Monday, December 23, 2024
spot_img

UTATU WA KIFO CHA KANUMBA – (2)

The Trinity of Steven Kanumba’s Death

HAMEES SUBA

0672 86 65 74

ILIPOISHIA

JAMBO la kwanza, napinga kwa nguvu zote madai yote kwamba kifo cha Kanumba kina mkono wa Freemason. Sipingi uwepo wa Freemason wala sipingi kwamba Freemason hawaui watu, ninachopinga ni Freemason kuhusika na kifo cha Kanumba.

Nitaeleza dhana hii ilipoanzia, historia ya Kairuki, watu walioshupalia dhana hii mpaka ikakuwa, Kanumba aliizungumzia vipi Freemason enzi za uhai wake na baada ya hapo ndipo nitaizungumzia dhana ya tatu ya kifo cha Kanumba. Tukutàne wiki ijayo.

TUUNGANE NAYO

KANUMBA NA DHANA YA FREEMASON

Taarifa za uhusiano wa Kanumba na Freemason zilianzia kwenye magazeti ya udaku likiwemo gazeti la Kiu ya Jibu ambalo mimi nilikuwa mmoja wa wahariri wake.

Kila jambo lina zama zake, miaka ya 2000 ndipo makala nyingi kuhusu Freemason ziliibuka na kushamiri katika vyombo vya habari hususani magazeti. Haikuwa katika magazeti ya udaku tu bali hata katika magazeti ya ‘hard news’ au kama yalivyozoeleka kuitwa magazeti ya siasa, kuona makala tofauti tofauti kuhusu Freemason zikiandikwa.

Kila mwandishi kwa utashi wake na kwa kuzingatia sera ya chombo chake aliandika na kuzinogesha makala kuhusu Freemason kwa jinsi ya uelewa wake.

Ukiachana na ile nembo iliyokuwa ikitumika kama chapa kuu ya Freemason ya ‘Square & Compass’ alama nyingine iliyokuwa ikitumiwa na watu kujitambulisha kama wafuasi wa Freemason ni ile ya vidole viwili vya muonekano wa ‘V.’

Kwa upande wangu nilishuhudia wasanii wengi wa filamu na hata muziki wakiomba kupigwa picha huku wakiwa wameonyesha alama ya ‘V’ ili watambulike kama wafuasi wa Freemason, lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa mwanachama wa Freemason na wengine hawakuwa wakifahamu chochote kuhusu Freemason.

Kwao wao walichukulia kama sehemu ya kutengeneza ‘kick’ au ‘tension’ kwenye jamii ili kazi zao ziweze kutambulika kirahisi.

Chapa ya ‘Square & Compass’ ilikuwa ikitumika zaidi kwenye upande wa mavazi, yaani msanii ananunua nguo yake dukani anakwenda kwa fundi na lebo zenye chapa ya ‘Square & Compass’ anamwambia aishonee kwenye mabega au sehemu ambayo akivaa nguo hiyo itaweza kuonekana kwa urahisi kisha anapiga picha na nguo hizo tayari anakuwa mwanachama wa Freemason. Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa yanakwenda.

Kwa upande wa Kanumba, mwishoni mwa miaka ya 2000 ndipo alianza kufanya promosheni za namna hii hasa katika mavazi yake na mimi nilikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimpromoti kwa staili hiyo.

Lakini suala la Kanumba na Freemason lilipamba moto zaidi baada ya kuigiza filamu ya ‘Devil’s Kingdom’ aliyomshirikisha nguli wa filamu kutoka nchini Nigeria, Ramsey Noah.

Kwanini ‘u-freemason’ wa Kanumba ulipamba moto? Twende hatua kwa hatua. ‘Story line up’ ya filamu hiyo moja kwa moja ilihusu ‘u-freemason, ilihusu kisa cha mtumishi wa Mungu aliyekuwa na kanisa lake lakini aliyekumbana na changamoto ya kutopata mwitikio wa waumini.

Yaani licha ya karama na kipawa cha maombezi na utendaji wa miujiza alichokuwa nacho mtumishi huyo lakini bado waumini hawakuvutika na hudumu yake jambo lililokuwa likimchanganya sana akili mtumishi huyo ambaye ni Kanumba katika filamu hiyo.

Wakati akitafuta jibu la changamoto hiyo ndipo anakutana na mtu anayemshawishi kujiunga Freemason ili mambo yake yamnyookee ikiwa ni pamoja na kuahidiwa kupata waumini watakaojaza kanisa lake na kupewa nguvu ya kufanya miujiza na ishara za kutisha.

Kwa wale waliobahatika kuiona filamu hiyo watakuwa wanaelewa kilichomo ndani yake. Lengo langu si kusimulia stori iliyomo ndani ya filamu hiyo.

Kwa ufupi ni kwamba ni filamu iliyohusu mwenendo wa Freemason katika kuwahadaa na kuwapoteza kiimani watumishi wa Mungu.

Sasa basi, baada ya kukamilika kwa filamu hiyo kama ilivyo ada wafadhili wakuu wa mradi huo Kampuni ya Steps Entertainment walitaka waandishi wazoefu wa promosheni za wasanii watakaowatumia kupanga namna ya promosheni ya filamu hiyo itakavyofanyika. Mimi nilikuwa mmoja wa waandishi walioshirikishwa kwenye kuratibu jambo hilo.

Kampuni ya Steps Entertainment walikuwa ndiyo wasambazaji wakubwa wa filamu kuliko wote hapa nchini. Utaratibu wao ulikuwa ni kununua filamu kutoka kwa wasanii mbalimbali na kuzisambaza nchini na nje ya nchi lakini baada ya tasnia kukuwa walianzisha programu ya kuwapa mitaji wasanii wakubwa kwa ajili ya kutengeneza filamu kupitia kampuni zao kwa masharti ya kuwauzia wao kama wasambazaji.

Programu hii ndiyo iliyowatoa wasanii wengi wenye majina hapa nchini akiwemo Vincent Kigosi, almaarufu kwa jina la Ray na Marehemu Kanumba.

Kumewahi kuwepo taarifa kuwa Kampuni ya Steps Entertainment waliwawekea kwenye akaunti zao wasanii Ray na Kanumba kiasi cha Shilingi milioni mia moja kila mmoja kwa mkataba wa kutengeneza filamu nne ndani ya mwaka mmoja na kuzikabidhi kwa Kampuni ya Entertainment Steps kama mali yao.

Kwa maana hiyo Kampuni ya Steps Entertainment walishafikia hatua ya kununua ‘master dvd’ moja ya filamu kutoka kwa Ray au Kanumba kwa gharama ya Shilingi milioni 25.

Kutokana na ukubwa wa biashara ya filamu ulipokuwa umefikia ndio maana wasambazaji hao walisimamia mambo muhimu ya kimasoko ikiwemo promosheni za wasanii na kuzilipia wao ili wasije wakaingia hasara endapo filamu haitafanya vizuri sokoni.

Ramsey Noah na Marehemu Steven Kanumba

Kwa mujibu wa muongozaji wa filamu, Selles Mapunda aliyewahi kufanya kazi Kampuni ya Steps Entertainment amebainisha kuwa Ramsey Noah alilipwa na Kampuni ya Steps Entertainment kiasi cha Dola za Marekani 10,000, nauli ya ndege (Go & Return) na gharama zote za hoteli kwa siku zote alipokuwa jijini Dar es Salaam kuigiza filamu ya ‘Devil’s Kingdom.’

Kanumba aliiuza filamu hiyo kwa Kampuni ya Steps Entertainment Shilingi milioni 60 za kitanzania. Pia, inaelezwa kuwa ndiyo filamu iliyotengenezwa kwa gharama kubwa kuliko filamu yoyote hapa nchini mpaka Kanumba anafariki. Turejee kwenye mada.

Kamati ya promosheni ilipokutana ilijadili namna nyingi za kuipromoti filamu hiyo lakini kutokana na maudhui yaliyokuwemo ndani ya filamu hiyo, na kutokana na wasanii wengi kuwa tayari walishakubali kujitangaza kama wanachama wa Freemason ili ‘kubusti’ kazi zao iliazimiwa kuendelea kutumia ‘kick’ za Freemason katika kuitangaza filamu hiyo.

Lakini kwa mara ya kwanza nilimsikia Kanumba akitilia shaka kuendelea kutangazwa kama mwanachama wa Freemason kwa kile alichodai kwamba inaweza kumletea shida kiimani.

Binafsi nilimuuliza kwanini iwe kipindi hiki wakati huko nyuma hakuwa akihofia chochote kuhusu kuhusishwa na Freemason?

Akanijibu hivi; “Ogaa, unajua hii filamu ni tofauti sana na filamu zangu nyingine zote, kule nyuma sikuwa nikihofu kwa sababu hakukuwa na uhalisia wa filamu na maisha tunayoishi lakini filamu hii kuna mdahalo mkali sana kuhusu mimi na Freemason, tumeyachalenji sana maandiko ya Biblia Takatifu ndiyo maana naona kama inaweza ikaleta shida pale watu watakaposhindwa kunielewa na kuamini kuwa mimi ni Freemason.”

Kimsingi Kanumba alishaanza kuhisi madhara ya promosheni zile endapo watu wataamini kuwa ni mwanachama wa Freemason au amewahi kuwa kwenye mtandao huo. Ilifikia mahali akataka kuwaomba mabosi wa Kampuni ya Steps Entertainment kuzungumza na kamati ya promoshenu kutafuta namna nyingine ya kuipromoti filamu hiyo badala ya kumtangaza kuwa ni mwanachama wa Freemason.

Lakini kwa kuwa ilikuwa ni biashara na tayari alikuwa ndani ya mkataba hatimaye alikubali ifanyike promosheni vyovyote ilivyoamuliwa.

Kwa hiyo, zikaanza stori za kila namna za kumuhusisha Kanumba na Freemason na hata baada ya filamu hiyo kutoka baadhi ya magazeti yaliendelea kuzitangaza filamu zake zilizofuata kwa kumuhusisha na Freemason. Mmoja wa watu waliokuza sana dhana hii ni Mhubiri George Kairuki.

KAIRUKI NI NANI?

Jina lake halisi ni George Kariuki lakini hapa nchini Tanzania anafahamika kwa majina ya George Kairuki. Kuna tofauti ya Kariuki na Kairuki. Asili ya jina Kairuki inatoka mkoani Kagera, ni miongoni mwa majina ya Kihaya lakini Kariuki ni jina lenye asili ya makabila ya Kenya.

George Kariuki asili yake ni Kenya na hata familia yake mpaka sasa inaishi nchini Kenya. Haifahamiki aliingia nchini mwaka gani lakini taarifa za kihabari zinabainisha kwamba alikuwepo nchini tangu mwaka 2011 wakati huo akijihusisha na mahubiri ya mtaani (Street Precher) na akijitambulisha kwa jina la Nabiii Kairuki.

Alianza kuwadanganya watu kwamba amewahi kuwa mwanachama wa Freemason mara baada ya kujiunga na chama hicho kule Likoni, Mombasa nchini Kenya.

Kwa kufuata upepo ule ule wa promosheni za Kanumba na Freemason, mara baada ya kifo cha Kanumba akaona mgodi umetema, pale alipopataka pamewadia. Akaibuka na mapya kabisa tena akidai kwamba yeye ndiye aliyemwingiza Kanumba kwenye ‘ufreemason.’

Hakuna shuhuda yoyote inayoweza kuthibitisha kwamba Kanumba na Kairuki wamewahi kukutana au hata kupishana njiani japo mara moja katika kipindi chote cha uhai wa Kanumba. Hii ina maana kwamba maneno yote anayoyazungumza Kairuki kuhusu Kanumba ni ya kubuni na kutengeneza. Kwa maoni yangu anapaswa kupuuzwa kwani sio mara yake ya kwanza kufanya hivyo.

Miongoni mwa matukio ya hatari aliyowahi kuyafanya Kairuki ni pamoja na kujisingizia kifo kwa minaajili ya kujipatia pesa na umaarufu.

Tukio lenyewe kilikuwa hivi; Alipiga picha akiwa ndani ya jeneza mithili ya mtu aliyekufa na kuwatuma washirika wake wazisambaze kwenye vyombo vya habari na kudai kuwa Freemason wamemuua. Lengo lilikuwa kwamba taarifa hizo zikishasambaa baadaye ajitokeza hadharani na kuilaghai jamii kwa mara nyingine kuwa ameyashinda mauti.

Tukio hili alilifanya mwaka 2013 akiwa na dhamira ya kuanzisha Kanisa endapo ‘dili’ lake hilo ‘lingetiki’ lakini kwa bahati mbaya janja yake ilibainika kutokana na upungufu uliokuwa ndani ya picha za maiti yake.

ITAENDELEA KESHO, HAKIKISHA UNAFUNGUA tanzaniapanorama.co.tz

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya