinyu wa bajeti na (iii) baadhi ya nchi kuitumia DRC kwa manufaa yao.

KUKOSEKANA KWA UTASHI WA DHATI KUTOKA UMOJA WA MATAIFA

Umoja wa Mataifa (UN) ni kikwazo kikubwa cha kushindikana kwa upatikanaji wa amani ya kudumu DRC na tatizo la Umoja wa Mataifa lipo katika maeneo makubwa mawili; (a) Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na (b) Idara ya Ulinzi wa Amani – Department of Peacekeeping Operations/Field Support (DPKO/DFS.)

BARAZA LA USALAMA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – United Nations Security Council (UNSC) linaendeshwa na nchi kubwa zenye kulinda maslahi yao. Nchi hizi ni zile wanachama wa kudumu wa UN (Permanent members of UN), hasa nchi za Magharibi.

Pale ambapo nchi hizo hazioni maslahi ya moja kwa moja katika mzozo au zina upande zinanufaika nao huchelewesha mzozo kuisha au kinyume chake (Rejea Gray, 2007).

Ikumbukwe kwamba uamuzi ya amani na usalama wa dunia unasimamiwa na UNSC (Rejea ibara ya 39 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa – UN Charter).

Wengi tumeshuhudia namna nchi za Magharibi zilivyosimama kidete kuhusu mzozo wa Urusi na Ukraine. Lakini kwa nini msimamo kama huo hauonyeshwi kwenye mzozo wa Serikali ya Ethiopia dhidi ya waasi wa Tigrinya au DRC?

IDARA YA ULINZI WA AMANI-DPKO/DFS

DPKO/DFS ni eneo la pili linalosababisha kutopatikana kwa amani ya kudumu DRC. DPKO ina ngazi mbalimbali za mamlaka na uongozi ambazo huakisi ufanisi wa mpango wa amani.

Muongozo wa sera wa UNDPKO authority, command and control in United Nations peacekeeping operations wa tarehe 25 Oktoba, 2019 umeainisha ngazi mbalimbali za mamlaka, amri na udhibiti (AC2) za ulinzi wa amani katika mipango ya Umoja wa Mataifa.

Kwa kutazama AC2 tunaweza kubaini kuwa muongozo huo umepambanua ngazi tatu za utekelezaji wa sera katika taasisi. Ngazi hizi ni ngazi ya mkakati (strategic level), ngazi ya kimbinu (tactical level) na ngazi ya operesheni (operational level).

Kwa bahati mbaya sana na labda inaweza kuwa ni makusudi, nchi za Afrika hazipo katika ngazi ya mkakati ambayo ni muhimu sana katika uamuzi wa mpango wa amani. Aidha, uwakilishi wa nchi za Afrika katika ngazi ya mbinu haupo na wakati fulani ni mdogo mno.

Eneo ambalo Afrika inahusika zaidi ni ngazi ya operesheni. Ngazi hii hupokea maelekezo kutoka kwa ngazi ya kimbinu na kimkakati. Hivyo ni ngazi ya utekelezaji tu.

Masuala yote juu ya sera, namna gani operesheni itafanyika, wapi kambi iwepo huandaliwa na ngazi ya mkakati na ngazi ya mbinu. Kwa mantiki hiyo hata kanuni za ulinzi wa amani huandaliwa na ngazi ya mkakati na wakati fulani kushauriana na ngazi ya mbinu. Hapa ndipo mzizi wa tatizo unapokuja.

Kwa kuzingatia kanuni hizo zinazoandaliwa na ngazi ya mkakati na mbinu, mpango wowote wa operesheni ya ulinzi wa amani (peacekeeping operation) huongozwa na mfumo wa kisheria (legal framework).

Mfumo huo huzingatia mambo sita ambayo ni: (i) mamlaka ya UNSC, (ii) dhana ya mpango wa ulinzi (mission concept), (iii) dhana ya operesheni – concept of operations (CONOPS), (iv) sheria za ushiriki – rules of engagement (RoE) na muongozo wa utumiaji mabavu – directives on the use of force (DUF.)

(v) Makubaliano ya nafasi na namna majeshi ya kigeni yatakavyofanya kazi – status of forces agreement (SOFA), (vi) mkataba wa makubaliano baina ya nchi zinazotoa vikosi/polisi na Umoja wa Mataifa – troops/police contributing countries MoU-T/PCC MoU.

Kwa kuzingatia mfumo huo wa kisheria tunaweza kubaini mkwamo wa kupatikana kwa amani katika muktadha ufuatao: Mamlaka ya UNSC yamekuwa yakitazama zaidi maslahi ya nchi tano zenye uanachama wa kudumu (P5) na hasa Marekani na washirika wake, hivyo mamlaka ya UNSC katika kuamua juu ya mustakali wa amani na usalama ni kikazwo kikubwa cha upatikanaji wa amani DRC.

Mission concept, hii huanisha lengo kuu la mpango wa ulinzi. Walio katika ngazi ya operesheni hufanya majukumu yao kwa kuzingatia dhana ya mpango wa ulinzi (mission concept).

Tafsiri hapa kama mpango ni kwenda kulinda raia tu na si kupambana na waasi basi majeshi yatatekeleza wajibu huo pekee. Mpango huo huainisha tu kwamba majeshi ya TCC yanaweza kushambulia kwa lengo la kujilinda/kujihami pindi yanaposhambuliwa tu. Hii ni changamoto inayovikabili vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyopo DRC (MONUSCO). Je UNSC haijui tatizo hili?

CONOPS, hizi ni nyaraka zinazoainisha mwenendo mzima wa mfumo wa ulinzi na namna gani maafisa na askari watatumia mfumo huo kwa kuzingatia matokeo tarajiwa. Nyaraka hizi hueleza nini mfumo huo utafanya na si namna gani mfumo utafanya.

Aidha, nyaraka hizo ambazo hutoka katika ngazi ya juu ya UNDPKO kuhusu mpango wa amani hueleza mantiki ya kufanya hivyo.

Hili ni tatizo lingine dhidi ya kupatikana kwa amani ya kudumu DRC, kwa nini? Kwa sababu nyaraka hizi huanisha utendaji kazi wa mpango mzima wa amani. Kwa msingi huo kama waandaaji wa nyaraka (strategic level) hawana utashi kuona amani inapatikana hakutakuwa na mafanikio. Hili ndilo linalojitokeza DRC.

Rules of engagement (RoE) – sheria za ushiriki (RoE) na Directives on the use of force (DUF) – muongozo wa utumiaji wa mabavu ni eneo lingine linaloakisi kusuasua kwa upatikanaji wa amani ya kudumu DRC.

Hizi ni sheria za ndani za UNDPKO na miongozo ambayo vikosi na polisi (T/PCC) hupewa. Miongozo hii huelezea mazingira, hali, kiwango na namna ambayo majeshi yatakabiliana na maadui. Lengo la utumiaji wa silaha za moto ni kulinda raia.

Halikadhalika, kwa upande wake DUF inabainisha kuwa silaha zitumike pale tu inapoonekana kuna tishio la kudhuriwa kwa T/PCC au kuuawa. Hivyo mantiki ni kujilinda tu.

Kwa bahati mbaya sana asilimia kubwa ya operesheni iliyopo DRC inahusisha ulinzi wa amani ambayo inatoa nafasi finyu ya utumiaji wa silaha labda pale ambapo majeshi ya ulinzi wa amani yanapojilinda dhidi ya adui. Rejea dhana ya non use of force in peacekeeping.

Non use of force ni kanuni mojawapo kati ya kanuni tatu zinazoongoza ulinzi wa amani (peacekeeping operation). Ni wazi kuwa kanuni hizi zinakwamisha juhudi za kupatikana kwa amani ya kudumu DRC.

Sote tunaweza kukumbuka namna ambavyo Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika – Southern African Development Community (SADC) ilivyofanikiwa kulizima kundi la waasi la M23 mwaka 2013.

Meja Jenerali James Mwakibolwa akiwa katikati ya makamanda wa vikosi vya majeshi ya SADC

Majeshi ya SADC chini ya mwamvuli wa Brigedi ya uingiaji ya kijeshi – force intervention Brigade (FIB) iliyokuwa ikiongozwa na Luteni Jenerali Mstaafu, James Aloizi Mwakibolwa (wakati huo akiwa Brigedia Jenerali) yalifanikiwa kwa sababu ya mabadiliko ya kanuni (RoE na DUF) ambazo kimsingi zilileta ufanisi katika kupambana na M23.

Katika hali ya kustaajabisha mwaka 2020 kuliibuka hali ya sintofahamu kati ya Umoja wa Mataifa na nchi za SADC. Umoja wa Mataifa ulizitaka nchi za SADC zisiwe hodhi wa ulinzi wa amani DRC ili kutoa mwanya kwa nchi nyingine kushiriki. Hatimaye mwezi Disemba, 2020 SADC ilikubali kuibadili FIB kuwa majeshi ya kujibu kwa haraka – quick reaction forces (QRF).

Kimsingi huku kunaashiria kubadilika kwa kanuni zilizoipa mafanikio FIB. Je ni kwa nini UN walikuwa wakilazimisha FIB iondoke na kuwapa nafasi wengine? Ni kina nani au nchi gani hizo nyingine? Kwa manufaa ya nani?

SOFA haina tatizo kwa DRC kama ilivyo T/PCC Mou. Kwa ujumla mafanikio ya upatikanaji wa amani ya kudumu DRC yatategemea utashi wa Umoja wa Mataifa katika kumaliza vita nchini humo. Kwa bahati mbaya utashi huo haupo katika ngazi za juu za UN hasa strategic level na UNSC.

(II) UFINYU WA BAJETI

Nchi takribani zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina changamoto ya ufinyu wa bajeti hivyo EASF/MF nayo inaweza kuathiriwa na ufinyu huo wa bajeti.

Kwa mfano, bajeti ya kupeleka vikosi vya Kenya Kivu ya Kaskazini inakadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 4.5 za Kenya sawa na Dolla za Marekani Milioni 37 katika miezi sita ya kwanza ya operesheni. Kiwango hicho kimelalamikiwa na baadhi ya wabunge wa Kenya kwamba ni kikubwa ukilinganisha na hali ya uchumi wa Kenya kwa sasa.

Kwa mantiki hiyo suala la ufinyu wa bajeti linahitaji dhamira ya dhati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kumaliza kabisa uwepo wa makundi wa waasi DRC ili kuleta mazingira mazuri ya kiuchumi.

(III) BAADHI YA NCHI KUITUMIA DRC KWA MANUFAA YAO.

Zipo baadhi ya nchi ambazo huitumia DRC kwa manufaa yao. Kwa mfano kumekuwa na malalamiko juu ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 na FDLR. Jambo hili limekuwa likielezwa mpaka katika viunga vya UN. Ni kwa kiasi gani hili ni kweli? Hili ni jambo ambalo linahitaji uchunguzi wa kitaalamu.

Ramani ya DRC

Lakini pia zipo nchi za nje ya Afrika Mashariki hasa Ulaya Magharibi nazo zinanufaika na mzozo wa DRC licha ya kwamba hazionekani kushiriki moja kwa moja. Rejea alichoandika Berman (2017) katika andiko lake ‘This mine is mine: How minerals fuel conflicts in Africa’.

NINI KIFANYIKE?

Ili EASF/MF ifanikiwe ni lazima ijielekeze kwenye kubadili mission concept, CONOPS, RoE na DUF. FIB ilifanikiwa kwa sababu hiyo, hivyo nayo EASF/MF itafanikiwa ikifanikiwa kubadili hizo kanuni.

Kuna ugumu katika hilo kwa sababu UN tayari walishailazimisha FIB kubadilika kuwa QRF hivyo kubadilika kwa kanuni. Hivyo la EASF linaweza kuwa gumu zaidi kwa upande wa kanuni.

Mbali na hayo, nchi za Afrika Mashariki ziangalie zaidi faida itakayopatikana endapo DRC itakuwa na amani ya kudumu kuliko kujiuliza sana kuhusu gharama za kupeleka vikosi. Lakini kwa ujumla yanayokwamisha amani DRC ni mamlaka ya UNSC, mission concept na CONOPS.

Aidha, RoE na DUF nazo hukwamisha upatikanaji wa amani ya kudumu kutokana na namna zilivyotengenezwa na ngazi ya juu ya uamuzi (strategic level).

Asanteni.

Abbas Mwalimu

(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia

(Facebook|WhatsApp)

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya