RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Mapato (TRA) imesema mazao ya chakula yanayosafirishwa kutoka nchini kwenda kuuzwa nje ya nchi hayatozwi kodi ya aina yoyote na mamlaka hiyo.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alipokuwa akijibu maswali aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni utata wa nyaraka za kikodi za Kampuni ya Nine Five Group Limited, ulioibuliwa na watu walio karibu na kampuni hiyo.
Taarifa zilizopatikana zimedai kuwa Kampuni ya Nine Five Group inayojihusisha na usafirishaji wa mazao ya chakula kutoka nchini kwenda nje ya nchi, imekuwa ikichezea nyaraka za usafirishaji mazao hayo kwa kushirikiana na kampuni moja ya uwakala wa usafirishaji mizigo.
“Tatizo kubwa lipo kwenye nyaraka za ku-clear mizigo kwa maana ya makontena yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi, hili likifanyiwa uchunguzi kwa mizigo yao yote waliyosafirisha tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo litabaibika.
“Kwanini nasema hivi, ni kwa sababu taratibu za usafirishaji mizigo nje ya nchi zina hatua muhimu za kufuata ili kukidhi vigezo. Hatua hizo ni pamoja na kufanya pre clearence documentation, custom declaration, consignment inspection, obtain TRA realese order na port clearance. Unapofanikisha mambo hayo ndipo unakuwa na uhalali wa kusafirisha mzigo wako ukiwa safi.
“Pia katika kila kipengele kuna taratibu zake, mfano kwenye TRA release order lazima ioneshe idadi ya mzigo kwa maana ya kontena zinazosafirishwa na namba zake, sasa baadhi ya release order za kampuni hiyo hazioneshi idadi ya kontena wala namba ya kontena wanazosafirisha jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
“Mbali na hayo, wakati release order haioneshi idadi na namba ya kontena zinazosafirishwa, kwenye loading permission inaonesha kampuni ilipakia kwenye meli kontena zaidi ya kumi kwa siku moja.
“Jiulize hata wewe kama release order ya TRA haitaji idadi wala namba ya kontena zinazosafirishwa, hizo kontena kumi zilizoainishwa kwenye loading permission zimetoka wapi?
“Halafu hapo hapo wakipewa release order ya TRA ambayo kwa kawaida msafirishaji hupewa akiwa amekwishakamilisha nyaraka zote muhimu na kwa mujibu wa taratibu msafirishaji hatakiwi kukaa na release order kwa muda mrefu, jamaa huwa wanakaa nayo hata wiki tatu na ujue kukaa na release order kwa kipindi kirefu ni kutengeneza dhana ya kuitumia tofauti na makusudio kwa maana kwamba unaweza kuitumia kusafirisha mizigo mingi kinyume na iliyoruhusiwa. Mpaka hapo wewe unapata picha gani?” kilidai chanzo cha habari.
Katika majibu yake Kayombo alisema mizigo ya transit hailipiwi kodi bali hupewa release order baada ya gharama za bandari na taasisi nyingine zinazoshughukilia mizigo husika kulipwa.
Alisema itambulike kuwa release order huambatana na nyaraka nyingine za mzigo husika ambazo hukaguliwa katika hatua mbalimbali na kwenye mifumo kabla mzigo haujatoka.
Kayombo alisema mazao ya chakula yanayosafirishwa kutoka hapa nchini kwenda nje ya nchi hayalipiwi kodi isipokuwa gharama za taasisi nyingine ambazo sio za TRA.
Tanzania PANORAMA Blog ilimuhoji zaidi Kayombo muda ambao msafirishaji anaruhusiwa kukaa na release order baada ya kupewa na TRA na iwapo inaruhusiwa kutumika kusafirisha mizigo zaidi ya iliyoombewa.
Pamoja na maswali mengine ilimuuliza pia iwapo release order inayotolewa na TRA huwa haitaji idadi ya kontena na namba zake, inakopelekwa ambako msafirishaji anapaswa kulipa kodi huwa wanajuaje kodi inayopaswa kulipwa kama nyaraka za TRA hazionyeshi mzigo uliosafirishwa.
Akijibu, Kayombo alisema siyo sahihi na haiwezekani kwa msafirishaji kutumia release order moja kusafirisha mzigo zaidi ya aliouombea lakini akakiri kuwa release order zinazotolewea na TRA huwa haziainishi mzigo zinaouruhusu kusafirishwa wala namba za kontena zinazosafirishwa.
Akiendelea kujibu, Kayombo alisema hakuna kodi ya forodha ambayo msafirishaji anapaswa kulipa anaposafirisha nafaka kwenda nje ya nchi wala hakuna kodi ya forodha wanayotozwa wasafirishaji wa mizigo ya transit.
Alisema idadi ya kontena zinazosafirishwa na namba zake huonekana kwenye loading declarations na kwamba hakuna sheria inayoelekeza release order za TRA kuainisha idadi ya mizigo inayosafirishwa na namba za kontena bali kutofanya hivyo ni utaratibu wa TRA.
Tanzania PANORAMA Blog ilifika katika ofisi za Kampuni ya Nine Five Group zilizopo eneo la Tazara ili kupata kauli ya kampuni hiyo lakini ilikutana na msaidizi wa mkurugenzi ambaye alikataa kutaja jina la bosi wake wala la kwake na kutaka aachiwe maswali kwa maandishi kwa ahadi kuwa atayafikisha kwa bosi wake ambaye atatoa majibu kwa njia ya simu, jambo ambalo hakulitekeleza.
PANORAMA Blog ilipofika tena katika ofisi hizo ilikuta mashine za kampuni hiyo zikihamishwa na ilipomuuliza mtu iliyemkuta awali aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wa mkurugenzi kuwa mashine hizo zinahamishiwa wapi, ilisema ameelekezwa na bosi wake kuifunga ofisi hiyo na mashine ziondolewe haraka zipelekwe nyumbani kwake na kwamba yeye haruhusiwi kuongea chochote.