Tuesday, December 24, 2024
spot_img

“MECCO NI UHUJUMU NA UTAKATISHAJI”

RIPOTA PANORAMA

IMEELEZWA kuwa skandari ya kuporwa kwa ardhi na mali za umma na kutumika kuchukua mkopo wa mabilioni ya Shilingi katika benki mbili kubwa za hapa nchini ukiwemo mkopo usiokuwa na ukomo inaweza kuhusishwa na wizi, uhujumu na utakatishaji.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vya habari vya Tanzania PANORAMA Blog ambavyo vimekuwa vikifuatilia skandari hiyo kwa karibu, zimedai kuwa iwapo taasisi za uchunguzi zitachunguza sakata hili na kwa kutumia sehemu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huenda uhalifu mkubwa ikiwemo uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha vikabainika.

Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimeonyesha kuwa baada ya kuvuja kwa habari za kuporwa mali za Serikali na Kampuni ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) ambaye ni mwanahisa mkubwa katika uendeshaji wa Kampuni ya Mwananchi Engeenering and Contracting Company Limited (MECCO), taasisi za Serikali zilifanya uchunguzi na kubaini madudu. SISICOL anamilili hisa asilimia 75 dhidi ya 25 za Serikali katika MECCO.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ukaguzi maalumu ulibaini kuwa mwanahisa mkuu wa  MECCO alihamisha umiliki wa baadhi ya mali zake kwenda kwenye kampuni yake ya SISICOL kama sehemu ya malipo ya deni la mwanahisa huyo lililoingizwa kwenye vitabu mwaka 2008.

Kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa uendeshaji wa Kampuni ya MECCO baina Serikali ya mbia wake huyo, ndiye mwenye jukumu la kusimamia shughuli za kila siku lakini si kuhamisha mali.

Tanzania PANORAMA Blog imedokezwa na vyanzo vyake vya habari kuwa baada ya  kufanyika kwa ukaguzi, iliamriwa mali za MECCO ambazo zilikuwa tayari zimefanyiwa mabadiliko ya hatimiliki na kusomeka jina la MAS Holding and Container Depot Limited ambayo ni kampuni dada ya SISICOL zirejeshwe katika umiliki wa MECCO.

Imebainika kwamba utekelezaji wa uamuzi huo ulikwana baada ya kubainika kuwa hati za mali hizo zilikuwa tayari zimetumika kama dhamana ya mkopo katika moja ya benki kubwa hapa nchini na ili kuzinusuru, Msajili wa Hazina aliombwa afanye mawasiliano na uongozi wa benki hiyo ili hati hizi zibadilishwe kwa kurejeshwa kwenye umiliki wa MECCO wakati zikiendelea kuwa katika uhifadhi wa benki hiyo.

Inadaiwa Msajili wa Hazina alilifanya hilo na hatua za kubadilisha umiliki wa hati ya mali hizo zilianza hadi kufika hatua ya kufanya malipo ya Stamp Duty na Capital Gain ili kukamilisha taratibu za kubadilisha umiliki.

Kwamba MECCO ilifanya malipo ya Stamp Duty kisha ikaomba kupatiwa msamaha wa Capital Gain Tax ambapo Mamlaka ya Mapato (TRA), ilielekeza kuwasilishwa hesabu za kampuni ya MECCO na zile za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited ili iweze kufanya makadirio ya kodi.

Hata hivyo, taarifa zaidi zinadai kuwa MECCO ilishindwa kuwasilisha nyaraka za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited na hivyo kuifanya TRA kusisitiza kodi husika huku ikitoa maelekezo zaidi kuwa iwapo kuna haja ya kuomba msamaha bila kuwasilisha hesabu za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited, maombi hayo yaelekezwe kwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Imeelezwa kuwa MECCO iliwasilisha kwa Waziri wa Fedha na Mipango maombi ya msamaha wa kodi kwa barua yenye namba MECCO/HQ/0043/ACC ya Novemba 19, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango iliijibu maombi hayo ya MECCO Mei 25, 2022 kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba CAB.481/547/01 iliyoielekeza MECCO kuwasiliaha nyaraka ilizokuwa imeelekezwa na TRA ili iweze kubaini kiasi cha msamaha unaoombwa kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya msamaha huo.

Ikiwa ni takribani miezi sita sasa, taarifa zinadai kuwa MECCO haijawasilisha nyaraka hizo kwa TRA kwa kile ambacho imekuwa ikidai kuwa Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited haijafanya kazi kwa muda mrefu.

Wakati taarifa hiyo ukaguzi maalumu ikibainisha hayo na mapendekezo yake yakikwama kutekelezwa, taarifa nyingine zilizopatikana zinadai kuwa uendeshaji wa Kampuni ya MECCO umekuwa na dosari nyingi ambazo ndiyo chanzo cha kuporwa mali zake kwani haijaitisha kikao cha wanahisa kwa ajili ya utendaji wa kampuni kwa mwaka 2020 na 2021.

Inadaiwa kuwa licha ya kubainika kwa dosari hiyo na Ofisi ya Msajili wa Hazina kuandikia barua Juni 3, 2022 ikielekeza kutekeleza wajibu huo, MECCO haijatekeleza.

Mbali ya hilo, inadaiwa zaidi kuwa, Kampuni ya MECCO katika kile kinachoweza kutafasiliwa kuwa ni kiburi kilichopitiliza kwa mamlaka za Serikali, kampuni hiyo imekuwa haitoi ushirikiano kwa mjumbe wa bodi aliyeteuliwa na Serikali kuiwakilisha.

Taarifa zimeonyesha kuwa mjumbe huyo wa bodi, Mhandishi Allen Banda aliteuliwa Agosti 12, 2021 na kujulishwa kuhusu uteuzi wake kwa barua ya Agosti 13, 2021 akichukua nafasi ya Mhandishi Patrick Mfugale aliyefariki dunia lakini tangu ateuliwa ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja sasa hajawahi kuitwa kwenye kikao cha Bodi ya MECCO hivyo haijajulikana kwa uhakika kama bodi ya kampuni hiyo imekuwa ikiketi pasipo ushiriki wake kama mwakilishi wa Serikali yenye hisa asilimia 25 au lah.

Mpaka sasa, jitahidi za Tanzania PANORAMA Blog kupata kauli ya Msajili wa Hazina, Benedicto Mgonya kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuwa ndiye anayepaswa kulizunguzia sakata hilo akiwa na dhamana ya kusimamia mashirika ya umma hazijafanikiwa.

Mgonya jana alieleza kuwa maswali aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu skandari hiyo yatajibiwa na watu aliosema watapiga simu lakini hawakupiga na hii inatokea ikiwa ni zaidi ya miezi sita sasa tangu ofisi yake ilipoulizwa kuhusu hilo lakini haijapata kujibu chochote.

USIKOSE KUSOMA MWENDELEZO WA SAKATA HILI KESHO HAPA TANZANIA PANORAMA BLOG

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya