Wednesday, December 25, 2024
spot_img

SERIKALI ‘YAAMKA’ SKANDALI YA MECCO

RIPOTA PANORAMA

HATIMAYE Serikali imetoa kauli kuhusu skandali ya kuporwa kwa ardhi na mali za umma na kutumika kuchukua mkopo wa mabilioni ya Shilingi katika benki mbili kubwa za hapa nchini, ukiwemo mkopo usiokuwa na ukomo.

Serikali imesema iko macho, inaifahamu skandali hiyo na inaifuatilia kwa karibu na kwamba katika kipindi kifupi kijacho mwelekeo wa jambo hilo utafahamika..

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Eric Mkuti amekiri kufahamu kuwapo kwa sehemu kubwa ya taarifa zilizotolewa na Tanzania PANORAMA Blog.

Alikua akijibu maswali ya Tanzania PANORAMA Blog ambayo iliiuliza hatua ambazo Serikali imechukua baada ya Kampuni ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) kupora mali ya umma ikiwemo kumega hisa za Serikali asilimia 25 inazomiliki kwenye Kampuni ya Mwananchi Engeenering and Contracting Company Limited (MECCO), na baadae kubadili hati kwenda kampuni ambayo si mbia wa MECCO.

Mbia mkuu kampuni ya SISICOL alihamisha hati za ardhi za eneo la MECCO kwenda Mas Holding and Container Depot Limited, ambao si wabia.

“Nimeelekezwa nijibu maswali yako, naomba nikujibu maswali yote uliyomuuliza Msajili wa Hazina. Serikali ilifanya ufuatiliaji na tukabaini kuwa ni kweli huyo mbia, Kampuini ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) alikuwa amepunguza hisa za Serikali kinyemela.

“Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ililiweka jambo hilo wazi na Serikali ilichukua hatua na hivi tunavyoongea hisa za Serikali ambazo zilikuwa zimechukuliwa kinyemela zimeisharejeshwa, na hata wewe ukienda kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela) utakuta hisa zote za Serikali asilimia 25 zipo,” alisema Mkuti.

Mkuti alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ( CAG) katika ripoti yake alionyesha kuwa mwanahisa mwenye hisa nyingi, asilimia 75 katika kampuni ya MECCO alikuwa amechukua kinyemela hisa za mwanahisa mdogo ambaye ni Serikali kutoka asilimia 25 na kumbakiza hisa asilimia 2,6 tu.

Alisema Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifuatilia hila hiyo iliyokuwa imefanywa na SISICOL na kufanikiwa kurejesha hisa zake zote.

Akizungumzia hila nyingine iliyofanywa na Kampuni Mas Holding and Container Depot Limited ambayo ni kampuni dada ya SISICOL ya kubadilisha kinyemela hati za viwanja viwili, kiwanja namba mbili na kiwanja namba 3B vilivyopo barabara ya Nyerere, Manispaa ya Temeke, ambayo ni mali ya MECCO kutoka MECCO kwenda kwenye umiliki wa Mas Holding and Container Depot Limited, Mkuti alisema hata hilo Serikali inalifahamu na imekwishachukua hatua.

“Hata hilo Serikali inalifahamu, inafahamu hila iliyofanyika na imekwishachukua hatua ingawa kulitokea mkwamo kidogo lakini umma uelewe kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu sana jambo hilo.

“Kwenye ule ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG ilibainika kuwa mwanahisa mkubwa alihamisha umiliki wa baadhi ya mali za MECCO kwenda kwenye umiliki wa kampuni yake ya SISICOL kama sehemu ya malipo ya deni la mwanahisa huyo lililoingizwa kwenye vitabu mwaka 2008.

“Kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa uendeshaji wa Kampuni ya MECCO baina ya Serikali na mbia wake huyo, yeye ndiye mwenye jukumu la kusimamia shughuli za kila siku za kampuni lakini hilo siyo ruhusa kwake kuhamisha mali.

“Serikali baada ya kulibaini hilo kama nilivyokwambia baada ya kufanyika kwa ukaguzi, iliamriwa mali za MECCO ambazo zilikuwa tayari zimefanyiwa mabadiliko ya hatimiliki na kusomeka jina la MAS Holding and Container Depot Limited zirejeshwe katika umiliki wa MECCO.

“Msajili wa Hazina alisimamia kazi hiyo ya utekelezaji wa uamuzi huo na hatua za kubadilisha umiliki wa hati hizo kurudishwa kwenye umiliki wa MECCO zilianza hadi kufika hatua ya kufanya malipo ya stamp duty na capital gain ili kukamilisha taratibu za kubadilisha umiliki.

“Katika hilo MECCO ilifanya malipo ya stamp duty kisha ikaomba kupatiwa msamaha wa capital gain tax lakini Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitoa maelekezo kuwa hesabu za Kampuni ya MECCO na zile za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited ni lazima ziwasilishwe kwa mamlaka hiyo ili ifanye makadirio ya kodi kabla ya kuangalia huo msamaha.

“Hao jamaa hawakufanya kilichosemwa na TRA na badala yake wakakimbilia kwa Waziri wa Fedha na Mipango ambako nako walirudishwa TRA kwani aliwaambia watekeleze walichoambiwa na TRA.

“Hapa nikwambie tu kuwa hawajatekeleza hayo maagizo ndiyo maana kuna mkwamo lakini Serikali inafuatilia kwa karibu sana,” alisema Mkuti.

Akijibu swali jingine lililohusu Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited kutumia hati za viwanja namba mbili na kiwanja namba 3B vilivyopo barabara ya Nyerere, Manispaa ya Temeke ambavyo ni mali ya MECCO kuchukua mkopo mkubwa katika moja ya benki hapa nchini pasipo kuihusisha Serikali ambayo ni mbia wake na hadi sasa mkopo huo haujarejeshwa alisema hata hilo pia Serikali inalifahamu na inalifanyia kazi.

“Hata hilo Serikali inalifahamu na imeishachukua hatua. Msajili wa Hazina alifanya mawasiliano na Benki ya NBC na hatua za kurejesha umiliki wa hati hizo zilianza lakini kama nilivyoeleza kulitokea mkwamo kidogo baada ya hawa jamaa kutowasilisha hesabu zao TRA.

“Unajua hawa jamaa wao ndiyo wanasimamia uendeshaji wa kila siku wa Kampuni ya MECCO kwa hiyo kila kitu wanasimamia wao lakini kama nilivyosema huo siyo mwanya wa wao kuvunja sheria au kwenda kinyume. Kinachofanyika Serikali inawasubiri kwenye mkutano wa wanahisa, katika majadiliano yatakayofanyika hapo mwelekeo wa jambo hilo utafahamika.” Alisema Mkuti.

Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa mkutano wa wana hisa haujaitishwa kwa muda mrefu alisema safari hii lazima utaitishwa kwa sababu mwaka jana haukuitihswa lakini pia hivi sasa Serikali inafuatuilia kwa karibu suala hilo.

“Mkutano wa wanahisa huwa unafanyika ndani ya miezi 18, mwaka jana haukuitishwa, hawakufanya mkutano hivyo mwaka huu lazima ufanyike na Serikali itawakilishwa na Msajili wa Hazina. Kwenye mkutano huo yatafanyika majadiliano ya kina na mwelekeo wa jambo hilo kutoka hapo utafahamika,” alisema Mkuti.

Akizungumzia kutoitwa kwa mjumbe mpya wa bodi kwa upande wa Serikali aliyeteuliwa mwaka jana kuchukua nafasi ya Marehemu Mhandisi Patrick Mfugale alisema hajaitwa kwa sababu tangu alipoteuliwa bodi hiyo haijafanya mkutano.

Kampuni ya SISICOL ambaye ni mwanahisa mkubwa  mwenye hisa asilimia 75 katika uendeshaji wa Kampuni ya Mwananchi Engeenering and Contracting Company Limited (MECCO) alipora hisa za Serikali yenye hisa asilimia 25 na kuibakiza hisa asilimia 2,6

Baada ya kufanya hilo, kampuni hiyo ilipora baadhi ya mali za MECCO ikiwa ni pamoja na kubadilisha umiliki wa hati za viwanja viwili kisha kuziweka dhamana benki ambako ilichukua mkopo mkubwa pasipo kuitaarifu Serikali.

Kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa uendeshaji wa Kampuni ya MECCO baina Serikali ya mbia wake huyo, ndiye mwenye jukumu la kusimamia shughuli za kila siku lakini si kuhamisha mali za kampuni hiyo ya umma.

Kwa mara ya kwanza Tanzania PANORAMA Blog iliripoti skandali hii mwezi April, mwaka huu na kukutana na vitisho vya hapa na pale lakini alisimama kidete kuuhabarisha umma ukweli.

USIKOSE KUSOMA RIPOTI MAALUMU KUHUSU SKANDALI HII HAPA TANZANIA PANORAMA BLOG

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya