HIVYO NDIVYO NINAVYOMFAHAMU DIAMOND PLATINUMZ – 4
HAMEES SUBA
ILIPOISHIA
HATIMAYE Diamond alifika ofisini, sikutaka kumueleza yaliyonipata kwa sababu nilihisi nitamvunja moyo au kumkatisha tamaa na sikuwa na mambo mengi ya kuzungumza naye zaidi ya kumpa ujumbe mahususi niliokuwa nao.
āNimefikiria sana nimeona siwezi kukupambanisha na Mr Blue au msanii mwingine zaidi ya Ali Kiba, unachotakiwa wewe ni kuvumilia tu matusi hayaui na tambua kwamba wewe unatakiwa kufika alipofika Ali Kiba kwa hiyo tutakwenda hivyo hivyo, wacha waseme mwisho watakaa kimya.ā
Diamond aliinamisha kichwa chini kwa sekunde kadhaa kisha kusema; ānimekuelewa mkuu, fanya unavyoona inafaa.ā
SASA TUENDELEE
Niliielewa hofu yake ya kuogopa kunangwa na wasomaji wa magazeti hususani mashabiki wa Ali Kiba ilitokana na kutokuwa na uzoefu na vyombo vya habari kwa wakati ule, lakini baada ya kumuelewesha na kumsisitiza kwamba lazima apambane na mtu aliye juu ili naye aweze kuwa juu alinielewa vizuri na kujivika ujasiri.
Tulizungumza machache kisha nikamruhusu kuondoka ili kila mmoja aendelee na majukumu yake. Kwa upande wa Papaa Misifa na menejimenti yake nao waliendelea na mipango ya maandalizi ya video. Walikuwa wakiumiza kichwa kumpata ādirectorā mkali anayeweza ākushutiā video ya kwanza ya wimbo wa ānenda kamwambie.ā
Kazi hiyo iliangukia āvisual lab – next levelā kwa āprodyuzaā Adam Juma. āProdyuzaā huyo ndiye aliyekuwa āaki-hitā kwa ubora wa kazi za kurekodi picha za video kipindi hicho na hata bei yake ilikuwa ya juu tofauti na āmaprodyuzaā wengine waliokuwa tayari na majina makubwa katika āindustryā ya video za muziki.
Kulikuwa na ma ādirectorā wazoefu kama Karabani, Starford wa G/Video, Musa Tagalile, Chapakazi Productions na wengineo. Pia kulikuwa na makampuni ya āvideo productionsā kama vile ITV, Mwananchi Productions, Emptysoulz Productions, Bench Mark, Royal Productions, Chapakazi Productions n.k.
Hatimaye video ya nenda kamwambie ikatoka ikiwa imewashirikisha ndugu wawili wa Papaa Misifa, mmoja akiitwa Kesi na mwingine Boni ambaye hivi sasa ni marehemu pamoja na washiriki wengine. Ikasambazwa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni vya hapa nchini ikiwa imetanguliwa majuma kadhaa na āaudioā ya wimbo huo redioni.
MILANGO YAFUNGUKA
Baada ya kutoka kwa video ya ānenda kamwambieā niliitwa kwenye kikao kingine na viongozi wa Aljazeerah akiwemo Papaa Misifa na Denis Mgatha āMcDenisā ili kujadili mambo kadhaa ya kuongeza nguvu ya promo na msukumo kwenye televisheni ili ichezwe japo mara tatu kwa kila siku.
Jambo hilo lilikuwa ni muhimu sana kwa sababu mbeleni kulikuwa na tuzo za āKili Music Awardsā hivyo ilipitishwa azma kwamba zifanyike kila jitihada za kuhakikisha Diamond anaingia kwenye kinyangāanyiro cha tuzo hizo za mwaka 2010.
Ndani ya kikao hicho pia kulijadiliwa suala la muonekano wa Diamond katika video zijazo kwa sababau katika video ya ānenda kamwambieā ilionekana kuwepo kwa dosari kadhaa zilizopaswa kufanyiwa kazi kabla ya kushuti video nyingine.
Miongoni mwa dosari hizo ni suala la Diamond kuimba huku akiwa amekunja ndita kwenye paji la uso (rejea kwenye video hiyo unaaweza ukaona). Pia suala la kulamba lamba midomo kila wakati ilionekana kama mambo yasiyofaa sana katika video zijazo hivyo kamati iliamua kuyafanyia kazi kwa kumshauri Diamond kuachana na mambo hayo ili kuongeza mvuto wake kwenye video zijazo. Dosari hizo alielezwa Diamond nikiwa nasikia na alizielewa na kukubali kuzirekebisha.
Kutokana na kutokuwa na ushindani mkubwa kwenye televisheni zilizokuwa na vipindi vingi vya burudani kipindi hicho, video ya nenda kamwambie ilifanikiwa kupata āair timeā ya kutosha kuliko tulivyotarajia.
Televisheni kama C2C, DTV na Channel Ten zilifanya kazi nzuri sana kuipromoti video hiyo. Ilifikia kipindi C2C Televisheni wakawa wanaicheza zaidi ya mara tatu kwa siku.
Msimu wa tuzo ukafika, Diamond akatajwa kuwania kategori zaidi ya tatu. Mchakato ukaendelea hadi siku washindi walipotangazwa ambapo Diamond aliibuka na tuzo tatu. Tuzo ya kwanza ilikuwa tuzo ya msanii bora anayechipukia, tuzo ya pili ilikuwa wimbo bora wa R&B na tuzo ya tatu ilikuwa ya video bora. Tuzo hizo ndizo zilizofungua milango wa mafanikio ya Diamond.
Haraka haraka uongozi wa Aljazeera ulikutana na kujadili mafanikio ya tuzo hizo pamoja na suala la kukamilisha nyimbo nyingine kwa ajili ya albam. Ikumbukwe kuwa muziki wa zamani ulikuwa ukitegemea mauzo ya albam kuliko maonyesho jukwaani hivyo ili msanii atimize ndoto yake ni lazima ahakikishe ametoa nyimbo za kutosha kwa ajili ya kukamilisha albam.
Aljazeerah waliendelea kurekodi nyimbo na video zikiwemo āmbagalaā na ānitarejea.ā Katika wimbo ambao ulimtambulisha vizuri zaidi Diamond kuliko hata ānenda kamwambieā ni wimbo wa āmbagala.ā
Wimbo huu pia pamoja na wimbo wa ānitarejeaā zilirekodiwa Sharobaro Records kwa Bob Junior. Baadae Papaa Misifa aliniambia kwamba wao kama Aljazeerah walikubaliana kurekodi nyimbo sita lakini albam ilihitaji nyimbo zaidi ya hizo hivyo watalazimika kusaka baadhi ya nyimbo za zamani za Diamond na nyingine ambazo atarekodi nje ya lebo yao ili kukamilisha albam.
Kweli, walifanikiwa kupata nyimbo nyingine sita na kukamilisha albam yenye jumla ya nyimbo 12. Nyimbo nyingine ninazozikumbuka katika albam hiyo ambazo hazikurekodiwa kwa mfuko wa Aljazeraa ni pamoja na ājisachiā ambayo Diamond aliimba kwa kumshirikisha ndugu yake, Rommy Jonnes na Geezy Mabovu. Wimbo mwingine ni āI hate youā ambao Diamond aliimba kwa kumshirikisha Hemed PHD na wimbo wa ānalia na mengi.ā
Pia kuna wimbo ambao Diamond aliimba na Mr Blue (siukumbuki jina). Zilipokamilika nyimbo 12 ilitengenezwa albam na kuuzwa kwa mdau wa burudani na mmiliki wa FM Studio, Felician Mutta.
KIMBEMBE OFISINI
Wakati hayo yote yakiendelea mimi niliendelea kuongeza kasi ya promo katika magazeti yetu na hata kwa kutumia magazeti yaliyokuwa yakisimamiwa na rafiki zangu. Ilikuwa kila toleo la gazeti la Kiu ya Jibu lilitoka lazima kuwepo habari inayomuhusu Diamond katika ukurasa wa mbele au wa nyuma.
Jambo hili likaanza kunilitea shida ofisini kwani baadhi ya wafanyakazi wenzangu walianza kulalamika kuwa ninatumia madaraka yangu vibaya kwa kumuandika msanii mdogo na asiye na jina na kumuweka katika kurasa hizo ambazo wenyewe tulipenda kuziita kurasa za mauzo.
Ilinitokea siku moja baada ya kutumia sehemu ndogo tu ya juu katika ukurasa wa mbele wa gazeti (Ear Piece) kwa kuweka habari ya Diamond na picha yake na kuzua maneno mengi sana ofisini! Ukweli ni kwamba magazeti yetu yalikuwa yakiangalia uzito wa msanii ndipo aweze kukaa ukurasa wa mbele na si vinginevyo.
Hii ni hutokana na sababu za kibiashara kwani tabia za wasomaji au za kisoko ndizo hutoa mwongozo wa kipi kikae mbele ya gazeti au nyuma. Kuna wakati ilikuwa ukimuweka ukurasa wa mbele msanii ambaye hajakubalika kwa wasomaji, mabaki ya gazeti huwa ni mengi sana sokoni hivyo yanaporudi ofisini lawama huwa ni za mhariri.
Hata kama upepo wa kisoko siku siyo mzuri kutokana na mazingira mengine kama vile gazeti kukutana na mvua kubwa sokoni nk, lakini kwa sababu utakuwa umeweka stori ya mtu asiyekubalika kiofisi lawama zinaelekezwa kwa mhariri.
Siku hiyo upepo haukwenda vizuri sokoni hivyo basi lawama zilikuwa ni nyingi sana. Haijalishi ukubwa au udogo wa nafasi iliyotumika kwenye stori ya Diamond lakini kwa sababu soko halikwenda vizuri nilistahiki lawama na nililaumiwa katika kikao cha asubuhi ndani ya chumba cha habari.
Nilitoa hoja nyingi sana ikiwemo kuzingatia weledi wa kuwapromoti wasanii wachanga lakini haikusaidia, nilikumbushwa majukumu yangu ya kimkataba wa ajira kama mhariri kuzingatia asilimia za mabaki ya magazeti katika kila toleo ama sivyo nitalazimika kukatwa pasho zangu kama hali hiyo sitaizingatia.
Nilikubalina na yote lakini sikuwahi kuwaza kuacha kuendelea kumpromoti Diamond. Hivyo basi ili kukwepa lawama za ofisini na ili kuzinusuru posho zangu niliamua jambo moja, kuhakikisha kuwa katika kila habari ambayo Diamond ataonekana ukurasa wa mbele lazima niwe na habari kubwa ili yasitokee mabaki mengi ya magazeti sokoni kama ilivyotokea siku hiyo.
Namshukuru Mungu kwa hilo nilifanikiwa sana kiasi cha kuwatuliza wale wote waliokuwa wakinipiga vijembe kuhusu kumwandika Diamond.
Malalamiko yalipungua kidogo kidogo na ilifika wakati malalamiko yakatoweka kabisa. Diamond akaanza kuzoeleka kihabari. Ikaonekana si tatizo tena kuandikwa katika kurasa za mbele na nyuma kwani hata magazeti mengine ya Udaku ya nje ya kampuni yetu nayo yalishaanza kumtumia kihabari na hata kumuweka katika kurasa hizo.
USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA TANO YA SIMULIZI HII YA KWELI NA YENYE MAFUNZO MENGI