MAUREEN MALLYA
MMOJA wa bibi zangu aliyefariki miezi michache iliyopita alikuwa na mali nyingi sana; majumba, viwanja na magari ya kifahari, alikuwa tajiri na watoto wake waliishi walipendana sana. Lakini kabla hajamaliza mwaka mmoja tangu mauti yalipomkuta watoto wake japo ni watatu hawaongei, kisa wanagombea mali ambazo hata wao hawawezi kuzimaliza.
Mbali na bibi yangu huyo, mmoja wa babu zangu alifariki akiwa ameacha nyumba zaidi ya saba lakini mirathi yake ilisumbua kwa zaidi ya miaka 20.
Matatizo yote haya yalitokea kwa sababu waliogopa kuandika wosia au walidhani familia zao hasa watoto wanapendana na watagawana mali bila kugombana, lakini imani hiyo ikawa kinyume.
Wanasema “ukimpenda utamlinda,” huu msemo ni vema kila mtu akiukariri kama ‘table’ ya tano katika hesabu. Kama unampenda mkeo na watoto wako basi huna budi kuwalinda.Mapenzi yawekwe kwenye vitendo na sio maneno maana maneno matupu hayavunji mfupa.
Kila siku tunatembea na kifo kama kivuli. Hakuna anayejua saa wala dakika ambayo Mungu ataitisha namba yake. Hatuna budi kujipanga na kuweka kila kitu sawa ili kurahisisha maisha ya wale tunaowaacha nyuma.
Watu wengi wamefariki na kuziacha familia zao kwenye wakati mgumu kiuchumi na migogoro isiyokuwa ya lazima. Ni muhimu kupanga mambo yako mapema bila kujali kama una mali nyingi au la maana hata kuandika unataka uzikwe wapi ni muhimu pia.
Watu wamefariki na kuwaacha ndugu na familia zao katika ugomvi wa kugombea miili yao kwenda kuizika, wanaoachwa wanabaki wakigombania mwili wa marehemu, wanaogombana, kila mmoja anataka marehemu akazikwe sehemu anayoiona yeye inafaa.
Wapo wajane na watoto waliojikuta wakinyang’anywa mali na ndugu na kuachwa bila kitu. Mifarakano katika familia na tatizo la kuchukua muda mrefu kuendesha kesi za mirathi ni mambo yanayoonyesha/kusisitiza umuhimu wa wosia.
Hebu tujifunze kidogo kuhusu wosia, aina za wosia, faida zake na namna ya kuuandaa na kuuhifadhi.
Wosia ni kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake mwenyewe kuonyesha nia yake; jinsi gani angependa mali yake igawanywe baada ya yeye kufariki.
Kuna faida nyingi za kuandaa wosia na baadhi ya hizo ni kama zifuatazo. Mtu anapata nafasi ya kugawa mali zake kwa warithi wake na kuamua namna mali zake zitakavyosimamiwa.
Wosia unampa mtu nafasi ya kumchagua msimamizi wa mali zake, huepusha watu wadanganyifu kujinufaisha na mali zake, lakini faida kubwa zaidi ya wosia ni kuiepusha familia na migogoro yoyote inayoweza kujitokeza kuhusu mali pindi mwenye nazo unapofariki.
Matatizo mengi ya miradhi yangeepukika kwa asilimia mia moja kama watu wangeacha wosia kabla ya umauti kuwakumba.
Kuna wosia wa aina mbili; mosi ni wosia wa maandishi na pili ni wosia wa mdomo/matamshi. Wosia wa maandishi ni wosia ambao muusia anaandika wosia yake kwenye karatasi.
Wosia wa maandishi kukubalika kisheria lazima uzingatie haya yafuatayo. Wosia wa maandishi lazima uandikwe kwa kalamu ya wino au uchapwe. Muusia awe na akili timamu, ataje tarehe ulipoandikwa, ataje kuwa muusia anayo akili timamu na ameandika wosia kwa hiari yake mwenyewe.
Pia ushuhudiwe na mashahidi wawili wanaojua kusoma na kuandika (mmoja wa ukoo / familia na mwingine mtu baki) kama muusia anajua kusoma na kuandika au kama muusia hajui kusoma wala kuandika wosia wake ushuhudiwe na mashahidi wasiopungua wanne (wawili wa ukoo na watu baki wawili).
Ila ikumbukwe kuwa warithi wa mtoa wosia hawaruhusiwi kushuhudia wosia. Wosia unatakiwa usainiwe na muusia mbele ya mashahidi wake wakiona. Mtoa wosia kwenye wosia wa maandishi anatakiwa aweke sahihi yake au kama hajui kusoma aweke alama ya dole gumba la kulia kwenye wosia na mashahidi waweke sahihi zao pia katika wosia huo.
Ni muhimu sana mashahidi wanaoshuhudia wosia wa muusia wawe wamechaguliwa na muhusika mwenyewe. Sio takwa la kisheria kwa mashuhuda kusoma maudhui ya wosia wa mtoa wosia kama mtoa wosia hatakuwa tayari kuweka bayana yaliyomo ndani ya wosia wake.
Mtoa wosia anayo haki ya kubadili wosia wake na wosia mwingine wa maandishi kwa kufuata taratibu hizo hapo juu lakini lazima aseme kwamba “wosia huu unabatilisha /futa wosia mwingine wowote ulio tangulia” ili kuondoa migogoro.
Kwa wosia wa mdomo ni lazima uzingatie haya yafuatayo; ushuhudiwe na mashahidi wanne (wawili wa ukoo na wawili watu baki). Mtoa wosia awe na akili timamu na mashahidi wachaguliwe na mtoa wosia mwenyewe.
Endapo mashahidi watakufa kabla ya mtoa wosia kufa, wosia hautakubalika na urithi utagawanywa kama urithi usio wa wosia hivyo basi kama mtoa wosia anataka kuwosia mali zake inabidi atoe wosia mpya mbele ya mashahidi wengine.
Wosia wa mdomo hauwezi kubatilisha wosia wa maandishi lakini wosia wa maandishi unaweza kubatilisha wosia wa mdomo.
Ni ushauri wangu kwa jamii kuwa ni vema mtu kuandaa wosia wa maandishi. Wosia huu unakua salama zaidi kwa sababu ni vigumu watu kubadilisha matakwa ya mtoa wosia.
Kama ilivyo muhimu kuandaa wosia ni muhimu zaidi kuuhifadhi mahali salama. Wosia unaweza kuhifadhiwa RITA na mtoa wosia anapofariki, msimamizi wa wosia atauchukua RITA na taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Pia wosia unaweza kuhifadhiwa kwa mwanasheria wa mtoa wosia au nyumbani. Muhimu uwe sehemu salama na uweze kunufaisha walengwa baada ya kifo cha muhusika.
Ni muhimu kukumbuka kwamba sisi wote tutakufa. Hakuna mtu atakae ishi milele hapa duniani. Wote sisi ni wasafiri hivyo yatupasa kuishi vema na kuweka mambo yetu vizuri wakati wote.
Mawazo ya kuogopa kuandika wosia kwa kuhofia kinachosemwa na baadhi yetu kuwa ni kujichukulia kifo ni mawazo hasi na yameshapitwa na wakati. Kama kweli unaipenda familia yako basi uilinde mapema.
Inasikitisha sana kuona matajiri wakubwa, wenye mali nyingi wanakufa na kuacha migogoro mikubwa kwenye familia zao kwa sababu ya mali walizochuma wakati wa uhai wao.
Masikini anapofariki mara nyigi kunakua hakuna migogoro ya kugombea mali lakini anapofariki mtu mwenye uwezo kunakua na balaa kubwa. Waswahili wanasema ukubwa wa pua sio wingi wa kamasi lakini kwenye mirathi, huu msemo huwa kinyume.
Wosia sio lazima, wosia ni hiyari lakini nadhani ni wakati sahihi kwako wewe kujiuliza, je unaipenda familia yako? na je ungependa wawe na maisha gani baada ya kifo chako? Ukiweza kuyajibu maswali haya vizuri ndio ufanye uamuzi sahihi kwa maisha yako na maisha ya uwapendao.
Na wosia pia sio kwa ajili ya akina baba peke yao, hapana hizi ni fikra potofu. Mtu yeyote mwenye umri zaidi ya miaka kumi na nane ana haki ya kuwa na wosia. Ifahamike kuwa sio lazima ubarikiwe kuwa na mali nyingi ndio uandae wosia.
Wosia unahusu mambo mengi zaidi ya mali kama vile wapi unataka kuzikwa, nini kifanyike kwenye mazishi yako, wadeni wako, wadaiwa na kadhalika.
Ikumbukwe, maiti haiulizwi sanda na maji yakimwagika hayazoleki. Ni wakati sasa tupendane kwa vitendo. Nikukaribishe wewe msomaji wangu sasa ujitathinini wewe na mali zako kisha uandike wosia wako.