RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Mapato (TRA) jana ilijikuta katika mtihani mzito wa kutoa ufafanuzi wa majibu ya maswali sita iliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu masuala ya kikodi yenye utata.
Hayo yalitokea baada ya Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo kushindwa kutoa ufafanuzi wa majibu ya maswali aliyokuwa ameulizwa awali na Tanzania PANORAMA Blog huku akilalamika kuandamwa na maswali kwa muda wa wiki mbili mfululizo.
Tanzania PANORAMA Blog ilitaka ufafanuzi wa majibu yaliyotolewa na TRA ambayo yaliacha maswali yasiyokuwa na majibu ambapo msingi wa kuibuka kwa maswali hayo ni madai kuwa kampuni ya usafirishaji nafaka nje ya nchi ya Nine Five Group imekuwa ikicheza mchezo mchafu.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog awali zilidai kuwa Kampuni ya Nine Five Group imekuwa ikitumia nyaraka zenye dosari kusafirishia makontena ya nafaka kutoka hapa nchini kwenda nje ya nchi na kwamba imekuwa ikifanya hivyo kwa msaada wa baadhi ya watumishi wa kampuni moja ya uwakala wa usafirishaji na upokeaji mizigo.
Ilidaiwa kuwa dosari zilizo kwenye nyaraka za Kampuni ni Nine Five Group ni pamoja na baadhi ya ‘release order’ zinazotolewa na TRA kwa kampuni hiyo kutoonyesha idadi na namba ya kontena wanazosafirisha kwenda nje ya nchi.
Pia ilidaiwa zaidi kuwa Kampuni ya Nine Five imekuwa akikaa na ‘release order’ zinazotolewa na TRA kwa zaidi ya wiki tatu hali inayoibua shaka ya kutumiwa kwa matumizi mengine tofauti na yaliyokusudiwa.
Vyanzo vya habari kutoka kampuni ya uwakala wa usafirishaji na upokeaji mizigo iliyohusika na usafirishaji wa kontena hizo vimedai kuwa ‘release order’ ni moja ya hatua za mwisho baada ya kampuni husika kukamilisha nyaraka zote za usafirishaji hivyo haipaswi kukaa muda mrefu kwa mteja bila kutoa mzigo ulipohifadhiwa na kupelekwa bandarini.
“Inapotokea kampuni ikakaa na ‘release order’ kwa muda mrefu wa zaidi ya wiki tatu hamuoni kama kuna ujanja unaotumiwa na kampuni husika kusafirisha mizigo yake mingine kwa kutumia ‘release order’ hiyo kwa lengo la kudanganya idadi ya mizigo inayosafirisha?
“Siku waliposafirisha mizigo yao, ‘Loading permission’ ilionyesha kuwa kwa siku moja walisafirisha kontena 10 kwenda Qingdao, China lakini kontena hizi zote hazikuonekana kwenye ‘release order’ utaratibu huu sijui umeanza lini.
“Waliwezaje kusafirisha kontena kumi kwa siku moja kama inavyoonekana kwenye ‘loading permission’ lakini kwenye ‘release order’ hazionekani? Na kwenye ‘release order’ hiyo kuna malipo ya ‘gross weight’ zaidi ya milioni 80 kwa kilo zaidi ya 300,000, ni za nini?”
Ili kupata ukweli wa madai hayo, PANORAMA iliiuliza TRA iwapo ni ruksa kwa wafanyabiashara kutumia ‘release order’ moja kusafirisha mizigo zaidi ya iliyo kwenye ‘release order’ hiyo iliyopewa kwa mzigo iliyoombea? na TRA kupitia kwa Kayombo ilijibu kuwa siyo sahihi na haiwezekani lakini swali la pili liliuliza kuwa baadhi ya ‘release order’ zinazotolewa na mamlaka hiyo hazionyeshi idadi ya kontena zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi wala namba ya kontena hizo ambapo TRA ilijibu jibu fupi kuwa; hilo ni sahihi.
PANORAMA ilimuuliza Kayombo kuwa baadhi ya nyaraka zinazodaiwa kuibua mashaka ni zile zinazoonyesha kampuni hiyo ililipa ‘gross weight’ ya mamilioni ya shilingi. Je, kama biashara inayofanywa na kampuni hiyo haitozwi kodi, ‘gross weight’ iliyolipia ilikuwa ya nini na hapo Kayombo alitoa jibu jingine fupi kuwa; Hakuna kodi ya forodha kwenye nafaka labda walitapeliwa.
Pia Kayombo aliulizwa ‘Custom Clearence’ inalipwa TRA au kwenye taasisi nyingine ya Serikali naye alijibu kuwa ‘Customs’ hakuna kodi ya aina hiyo na swali lililofuata liliuliza; kama ‘release order’ hutolewa na TRA naye alijibu kuwa inatolewa na taasisi yake hiyo na haina malipo.
Swali jingine lilihoji; ‘kama mizigo ya ‘transit’ huwa hailipiwi kodi hapa nchini bali hupewa ‘release order’ baada ya gharama za bandari na taasisi nyingine zinazoshughulikia mzigo husika kulipwa, hii maana yake ni kwamba kuna mizigo inayostahili kulipiwa kodi na isiyostahili, naomba kujua mizigo ya ‘transit’ hulipiwa kodi wapi?’
Akijibu, Kayombo alisema hakuna kodi ya forodha kwenye mizigo ya ‘transit,’ kama kuna malipo watu wanalipa waseme wamelipa wapi? au waonyeshe ‘control numbers.’
Mlolongo wa maswali ulikuwa mrefu, lililofuata lilisomeka hivi; ‘kama ‘release order’ inayotolewa na TRA haitaji idadi ya mizigo wala namba za kontena zinazosafirishwa, je huko wanakolipia kodi huwa wanajuaje kodi ya mzigo ambao haujatajwa kwenye ‘release order’ na Kayombo alijibu; ‘hakuna kodi inayolipwa, idadi ya kontena inaonekana kwenye ‘loading declarations.’
Swali la mwisho liliuliza hivi; ‘naomba kuijua sheria inayoruhusu mizigo kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila kuainishwa kwenye ‘release order’ na Kayombo alijibu ‘ni utaratibu tu, sio sheria.
Baada ya Tanzania PANORAMA Blog kuandika habari iliyokuwa na kichwa cha maneno ‘TRA – hakuna kodi kusafirisha mazao ya chakula nje ya nje’ ikinukuu maelezo yaliyotolewa na Kayombo kuhusu kutokuwepo kodi katika usafirishaji mazao ya nafaka nje ya nchi, baadhi ya wasomaji wetu waliwasiliana nasi na kuomba ufafanuzi zaidi wa maelezo yaliyotolewa na Kayombo kwa kile walichodai kuwa yalikuwa majibu ya jumla, yasiyoeleweka vizuri na yanayoacha maswali mengi.
Tanzania PANORAMA Blog kwa kuzingatia majukumu yake ya kuelimisha na kuupasha umma habari sahihi, ilirejea tena kwa Kayombo ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA akiwa pia na dhamana ya usemaji kumuomba ufafanuzi wa majibu ya maswali iliyomuuliza awali na iliweka bayana kuwa ufafanuzi huo una lengo la kutoa elimu kwa umma, ilimuuliza;
Mosi, Mamlaka ya Mapato (TRA) imeeleza kuwa hakuna kodi ya forodha inayotozwa kwenye mizigo ya ‘transit,’ kwa faida ya wasomaji wetu, tunaomba kujua ‘custom value’ inayotajwa kwenye ‘release order’ ya TRA kwa mizigo ya ‘transit’ ina maana gani? Naye alijibu hivi; ‘Hakuna kodi kwenye transit, hiyo value ni kwa ajili ya statistics tu.’
Pili; Mamlaka ya Mapato (TRA) imeeleza kuwa kwenye ‘release order’ hakuna sheria iliyowekwa ya kuainisha namba ya kontena zinazosafirishwa wala idadi yake. Kwa faida ya wasomaji wetu, tunaomba kujua, je TRA inapotoa ‘release order’ bila kujua namba ya kontena wala idadi ya wanacho ki‘release’ tafasili yake ni nini? Naye Kayombo alijibu; ‘Cargo Ref Number ndio ina taarifa zote za mzigo, ipo pale kwenye release order.’
Swali la tatu ambalo Tanzania PANIORAMA Blog iliomba kupata ufafanuzi kutoka kwa Kayombo lilisomeka hivi; ‘Ikiwa kuainisha namba na idadi ya kontena kwenye ‘release order’ ni utaratibu tu na sio sheria kama ilivyoelezwa na TRA, Tanzania PANORAMA Blog inaomba kujua, je, ni sahihi kuvunja utaratibu kwa sababu sio sheria? Naye Kayombo alijibu, ‘Utaratibu upi unaovunjwa? Hakuna utaratibu uliovunjwa, idadi ya containers zote inaonekana kwenye ‘loading permission’ na ndio utaratibu wa mizigo ya ‘export,’ jibu ambalo haliendani na lile alilotoa awali kuwa kuainisha mzigo kwenye ‘release order’ si sheria bali ni utaratibu uliowekwa na TRA.
Nne lilisomeka; ‘Mbali na Kampuni ya Nine Five Group kudaiwa kuvunja utaratibu wa kuainisha idadi na namba za kontena kwenye ‘release order,’ Tanzania PANORAMA Blog inaomba kujua ni kampuni ngapi mlizoziruhusu au zilizojiamulia kuvunja utaratibu huo? Na jibu lake ni hili; ‘Hatujaruhusu utaratibu kuvunjwa.’
La tano. ‘Tanzania PANORAMA Blog inaomba kujua kuna haja gani kwa TRA kuunda utaratibu ambao hauna ulazima wa kuufuata? Naye alijibu; ‘Hatujawahi kufanya hivyo.’ Kayombo alitoa jibu hili ikiwa na siku chache tu baada ya kueleza kuwa kuanisha mizigo kwenye ‘release order’ ni utaratibu uliowekwa na TRA lakini siyo sheria lakini jana alikana kauli yake mwenyewe.
Aidha, aliulizwa hivi; ‘TRA imeeleza kuwa mizigo ya ‘transit’ hailipiwi kodi ya forodha, tunaomba kujua ni kodi zipi tofauti na forodha zinazolipwa kwa mizigo hiyo? Na yeye alijibu hivi; ‘Hakuna kodi yoyote.’
Mwisho aliulizwa, ‘TRA imeeleza kuwa ‘release order’ moja haiwezi kamwe kutumika kusafirisha mzigo zaidi ya uliokusudiwa, je, ikiwa ‘release order’ haitaji aina ya mzigo uliokusudiwa kusafirishwa, TRA inawezaje kufahamu kama mzigo unaosafirishwa ndio uliokusudiwa? Naye alijibu kuwa, ‘TRA system inatambua vizuri aina ya mzigo uliokusudiwa kwa kila ‘loading permission ref No.’
Jitihada za kumpata Waziri wa Fedha na Mipango ili atoe ufafanuzi wa kina wa maswali haya ambayo yameibua mkanganyiko mkubwa bado zinaendelea.