Monday, December 23, 2024
spot_img

UTATU WA KIFO CHA KANUMBA (1)

(The trinity of Steven Kanumba’s death)

HAMEES SUBA

0672 86 65 74

MIONGONI mwa fahari ilizowahi kupata Tanzania ni uzao wa aliyekuwa nguli wa filamu, Marehemu Steven Charles Kanumba, almaarufu Kanumba the great.

January 8, 1984 wakati tumbo la uchungu lilipomsukasuka Flora Mtegoa na kujikuta akikimbizwa hospitalini ambako saa chache baadaye alijifungua mtoto wa kiume aliyekuja kuitangaza vema bendera ya Tanzania kupitia tasnia ya filamu.

Haikuwa furaha kwa Flora Mtegoa peke yake bali hata kwa mumewe, Mzee Charles Kusekwa Kanumba baada ya kupata taarifa kuwa ukoo wake umeongezeka kwani Flora Mtegoa amejifungua dume la Mbegu. Huo ndio ulikuwa ujio wa Steven Charles Kanumba the great hapa duniani.

Kanumba hatupo naye tena duniani lakini kumbukumbu alizotuachia bado ni hazina kubwa inayopaswa kuendelea kusimuliwa kwa vizazi na vizazi.

Licha ya kuondoka duniani akiwa na umri mdogo wa miaka 28, Kanumba alitekeleza majukumu mengi na makubwa katika tasnia ya filamu nchini na mpaka sasa rekodi zake hakuna msanii aliyeweza kuzifikia, achilia mbali kuzivunja.

Anayebisha tukumbushane kidogo. Ni muigizaji gani wa kwanza aliyeweza kuvuka nje ya mipaka ya nchi kwenda kuwatia hamasa waigizaji wa nje kuja kuigiza hapa nchini Tanzania? Jibu halihitaji tochi wala mwanga wa jua, Kanumba the great ndio jibu.

Waigizaji Kama Mercy Johnson, Emanuel France, Nkiru Silvanus na Ramsey Noah wote kutoka Nigeria tungewajuaje kama si Kanumba? Inawezekana tungekuja kuwajua lakini isingekuwa mapema kama alivyotufanyia Kanumba.

Ile barabara ya watu maarufu kule Hollywood nchini Marekani, maarufu kama Walk of Fame tungeifahamu vipi kama si Kanumba? Inawezekana tungeifahamu lakini si kwa kushuhudia ikikanyagwa na kijana kutoka kijijini Bugoyi kule Shinyanga.

Studio maarufu duniani kama Warner Bros na Universal Studio zilizoko nchini Marekani tungezijuaje kama si Kanumba? Inawezekana tungezijua lakini si kwa kutembelewa na muigizaji wa filamu kutoka hapa nchini.

Mada yangu leo sio kuelezea sifa za Kanumba au ubora wake lakini imenilazimu kugusia baadhi ya vitu hivyo ili kutambua heshima na mchango wake katika kuinyanyua tasnia ya filamu hapa nchini. Turudi kwenye mada sasa.

Mnamo tarehe 7 Aprili, 2012 Taifa lilipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Kanumba. Kwa sisi watu wa habari taarifa zilianza kutufikia majira ya saa mbili usiku kuhusiana na tukio la kifo cha Kanumba kilivyotokea.

Binafsi nilikuwa mitaa ya Sinza na ndipo nilipokuwa nikiishi. Sikuwa mtaani kwangu ndio maana nimesema nilikuwa mitaa ya Sinza. Kanumba naye alikuwa akiishi Sinza jirani na maeneo ya Vatican.

Alikuwa amepanga kwenye nyumba moja iliyokuwa jirani na barabara iendayo Tandale. Ukitokea Sinza madukani ukakipita kituo cha Lion Hotel, hatua chache mbele upande wa kulia ndipo yalipokuwa makazi ya Kanumba na kifo ndipo kilipomkuta katika makazi yake hayo.

Tuendelee na mada yetu. Kwa mazingira yoyote kifo kinapotokea mtu wa mwisho kukithibitisha ni daktari. Huo ndiyo utaratibu unaokubalika hata kisheria.

Inafahamika kuwa kifo cha Kanumba kilitokana na ajali ya kusukumwa na aliyekuwa mpenzi wake na muigizaji mwenzake, Elizabeth Michael maarufu zaidi kwa jina la Lulu. Ripoti ya daktari aliyeufanyia uchunguzi (Post Moterm) mwili wa Kanumba ilithibitisha hilo.

Alipatwa na mshtuko kwenye ubongo ‘Brain Concussion’ alipodondoka kwa nyuma baada ya kusukumwa.

Lakini tukiachana na ripoti hiyo ya daktari, kumekuwa na dhana nyingine mbili zinazohusishwa na kifo cha Kanumba hivyo nimeona niziandikie andiko hili na kuainisha kile kinachosababisha watu kuwa na dhana hizo.

Narudia kusema kwamba tayari ripoti ya daktari ilishathibitisha kilichomuua Kanumba lakini kwa kuwa Kanumba alikufa akiwa mtu maarufu, si vibaya kuzungumza yale yenye utata katika maisha yake.

Dhana hizo mbili nitakazozitaja hapa ukiongeza na ripoti ya daktari kama ilivyobainisha ndivyo vinavyotupa kichwa cha habari katika makala hii ya ‘Utatu wa kifo cha Kanumba.’

Tukiachana na ripoti ya daktari, wapo wanaoamini kuwa Kanumba aliuawa na Freemason na cha kushangaza zaidi kwenye dhana hii ya kwamba Kanumba aliuawa na Freemason, wengi ni viongozi wa dini. Tena wapo viongozi wakubwa kabisa katika makanisa na hata misikiti wanaoamini kwamba Kanumba aliuawa na Fremason.

Mfano rahisi ni kijana aliyekuwa mhubiri wa mitaani (Street Preacher) George Kairuki maarufu kama Nabii Kairuki. Huyu alikwishatangaza sana kwamba Kanumba aliuawa na Freemason na si mitaani tu bali amewahi kusikika hata kwenye vituo vya redio akitangaza jambo hili na kulitolea shuhuda mbalimbali.

Kuna wakati Nabii Kairuki alifika mbali na kusema kuwa siku chache kabla ya Kanumba kufariki, alimfuata na kumweleza kwamba Fremason wanataka kumuua kwa sababu amekataa kumtoa mama yake kama sadaka. 

Kwanini nimesukumwa kuandika makala haya? Kuna vitu nataka kuviweka sawa hapa ili jamii ijichagulie kile itakachoona ni sahihi kubaki nacho katika utatu wa kifo cha Kanumba.

Jambo la kwanza, napinga kwa nguvu zote madai yote kwamba kifo cha Kanumba kina mkono wa Freemason. Sipingi uwepo wa Freemason wala sipingi kwamba Freemason hawaui watu, ninachopinga ni Freemason kuhusika na kifo cha Kanumba.

Nitaeleza dhana hii ilipoanzia, historia ya Kairuki, watu walioshupalia dhana hii mpaka ikakua, Kanumba aliizungumzia vipi Freemason enzi za uhai wake na baada ya hapo ndipo nitaizungumzia dhana ya utatu wa kifo cha Kanumba.

USIKOSE KUPERUZI Tanzania PANORAMA Blog ILI USIPITWE NA SEHEMU YA PILI YA MAKALA HAYA.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya