RAMADHANI MSANGI, RSA TANZANIA
IDADI kubwa ya madereva bodaboda wanaopata ajali na kulazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) si wanachama wa huduma za bima ya afya, jambo linalosababisha familia zao kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia matibabu yao huku wale wasio na ndugu, mzigo wa kuwahudumia ukipelekea sekta ya afya kukabiliwa na changamoto kubwa.
Hayo yamebainishwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa taasisi hiyo, Theresia Tarimo wakati akiwakaribisha mabalozi wa usalama barabarani kutoka RSA Tanzania, waliotembelea taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya waathirika wa ajali za barabarani duniani, yaliyofanyika mwisho wa wiki.
Theresia alisema kuwa gharama za matibabu kwa majeruhi wa ajali za barabarani ni kubwa kwa wagonjwa wanaolazwa wenye kuhitaji kufanyiwa upasuaji kwani gharama ya kumtibu mgonjwa mmoja mwenye kuhitaji upasuaji, inaweza kuwa zaidi ya Shilingi milioni mbili, kiasi ambacho ni kikubwa mno kwa familia nyingi ambazo hali zao kiuchumi ni ndogo.
“Hata hivyo, changamoto hii ya mzigo wa matibabu inaweza kuepukika endapo sote tutakuwa na utamaduni wa kujiunga na huduma za bima ya afya ambazo hivi sasa zimekuwa zikipatikana kwa urahisi na kwa unafuu kulinganisha na gharama za matibabu ambazo mgonjwa atatakiwa kuzibeba endapo ataumwa akiwa hana bima” alisema na kuongeza kuwa;
“Ndugu zetu waendesha bodaboda na madereva wa vyombo vingine vya moto kwa ujumla ni kundi ambalo liko kwenye hatari ya kukumbwa na majanga ya ajali za barabarani ambazo zinaweza kuzifanya familia kuwa na mzigo mkubwa wa kumpoteza aliyekuwa akitafuta kipato cha familia lakini pia kumhudumia akiwa hospitali, hivyo ni vema wakajiunga na mifuko ya bima ya afya ili kuepuka mzigo huu pale wanapokumbwa na majanga,” alifafanua zaidi.
Afisa Ustawi huyo alisema kuwa changamoto ya wagonjwa wengi kutomudu gharama za matibabu imekuwa pia ikiliongezea Taifa mzigo mkubwa katika kuboresha huduma za afya kwani fedha ambayo ingewekezwa kuimarisha sekta hiyo, zimekuwa zikilazimika kuelekezwa katika kuhudumia wagonjwa wasio na uwezo wa kujigharamia matibabu, wakiwemo pia wale ambao hawana ndugu.
“Nitoe wito kwenu mabalozi wa usalama barabarani kuchukua pia jukumu la kuwa mabalozi wa kuhamasisha madereva na Watanzania kwa ujumla kujiunga na mifuko ya bima ya afya ili iwe rahisi kwao kupata matibabu wanapopata majanga, bila kuhofia kuteteresha mustakabali wa familia zao kiuchumi,” alihitimisha Theresia.
Kwa upande wake Josephine Hiza, ambaye ni Afisa Muuguzi wa wodi namba 3A ambayo ni moja ya wodi zinazohudumia wagonjwa watokanao na ajali za barabarani aliwashukuru mabalozi hao kwa msaada waliotoa kwa wagonjwa huku akitoa wito kwa wadau zaidi kujitokeza kutoa misaada mara kwa mara bila kusubiri siku maalumu kama hiyo ya kukumbuka waathirika wa ajali.
“Kuna wagonjwa wengi ambao huletwa hapa na wasamaria wema waliowaokota huko barabarani baada ya kupata ajali, hawa wanakuwa hawana ndugu, jamaa wala marafiki wa kuwahudumia japo mahitaji yao kama chakula na mavazi, hivyo nitoe rai kwa mabalozi wa RSA Tanzania, kuimarisha utaratibu huu wa kutembelea vituo vya afya na kutoa misaada kwa wenye uhitaji,” alifafanua muuguzi huyo.
Akielezea kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi wa Mipango na Utawala katika RSA Tanzania, Augustino Mkumbo alisema kuwa, asasi yake kwa kushirikiana na ile ya Shirikisho la Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, waliamua kufanya hivyo ikiwa ni utekelezaji wa kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo.
“Tumeungana na wenzetu katika mataifa mbalimbali duniani kuadhimisha siku hii kwa kutembelea na kuwapa msaada wagonjwa watokanao na ajali za barabarani ikiwa ni utekelezaji wa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni kuwakumbuka waliofariki kwa ajali, kuwasaidia waliopata majeraha kutokana na ajali na kuchukua hatua ili kupunguza ajali na madhara yake,” alisema balozi Mkumbo
Misaada iliyokabidhiwa ni pamoja na fedha taslimu, sabuni za kufulia na kuogea, miswaki na dawa zake, maji na juisi ambavyo vilitokana na michango ya mabalozi wa usalama barabarani kutoka maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na michango ya wanachama wa Shirikisho la Bodaboda Dar es Salaam.
Maadhimisho ya siku ya waathirika wa ajali za barabarani duniani hufanywa kila mwisho wa wiki ya tatu ya mwezo Novemba kila mwaka. Siku hii iliasisiwa na Shirika la Road Peace la Uingereza, mwaka 1993 kabla ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Afya Duniani kuitambua na kuijumuisha siku hii katika matukio rasmi ya UN kuanzia mwaka 2015.
Huu ni mwaka wa nne sasa tangu Shirika la RSA Tanzania lianze kufanya maadhimishi ya siku hii hapa nchini ambapo tangu kuanza kufanya shughuli hii wapo waathirika ambao wamepata msaada wa kukatiwa bima ya afya kwao na familia zao pamoja na kuendeshwa kwa makongamano ya usalama barabarani.