Tuesday, December 24, 2024
spot_img

DEREVA, ‘ANKO’ WABAKA MTOTO MIAKA 6 KWENYE ‘SCHOOL BUS’

RIPOTA PANORAMA

MTOTO mwenye umri wa miaka sita anayesoma darasa la kwanza katika Shule ya Starlight Pre and Primary iliyopo Tegeta Wazo mkoani Dar es Salaam (jina kapuni) amebakwa na wanaume wawili watu wazima kwenye gari la shule, ‘school bus.’

Wanaume hao ni dereva wa basi la Shule ya Starlight Pre and Primary na kondakta wake ambaye anafahamika zaidi na watoto kwa jina la ‘anko’ na kwamba mtoto huyo amekuwa akifanyiwa ukatili huo kwa muda mrefu bila kuwaambia wazazi wake kwa sababu wabakaji hao walikuwa wakimtisha kuwa akisema watamuua.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, mzazi wa mtoto huyo (jina limehifadhiwa) amesema alibaini mtoto wake kufanyiwa kitendo hicho cha kikatili baada ya kulalamika mfululizo kuumwa na tumbo ndipo alipoanza kumdadisi jinsi anavyoumwa huku akimfanyia uchunguzi wa mwili.

“Siamini kwa sababu sikuwahi kufikiria wale watu wazima tena wa shule tunayoiamini kuwafuata watoto wetu nyumbani kuwapeleka shule na kuwarudisha wanaweza kufanya kitendo cha kikatili hivyo. Mtoto alikuwa haishi kulalamika kuumwa tumbo, nimempeleka Kitengule Hospitali zaidi ya mara tano, tunapewa dawa lakini malalamiko ya kuumwa tumbo hayaishi.

“Majuzi akaanza kulia tena tumbo linamuuma, nikachanganyikiwa kabisa maana kila nikienda hospitali hawaoni tatizo, nikaamua kukaa naye chini kumbembeleza huku nikimuuliza tumbo linaumaje, akawa anasita kusema, hapo akili ikashtuka.

“Nikazidisha utulivu huku nikimbembeleza asilie bali aseme linaumaje akasema anaogopa kwa sababu watamuua, nikamuuliza akina nani, hakusema. Nikamwambia hakuna wa kumuua mimi nipo na baada ya kumbembeleza sana ndiyo akaanza kusema dereva na ‘anko’ wa gari lao la shule yaani ‘school bus’ huwa wanambaka, wanambaka kwa zamu.

“Alieleza kila kitu, alisema wanavyomshika mpaka wanavyomvua nguo na wao wanavyovua. Alisema wakati wanarudishwa nyumbani kutoka shuleni watoto wote huwa wanapelekwa kwanza anabaki yeye peke yake kwenye gari, kisha gari linapelekwa eneo la ukimya, wanafunga vioo na mapazia ya kwenye vioo vya gari ndiyo wanamtendea huo unyama, wakimaliza ndiyo wanamrudisha nyumbani huku wakimtisha kuwa akisema watamuua,” alisema mzazi wa mtoto huyo na kuongeza.

“Usiku ule ule tulimpeleka hospitali akapata matibabu ya awali na wakatuambia ni kweli kaishaharibiwa kabisa. Tuliwasiliana na polisi usiku huo huo wakawahi nyumbani asubuhi asubuhi ile gari ya shule ilipofika tu yule dereva akatiwa nguvuni ila huyo mwenzake alikamatwa baadaye wakapelekwa kituo cha polisi cha Madale, kesi namba iliyofunguliwa ni MDL/RB/3889/2022, KUBAKA. Hivi sasa tunaendelea na matibabu ya mtoto katika Hospitali ya Mwananyamala.

Tanzania PANORAMA Blog jana ilifika Shule ya Starlight Pre & Primary na kukutana na mwalimu mkuu wa shule hiyo ambaye hakuwa tayari kujitambulisha jina na baada ya kuulizwa kuhusu tukio la kukamatwa kwa wafanyakazi wa shule yake, alisema hawezi kuliongea kwa sababu anajiandaa kwenda kuswali hivyo aulizwe meneja wa shule na kumuongoza mwandishi ofisi kwa meneja.

Alipoulizwa meneja wa shule ambaye naye hakujitambulisha jina lake alisema hana taarifa kuhusu tukio hilo na kuomba muda wa kuwasiliana na mkurugenzi wa shule ambaye aliomba kuongea na Tanzania PANORAMA Blog na kukanusha katakata wafanyakazi wa shule yake kubaka mtoto mwenye umri wa miaka sita huku akisisitiza wafanyakazi wake wote wapo kazini kama kawaida.

Baadhi ya wafanyakazi wa shule hiyo waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog wamethibitisha kukamatwa kwa wenzao wawili wanaotuhumiwa kumbaka mtoto huyo na kueleza kuwa uongozi wa shule unafanya kila jitihada kuficha ukweli.

Wakati uongozi wa Shule ya Starlight Pre and Primary ukikanusha kwa nguvu kubwa wafanyakazi wake kukamatwa kwa tuhuma za kumbaka mtoto mdogo wa miaka sita, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa upelelezi umeishakamilika na jalada la kesi hiyo litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Tanzania PANORAMA Blog INAENDELEA KUFUATILIA KWA KARIBU TUKIO HILI LA KIKATILI.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya