Thursday, June 19, 2025
spot_img

MCHAWI WA WANAWAKE NI WANAWAKE WENYEWE

.MAUREEN MALLYA

ASUBUHI moja tulivu katika eneo la kivuko cha Kigamboni (ferry) kuna umati mkubwa wa watu wanaosubiri kivuko, katika umati huo mimi nilikuwepo.

Watu wakiwa wamekaa katika vikundi vidogo vidogo wakisogoa mara anapita msichana mrembo sana mbele yetu, anapotupa mgongo wanawake na wanaume tunamsindikiza kwa macho tukifurahia urembo wake.

Pembeni yangu kuna msichana mmoja kasimama, naye anasubiri kivuko, huyu naye mzuri. Kama wengine naye anamsindikiza kwa macho mrembo aliyepita lakini yeye anamkazia macho zaidi huku akampandisha na kumshusha, halafu akamnyali. Mimi nikabaki nimedua huku nikijiuliza kama wanajuana au wamewahi kukoseana?

Maisha yana vituko sana jamani na sijui ni nini zaidi ya ‘JIK’ ambacho kinaweza kusafisha madoa sugu ya chuki baina ya wanawake.

Jana nikiwa ofisini, kuna dada alikuja na shida yake. Mmoja wa wafanyakazi wenzangu ambaye ni mwanaume alikwenda kumsikiliza. Waswahili wana msemo usemao, ‘umbea suna’ lakini katika hili wala haikuwa umbea kwa sababu wawili hao walikuwa wanaongea kwa sauti kubwa sana, nadhani walisahau kuwa wapo ofisini.

Kilichokamata hisia zangu katika mazungumzo yao ni jinsi dada yule alivyokuwa akiwazungumzia vibaya wanawake wenzake hasa wenye kipato kikubwa na wenye nafasi/vyeo katika jamii yetu kuwa wana roho mbaya hasa kwa wanawake wenzao.

Nikinukuu sehemu ya alichokisema; “unajua hata vitabu vya dini vinakataza wanawake kuwa viongozi labda haya matatizo ya kukosa maji na umeme kwa sababu ya ukame, itakuwa ni Mungu anajaribu kusema na sisi lakini hatusikii.”

Sio maneno yangu hayo, la hasha ni maneno ya huyo dada na alipokuwa akiyazungumza mimi kama mwanamke mwenzake nilijisikia vibaya sana. Huu ni ufinyu wa mawazo.

Mtu anawezaje kuwa na mtazamo hasi kiasi hicho. Hadithi haikuishia hapo, yule dada akamwambia mwanaume aliyekuwa anamuhudumia; “nashukuru wewe ni mwanaume maana ningekuta ni mwanamke nisingepoteza muda wangu hata dakika moja. Wanawake siyo watu wazuri kabisa hawana msaada. Kila ofisi tulipokutana na mwanamke mambo yetu yalikwama,”

Mwanaume aliyekuwa akimuhudumia akawa anacheka tu na haina shaka kicheko chake kilitokana na sifa kemkem za uanaume wake alizokuwa akipewa na au kwa husda na chuki kwenye jinsia ya kike.

Nilibaki na mshangao kwa sababu sikupendezwa na kauli za huyu dada lakini kwa upande mwingine, maneno yake yalikuwa na ukweli fulani ndani yake. Nadhani ni eneo zuri sana la kufanyia utafiti na kuona ni kwa namna gani tunaweza kuleta mtazamo chanya kwenye suala hili

Je, mchawi wa mwanamke ni mwanamke mwenzake? Kweli wanawake hawapendani? Kwa nini hawapendani? nini kifanyike kubadilisha hili?

Haina shaka suala la wanawake kutopendana wao kwa wao lipo wazi sana. Ni jambo ambalo halina kificho. Nimezungumza na watu wengi juu ya suala hili na wote wanasema ni kweli wanawake hawapendani.

Wengi wao wanatoa sababu zinazofanana na labda tuzitazame japo kwa uchache; ya kwanza ikiwa ni wivu ambayo imetajwa na wengi niliozungumza nao.

Rafiki yangu Grace anasema wanawake wanaoneana wivu wao kwa wao na kila wakati wapo kwenye mashindano bila sababu za msingi. Kwamba wanawake hawapendi kuona wanawake wenzao wanafanikiwa.

Anaeleza zaidi kuwa mwanamke yupo radhi kumfurahia na kuunga mkono mafanikio ya mwanaume kuliko mwanamke mwenzake na kwamba ushahidi wa hilo ni maisha ya kila siku majumbani, kazini, kwenye nyumba za ibada mpaka kwenye siasa.

Mwingine niliyezungumza naye, yeye anasema wanawake wanatishwa na mafanikio ya wanawake wenzao, maumbile, elimu na tatizo la kujiona bora kuliko wanawake wengine, mambo ambayo mtu akiyatafakari kwa makini utagundua hayana msingi.

Huyu anaeleza zaidi kuwa kutokujiamnini pia ni tatizo kwa wanawake, kwamba kujiamini kunaweza kutazamwa kwa mitazamo miwili katika hili. Mosi ikiwa kujiamini binafsi. “Ninaamini kwa asilima mia moja, kama mtu akijiamini mwenyewe na akiamini uwezo wake hawezi kuruhusu kubabaishwa au kunyimwa usingizi na maisha ya mwanamke mwingine. Ukiridhika na maisha yako nafsi yako inatulia.”

Maoni mengine niliyoyapata katika utafiti wangu mdogo ni tabia ya baadhi ya wanawake kuamini wanaume ni bora zaidi kuliko wao kama ilivyokuwa kwa dada aliyefika ofisini kwangu na kuhudumiwa na mwanamume. Kwangu mimi hili naliona kuwa na mizizi kuanzia kwenye dini, jamii, Serikali mpaka kwenye familia.

Wapo pia wanaosema kuwa dini nyingi zinawapa kipaumbele wanaume kuliko wanawake ambao hukuchukuliwa kuwa si lolote wala chochote.

Upo ukweli huu kwenye jamii zetu nyingi ambazo mara nyingi sana mtoto wa kiume huchukuliwa kama lulu fulani hivi kwenye familia kiasi kwamba wapo akina mama wanaowaita watoto wao wa kiume “baba” na kuwalea kama miungu fulani hivi au mayai bila kujua kuwa wanalea mayai viza.

Maoni ya wanaume niliowafikia na kuzungumza wao wakati wa utafiti wangu huu ni kwamba wanawake kiasili hawapendani na kutopendana kwao huwa hakuna sababu yoyote ya msingi bali ni asili yao. 

Lakini nikirejea kwa wanawake, sababu iliyonichekesha zaidi kuhusu wanwake kutopendana wao kwa wao ni ya uchache wa wanaume. Dada mmoja katika mazungumzo yetu anasema wanaume ni wachache kwa hiyo wanagombaniwa sana na wanawake jambo linalosababisha wanawake kushindana na wanawake wenzao kuwapata wanaume.

Mbali na maoni hayo, utafiti binafsi nilioufanya kuhusu hili unaonyesha kuwa katika jamii zetu  nyingi, kama mwanamke hajaolewa anaonekana hajakamilika. Wanawake wanapambana kupata stara za waume na hii inakuwa kama ule msemo wa “survival of the fittest.”

Lakini wapo baadhi ya watu wanaoamini  ni ‘stereotype’ tu. Kwamba hakuna ukweli wowote unaoweza kuthibitisha chuki iliyopo baina ya wanawake wao kwa wao bali ni ubaguzi au maneno ya kichochezi yaliyotengenezwa na watu. Mambo ni moto na wanawake ndio sisi, kazi sana.

Nikiongea kwa niaba ya wanawake wenzangu, nadhani ni wakati sasa kwa sisi wanawake kujiamini na kujikubali. Kila mmoja wetu ni mzuri na ameumbwa kipekee na Mungu ameweka karama katika kila mmoja wetu.

Hatuna sababu ya kushindana na ingependeza zaidi kama tungetiana moyo na kusaidiana kufikia malengo yetu na makusudi yetu katika maisha.

Hakuna mtu mzuri zaidi ya mwingine kwa sababu uzuri ni kitu binafsi. Kila mtu ana kitu anachokipenda kwa mtu, hakuna kiwango kimoja cha uzuri kwa kila mtu bali wote tumeumbwa kwa mfano wa Mungu na ukimjua na kumpenda sana Mungu pia utajikubali mwenyewe maana Mungu hafanyi makosa katika uumbaji wake.

Kutokujikubali ni kumtukana Mungu. Mwanamke mwenzio sio adui yako, hajajiumba mwenyewe bali naye kaumbwa. Riziki ya mtu haizuiliki na Mungu akikubariki, kakubariki mwanadamu hawezi kuzuia japo anaweza kukucheleweshea baraka ulizojaaliwa na Mungu.

Huu msemo utufundishe kufurahia maendeleo ya wengine tukiamini ni baraka za Mungu na kwamba hata sisi tuna baraka zetu. Mwingine akiwa na mafanikio zaidi yako mfurahie na kama kuna la kujifunza kutoka kwake jifunze ili na wewe usonge mbele lakini usiruhusu mafanikio ya mwanamke mwenzako yakupe sonona.

Jikubali na ujifurahie maana viatu vya watu wengine huwezi kuvivaa, vitakubana au vikupwaye. Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, shindana na wewe mwenyewe kuongeza tija kwenye maisha yako ukitambua kuwa wewe ni muhimu na unatosha.

Wanawake tufanye kazi kwa bidii kutafuta vipato vyetu wenyewe na kufikia mafanikio tunayohitaji. Wanawake tuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo na tunayo mifano ya wanawake wengi sana katika jamii kwa sasa.

Kila kitu kinawezekana mwanamke ukiamua na kuchukua hatua. Mafanikio ni lazima ukiamini inawezekana, ukiwa ‘busy’ na maisha yako utakuwa hauna muda wa kuhangaika na maisha ya watu wengine.  Ile tabia ya kujiona wewe bora kwa sababu wewe ndiyo mwanamke pekee kwenye ‘management’ iliyojaa wanaume ni ujinga. Shika wenzio mkono mpande pamoja.

Tunaishi katika zama za utandawazi, zamani kuzaa mtoto wa kiume ilikuwa ndiyo kila kitu lakini kwa sasa watu wanatamani kuzaa watoto wa kike.

Kuna kaka mmoja rafiki yangu ana watoto watatu wa kiume wakati anapata mtoto wa mwisho, nilipompongeza akashukuru na kuniambia “nina madume wote sasa sijui nani atatulea tukizeeka.”

Baadaye nilitafakari kauli yake nikamuelewa lakini kwa sababu mada hiyo sikuilenga kwenye makala haya, tuliweke pembeni hilo. Wanawake tunaweza na ni wakati wa jamii nzima kuamini hivyo hususani wanawake wenyewe. Mtoto wa kike ni muhimu sana kama mtoto wa kiume.

Zama zimebadika, tuna wachungaji wanawake na viongozi wakubwa wa kisiasa na kiutumishi. Tubadili mitazamo dhaifu dhidi ya watoto wa kike, tuwalee watoto kwa usawa wa kijinsia bila kumshusha thamani mtoto wa kike.

Nakubaliana na rafiki yangu Abdallah, yeye anasema wanawake wakipendana na kupatana wanaume watakuwa taabuni. Kama wanaume wanajua siri hii sisi wanawake nani katuloga tusijue nguvu ya umoja wetu?  

Maisha kwetu si mashindano ya urembo, mafanikio ya mali wala kupigania wanaume kwa vile tumeambiwa ni wachache na ni lazima umpate ili uolewe na kuonekana umefanikiwa kwenye jamii.

Muda umefika kwa wanawake kuona kuwa mtu pekee anayekuelewa kwa undani ni yule anayepitia njia sawa na yako, naye ni mwanamke mwenzio kama alivyosema Alice. Tuungane kwa pamoja kuzipinga tamaduni zinazolenga kutudidimiza, kutufanya tuonane kama washindani na tuchukiane.

Wakoloni walitumia mbinu ya “divide and rule” wakafanikiwa kututawala na hii ndiyo mbinu inayotumika kutugawa sisi wanawake na mbaya zaidi kwa kiasi kikubwa inatumiwa na sisi wenyewe.

Tukiungana na kupendana tunaweza kushinda na kufika mbali sana. Kama baba wa Taifa alivyosema, uwezo tunao, nguvu tunazo na nia pia. Kuna nguvu katika umoja ukizingatia wanawake tupo zaidi ya asilimia 51 katika Taifa letu.

Tuijiulize tukipendana kwa dhati itakuaje? Nadhani mpaka hapo tutakuwa tumeshajua kuwa mganga wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe, basi. Au vipi?

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya