HIVI NDIVYO NINAVYOMFAHAMU DIAMOND PLATINUMZ 5
HAMEES SUBA
ILIPOISHIA
MALALAMIKO yalipungua kidogo kidogo hadi yakatoweka kabisa. Diamond akaanza kuzoeleka kihabari, ikaonekana si tatizo tena jina lake kuandikwa katika kurasa za mbele na nyuma magazeti kwani hata magazeti mengine ya udaku ya nje ya kampuni yetu nayo yalishaanza kumtumia kihabari na hata kumuweka katika kurasa hizo.
TUUNGANE NAYO…
Tangu kuachiwa kwa wimbo wa Mbagala na kukamilika kwa albam na kuingizwa sokoni wimbo wa Mbagala, wimbo huo ndio ulioonekana kutamba zaidi na kuibeba albam hiyo kuliko hata wimbo wa nenda kamwambie uliokuwa tayari umeshampa Diamond tuzo tatu za Kilimanjaro Music Award.
Mashabiki wakazidi kumfahamu Diamond, Mbagala ukawa kama wimbo wa Taifa. Si kwenye daladala, redioni, mitaani na sehemu zote ambako muziki ulisikika ukakosa kusikia wimbo wa Mbagala ukichezwa.
Kwa ufupi ni kwamba kundi kubwa la mashabiki wa Diamond lilianza kumfahamia hapa. Wapo waliozifahamu nyimbo kama nenda kamwambie, nitarejea n.k baada ya kuusikia wimbo wa Mbagala, hivyo basi licha ya kwamba wimbo wa nenda kamwambie ndiyo uliomfungulia njia ya mafanikio Diamond lakini wimbo wa Mbagala ndiyo uliompatia umaarufu zaidi na mashabiki wengi zaidi.
Baada ya kutoka kwa albam hiyo ndipo kwa mara ya kwanza nikasikia tetesi kuwa Marehemu Rugemalila Mutahaba, maarufu zaidi kwa jina la ‘Ruge’ alimtaka Diamond. Sina maana kwamba Marehemu Ruge na Diamond hawakuwahi kukutana mpaka kufikia kipindi hiki bali ninachomaanisha ni kwamba taarifa rasmi za kimkakati kuwa Marehemu Ruge alitaka kumuweka Diamond katika himaya yake ndipo kipindi hiki nilipoanza kuzisikia.
Taarifa hizi nilizipata kwa watu wa karibu na Marehemu Ruge niliokuwa nikifanya nao kazi. Kwa mujibu wa taarifa hizo ilipangwa kuwa lazima Diamond atoke kwa watu waliokuwa wakimsimamia, yaani Aljazeerah Entertainment na kuwa chini ya Marehemu Ruge.
Hivyo basi ili ‘kumuwini’ Diamond kwanza iliazimiwa apewe shavu la kutumbuiza kwenye tamasha la Fiesta na baada ya hapo mambo mengine yataendelea.
Kweli, baada ya muda mfupi nikasikia Diamond akitajwa kwenye orodha ya wasanii watakaotumbuiza kwenye tamasha la Fiesta ikiwa ni mara yake ya kwanza. Papaa Misifa na menejimenti yake ya Aljazeereh Entertaiment walishangilia sana jambo hili bila kujua kwamba ulikuwa ni mpango wa kuwaharibia mkate wao.
Nakumbuka Papaa Misifa aliniambia maneno haya; “Tajiri unastahili pongezi, hakika umefanya kazi kubwa sana, dogo (Diamond) kapata shavu la Fiesta, Ruge kumkubali msanii wetu kutumbuiza kwenye Fiesta si jambo la mchezo.”
Ukubwa wa tamasha la Fiesta kila mtu anaujua hivyo sina haja ya kufafanua sana kwanini Papaa Misifa alizungumza maneno hayo kwangu.
Lakini pamoja na ukubwa na hadhi ya tamasha hilo ambalo moja ya msingi na malengo yake ni kutoa fursa kwa wasanii kuonesha vipaji vyao kupitia njia ya majukwaa ya tamasha hilo, nyuma ya pazia ukweli ulikuwa kwamba endapo ikitokea msanii kutokuwa na uhusiano mzuri na Marehemu Ruge au Clouds FM au na chochote chenye uhusiano na vitu hivyo viwili, basi msanii huyo ataishia kulisikia tamasha hilo redioni au kwenye Televisheni.
Ilikuwa ni vigumu kwa msanii kupata nafasi ya kushiriki kwenye tamasha hilo akiwa anapisha kwa chochote na mihimili hiyo miwili. Shuhuda ziko nyingi lakini kwa kuwa sio mada ya msingi ya andiko hili basi na itoshe tu kuelewa kwa hayo machache.
Kutokana na mazingira hayo na mambo mengine ya kiutendaji ndipo uzito wa tamasha la Fiesta ukajengeka. Kila msimu unapowadia wasanii walipandwa na presha huku wengi wakifanya kila jitihada za kujiweka kwenye uhusiano mzuri na mtandao wa Marehemu Ruge ili kuhakikisha wanakuwemo kwenye ‘listi’ ya wasanii watakaotumbuiza kwenye Fiesta.
Safari hii ikawa ni zamu ya Diamond kwenda kudhihirisha kipaji chake lakini nyuma ya pazia kukiwa na ajenda ya siri ambayo hata akina Papaa Misifa hawakuifahamu. Sina uhakika kama Diamond alikuwa akiifahamu ajenda hiyo au la lakini nina uhakika wa kutosha kuwa menejimenti ya Aljazeerah haikuwa ikifahamu chochote, wao walichukulia poa tu wakiamini kuwa ni zari limemdondokea msanii wao hivyo walipaswa kupiga makofi, vigelegele na kushangilia.
Siku ya siku ikafika, Diamond akaingia tamashani akiwa na kete za kutosha kuwadhihirishia mashabiki kuwa na yeye yumo. Bonge la ‘show’ likadondoshwa ndani ya viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam mbele ya maelfu ya mashabiki waliokuwa wamehudhuria tamashani. Katika kudhihirisha kuwa albam ilikuwa imeshaeleweka kwa mashabiki, baadhi walisikika wakimsindikiza Diamond kwenye kuimba viiitikio (chorus), viungio (bridges) na hata mashairi (lyrics) ya nyimbo zake.
‘Show’ ilikuwa ‘bab kubwa’ na ilipomalizika kila mtu akabaki na simulizi tofauti tofauti kuhusu alichokishuhudia kutoka kwa Diamond. Baadae ya ‘show’ hiyo uhusiano ya Diamond na Marehemu Ruge ukaendelea kuimarika siku hadi siku, haukupita muda mrefu nikasikia tena Diamond kapatiwa ‘dili’ nyingine na Marehemu Ruge ya Kwenda nchini Senegal kurekodi na mwanamuziki nguli wa Afrika, Youssou Ndour.
‘Dili’ hii lilitokana na ule mradi wa kupiga vita Maleria uliojulikana kama ‘Malaria No More.’ Mradi huu pia ndio ule ulioleta matatizo makubwa sana ya kiuhusiano kati ya Marehemu Ruge na ‘Legendari’ wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu au kwa majina mangine Mr II na 2 Proud, tuyaache hayo.
Yote kwa yote sijui ‘dili’ hiyo ilikwendaje kwa sababu mpaka leo hii ninapoandika andiko hili sijawahi kuusikia wimbo aliorekodi Diamond na Youssou N’dour kupitia mradi huo. Niliwahi kusikia tetesi kuwa Youssou N’dour aligoma kurekodi na Diamond kwa madai kwamba hakuwa na ubora wa kumix’ kazi zao hasa kwenye upande wa key, codes na vocal.
Kama unavyojua wanamuziki wa zamani wengi ni wafuasi wa muziki unaofuta mpangilio wa kitaaluma zaidi kuliko kipaji. Lakini kwa kuwa hakuna maelezo ya kutosha kuhusiana na tetesi hizo na kile kilichotokea nchini Senegal, hebu tuliache hili.
Hakika kilikuwa ni kipindi chenye mambo mengi kwenye kumbukumbu zangu. Kama sikosei ni katika kipindi hiki ambapo Diamond alifiwa na bibi yake kipenzi. Nasema bibi yake kipenzi kwa sababu najua ni namna gani bibi huyo alivyokuwa akimchukulia Diamond.
Ni bibi aliyekuwa na mapenzi makubwa sana kwa mjukuu wake kwa maana ya Diamond na Diamond pia alikuwa akimpenda sana bibi yake huyu kwani alikuwa haishi kumzungumzia kila wakati tulipokuwa tukipiga stori za kimaisha, (Mungu amuweke mahala pema peponi, amina).
Katika kudhihirisha upendo wa Diamond kwa bibi yake huyu wakati wa ‘kushuti’ video ya nenda kamwambie, Diamond aliomba bibi yake aingizwe katika video hiyo kama kumbukumbu na ilifanyika hivyo, na hili tuliachie hapa.
Lakini kipindi kifupi baadaye Diamond alipata msiba mwingine baada ya kuondokewa na mjomba wake (Mungu amuhifadhi mahali pema peponi, amina). Nadhani ilikuwa ni kipindi anatoa albamu yake ya pili.
Kutokana na vifo hivi viwili kutokea wakati Diamond akiwa kwenye utoaji wa albam zake kuliibuka maneno ambayo kimsingi hayafai kuyasimulia hapa, hivyo tuyaache hapo.
Lakini katika kipindi hiki pia, ndipo nilipopata taarifa za uhusiano wa kimapenzi kati ya Diamond na Hawa (mwanadada aliyeimba naye kwenye wimbo wa nitarejea). Nakumbuka nilikuwa nikipiga stori na mmoja wa wakurugenzi wa Aljazeera kuhusu maendeleo ya Diamond kuhusu nini cha kuongeza kwa ajili ya kuendelea ‘kumbusti’ zaidi ya pale alipokuwa amefika.
Mkurugenzi huyo akaniambia hivi: “Dogo anakwenda vizuri na nyota yake inazidi kung’aa lakini ameshaanza kujiingiza kwenye mambo ya mapenzi, asipokuwa makini hii inaweza kumuondoa kwenye reli”
Nilipomdadisi zaidi ndipo akafunguka kwamba Diamond alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Hawa na alikuwa akikaa naye nyumbani kwao Tandale.
Katika kunithibitishia hilo akaniambia uhusiano wao ulianza wakati Hawa akiwa anauza duka la nguo la Zizzou Fashions lililokuwa maeneo ya Afrika Sana, jirani na Atriums Hotel. Akasema walikwenda na Diamond kwenye duka hilo kununua nguo kwa ajili ya video ya Mbagala ndipo akakutana na Hawa na kuanzisha uhusiano.
Uhusiano wao haukufahamika sana licha ya kudumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na ulikuja kufa ukiwa hauna ‘kick’ yoyote kama ilivyokuja kutokea kwenye uhusiano wake na wasichana wengine.
Baada ya uhusiano huo kufa, Hawa alipoteza mwelekeo kabisa kwani hakuwika tena kimuziki na wala hakusikika kwenye vyombo vya habari kuhusu shughuli zake zozote. Mara ya mwisho mimi kukutana na Hawa ilikuwa mwaka 2017 huko Kigamboni akiwa kwenye kituo cha Sober House akimalizia dozi yake ya kumuondoa kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa maana hiyo hapo katikati Hawa alijiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya hali iliyosababisha kuua kipaji chake cha muziki na kumvurugia ndoto zake nyingi za maisha. Mungu amlinde na kumuongoza kama alifanikiwa kumaliza kutumia dawa hizo.
DIAMOND NA VESPA
Baada ya Diamond kuanza kuzishika noti, siku moja nikiwa naendesha gari barabara ya Tandale kuelekea Sinza, nikiwa eneo la Tanesco, ghafla pikipiki aina ya Vespa ‘iliniovateki’ kwa mwendo wa kasi sana. Uendeshaji huo haukunifurahisha.
Haikwenda mbali sana ikapunguza mwendo na kukata upande wa kushoto kuelekea njia za uswahilini. Kwenye gari nilikuwa na marehemu Boni, ndugu yake na Papaa Misifa, yule anayeonekana kwenye video ya nenda kamwambie. Akanisikia nikisonya kutokana na kutofurahishwa na kitendo cha mwendo kasi wa ile Vespa. Akanitazama akacheka, kisha akasema; “Unakasirika nini haya yote umeyasbabisha mwenyewe.”
Sikumuelewa alichomaanisha lakini kabla sijamuuliza chochote akaniongeza neno hili; “Mwanao huyo ndio anakufanyia vurugu barabarani.”
Alimaanisha kuwa aliyepita na ile Vespa kwa mwendo wa kasi alikuwa Diamond. Sikuamini alichokuwa ameniambia, nikamuuliza; “kaanza lini kuendesha Vespa na mbona mwendo anaokwenda nao ni wa hatari sana?”
Akajibu; “Mambo ya ujana, hiyo Vespa ni ya kwake kainunua.”
USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA SITA YA SIMULIZI HII YA KWELI NA YENYE MAFUNZO MENGI