HAMEES SUBA
Ilipoishia
BAADA ya kuimba nyimbo hizo nilibaini vitu vingi kwa Diamond, kwanza alikuwa na kipaji cha muziki na dhamira ya kweli ya kupambania ndoto yake, jambo la pili hakuwa mtu wa kukata tamaa na jambo la tatu alitanguliza nidhamu kuliko kitu chochote katika kuhakikisha anatimiza malengo yake. Haya mambo matatu nitakuja kuyafafanua zaidi mbeleni.
Basi, baada ya kufanya kile tulichotaka kukisikia kutoka kwake nilijikuta nikimwambia Papaa Misifa: āMchukue dogo anafaa sana.ā
Chipsi alipiga makofi akipongeza ushauri wangu kwa kuwa yeye alishamtanguliza kwenye mikono ya Papaa Misifa kabla yangu.
Twende sasaā¦
Baada ya wote watatu kukubaliana kwamba Diamond anafaa kudhaminiwa na Papaa Misifa ndipo Papaa Misifa akamruhusu Diamond kuondoka kwa maagizo kwamba arudi baadaye ili sisi tupate muda wa kujadiliana mambo mengine kibiashara kama vile ni namna gani ya kumsainisha mkataba na jinsi āpromotionsā zake zitakavyofanyika kupitia magazeti.
Ikumbukwe kwamba kipindi hicho hakuna promo ya msanii wa filamu, muziki au wa tasnia ya urembo iliyoweza ku-kick ipasavyo bila kutumia magazeti ya Udaku. Ni kipindi ambacho nguvu ya promo ya magazeti ya Udaku kwa wasanii wa tasnia hizo ilikuwa kubwa sana kuliko aina yoyote ya magazeti na hata radio.
Hakukuwa na Social Media kama ilivyo sasa japokuwa huduma ya Internet ilikuwa tayari inatumika nchini na mtandao wa Email uliokuwa maarufu sana ulikuwa ni Hotmail, baadae ikaja Yahoo ndipo ikaja G.mail. Pia hakukuwa na simu janja.
Tuliweka kikao kingine na kujadiliana namna ya ākumpromotiā Diamond ambapo miongozo yote niliitoa mimi ikiwemo kuunda skandari za kulazimisha na kumpambanisha Diamond na wasanii waliokuwa wakiwika wakati huo na namna ya kumfanyia promo zitakazomwezesha ku-kick kwa haraka.
Wakati huo mwanamuziki aliyekuwa akitingisha soko la Bongo Fleva alikuwa Ali Kiba, akisumbua na ngoma kali kama Cindirela, Mac Muga, Nakshi Nakshi na nyinginezo.
Wanamuziki wengine waliokuwa vizuri sokoni kwa kipindi hicho ni pamoja na Shaban Katwila au Q- Chief (sasa hivi Q- Chillah), Mr. Blue, Lady Jaydee, Matonya, TID, Dully Sykes, Marlaw, Profesa Jay na makundi kama TMK Familiy na TMK Wanaume.
Nikisema walikuwa vizuri sokoni sina maana kwamba wao ndio walikuwa āmaligendariā wa muziki wa kizazi kipya kwa wakati huo, hapana, maana yangu ni kwamba ndio walikuwa na ngoma zinazobamba mpaka kipindi hicho ambapo Diamond alikuwa āakifaitiā kuchomoka. Lakini āmalegendariā walikuwa wengi sana ila siwezi kuwazungumzia kwa sasa kwa sababu ni nje ya mada.
Lakini kwa staili aliyokuwa anakuja nayo Diamond ilionekana kikwazo kikubwa kwake ni Ali Kiba. Na ikumbukwe pia kwamba ni kipindi hiki ambapo soko la HipHop lilianza kushuka na kuanza kupanda kwa Bongo Fleva au kama walivyokuwa wakiitwa wanamuziki wa staili hii āWABANA PUAā. Uimbaji wa Q – Chillah, Matonya, Ali Kiba na ujio wa Diamond vilikuwa ishara ya kuididimiza HipHop na kuipaisha staili ya Bongo Fleva.
Tulijadiliana kwa takribani saa zima ndipo tukapata muafaka wa nini cha kufanya, baada ya hapo tukaagana na Papaa Misifa kisha mimi na Chipsi tukaondoka na kuelekea Sinza Kwa Remmy nilipokuwa nikiishi.
Kesho yake sikuweza kufika kwa Papaa Misifa kama tulivyokuwa tumekubalina kutokana na majukumu ya kazi. Papaa Misifa alinipigia simu na kunikumbusha ahadi yetu nilimwambia sitaweza kufika lakini nilimuahidi kufika kwake siku inayofuata.
Kweli siku iliyofuata nilifika kwa Papaa Misifa nikiwa nimeongozana na Chipsi kwa mara nyingine. Ilikuwa lazima nikutane na Chipsi kila siku kwa ajili ya kupanga ratiba za mashindano ya Miss Tourism na mambo mengine ya shindano hilo ndio maana nilikuwa nikiongozana naye.
Tulipofika tulimkuta Papaa Misifa, Diamond na Boni (hivi sasa Marehemu) wakisilikiza Demo ya wimbo wa Nenda Kamwambie. Kila mmoja aliukubali wimbo huo kwamba unafaa kuachiwa kama wimbo wa kufungua njia ya mafanikio ya Diamond.
Lakini baada ya kuusikiliza kwa zaidi ya mara tano iligunduliwa kuwa wimbo huo ulikuwa na dakika mbili na sekunde 58 tu, yaani ulikuwa haufiki dakika tatu. Tulipofananisha na nyimbo nyingine zilizokuwa zikifanya vizuri sokoni kwa kipindi hicho tuliona kwamba suala la ufupi wa wimbo huo linaweza kuutia dosari sokoni hivyo tukashauri ukaongezwe japo vionjo (vinanda) ili ufikishe dakika tatu japo na sekunde kadhaa.
Kwa wale wanaoufahamu wimbo huo, vile vinanda vinavyosikika mwanzoni havikuwemo awali ulipotoka studio kama Demo, viliongezwa kutokana na ushauri wa kamati iliyoupitia wimbo huo baada ya kurekodiwa Sharobaro Studio na Prodyuza Raheem Nanji a.k.a Bob Junior.
Ushauri huo ulikubalika na wimbo ukarudishwa studio kuongezwa vionjo pamoja na kufanyiwa mixing ndipo ukapewa baraka za kwenda kwenye vituo vya redio ili watu wakausikie.
Baada ya maridhiano ya kuachiwa kwa wimbo huo katika vituo vya redio tulifanya kikao cha mwisho kilichohusisha watu wawili tu mimi na Papaa Misifa.
Kikao hiki tulikifanyia chumbani kwa Papaa Misifa. Aliniita chumbani kwake na kuniuliza kwa mara ya mwisho kama akitumbukiza pesa yake itarudi au itapotea! Kwa maneno yake Papaa Misifa alisema:
āKaka Suba ebu niambie ukweli, nikiingiza pesa yangu kwa huyu dogo haitapotea?ā
Maneno haya Papaa Misifa aliyatamka kwa woga sana tofauti na siku zote ambapo alikuwa akizungumzia suala la pesa alitoa sauti ya kujitapa, alionesha kuwa na imani kubwa sana kwangu kuhusu suala la kumsainisha mkataba Diamond.
Ukumbuke huko nyuma alipenda kuniita kwa jina la tajiri lakini siku hii alibadili jina na kuniita kaka. Nilimuelewa alichokuwa akimaanisha kwani miezi kadhaa nyuma alikuwa amefanya shindano la Miss Tourism Kahama na kupata hasara kubwa iliyosababisha gari lake kubaki rehani. Hivyo hakutaka tena kupoteza kile alichokuwa amebaki nacho mfukoni.
Nakumbuka aliniambia kuwa, katika akiba yake alikuwa na pesa isiyozidi shilingi milioni sita tu na kama hiyo itapotea basi hana budi zaidi ya kurudi kijijini kwao Urambo, Tabora kwenda kulima Tumbaku.
Maneno yake yalinisikitisha hata mimi lakini niliingiwa na ujasiri na kumwambia āpesa itarudi tajiri, amini maneno yangu.ā
Sikujua imani hii niliitoa wapi lakini naweza kusema ni mipango ya Mungu iliyonisikuma kumpa imani hiyo Papaa Misifa.
Baada ya kumuhakikishia hilo, Papaa Misifa alisema, āSina neno la nyongeza kaka Suba, kila kitu nakuachia wewe, utajua utakachokifanya ili dogo (Diamond) āashainiā nchi nzima, nilirudia kumwambia asiwe na shaka.
Tulifunga kikao rasmi Papaa Misifa akaniambia baadaye atakuwa na kikao na memba wenzake wa kampuni ya Aljazeera kwa ajili ya kumsainisha Diamond kwenye lebo yao.
Kweli kikao hicho kilifanyika na Papaa Misifa alinieleza kuwa walikubalina na Bob Junior kulipia nyimbo sita kwa awamu ikiwemo nenda kamwambie.
Niliondoka nyumbani kwa Papaa Misifa majira ya saa tatu usiku kwa ahadi kwamba kesho yake mapema, Diamond afike ofisi za Gazeti la Kiu akiwa na picha zake kwa ajili ya kuanza promo za hatari.
Siku iliyofuata niliamka mapema kama kawaida yangu lakini kabla sijawasha gari kuondoka nikapigiwa simu na mtu wa ulinzi pale ofisini Jacob Washokera, akinijulisha kuwa, kuna kijana amefika ofisini ananiulizia. Nilimwambia anipe huyo kijana niongee naye ili kumtambua, alikuwa ni Diamond aliyefika ofisini kwa ajili ya kunipatia picha za promo.
Alikuwa amewahi sana kuliko tulivyokubaliana lakini nilifurahishwa na jambo hilo, nilianza kuona kweli alikuwa na nia ya dhati ya kupigania kutoka kimuziki. Nilizungumza naye kwa dakika chache sana kisha nikamwambia, ānisubiri nipo njiani nakuja.ā
Baada ya kama dakika arobaini hivi nikawa nimefika ofisini, nilimkuta akiwa ananisubiri kwenye benchi la kukaa wageni. Aliponiona tu akanyanyuka na kunifuata, alionekana mchangamfu kuliko siku nyingine tulizokutana, akanisalimia āshikamoo mkuu,ā nikaitikia salamu yake.
Akanifahamisha kuwa ameleta picha za promo. Nilizipokea na kuzitazama lakini hazikunivutia hata kidogo kwa sababu zilikuwa hazina ubora wa kutosha lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kuzipokea. Nilichukua maelezo machache kwa ajili ya kutengeneza habari kisha nikamruhusu Diamond aondoke.
Nilizichukua zile nikaziweka juu ya meza yangu kisha nikatoka kwenda kupata chai. Nilipita njia ya nyuma ya jengo la Ushirika na kutokea mtaa wa Kipata ambapo kulikuwa na migahawa miwili ya Riki Hotel na Keys Hotel tuliyokuwa tukiitumia kwa chai, chakula na vinywaji.
Niliingia mgahawa wa Riki nikastafutahi kisha nilirudi ofisini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yangu na nilikuwa nimepanga kuanza na Diamond. Lakini katika hali ya kushangaza nilipoifikia meza yangu sikuzikuta zile picha za Diamond.
Baadhi ya wafanyakazi walishawasili ofisini. Nilizitafuta zile picha kwa dakika kama tatu hivi bila mafanikio, nilitoka nje na kumuuliza mtu wa ulinzi kama amemuona mtu yeyote akiwa na picha hizo lakini alinijibu kwamba hakumuona mtu yeyote na hizo picha.
Nilihofia kuwauliza staff waliokuwa wamefika ofisini kwa sababu sikutaka mtu yeyote ajue kinachoendelea kati yangu na Diamond. Nilitoka nje na kwenda kusimama kwenye ngazi inayotokea nyuma ya jengo hilo nikitafakari juu ya upotevu wa ghafla wa picha hizo.
Pembeni ya ngazi kulikuwa na sehemu ya kutupia taka za maofisini (dust bin) Kwa hiyo mahali nilipokuwa nimesimama nikawa natazama zile taka, ghafla nikaona picha moja ikiwa katikati ya taka zile. Nikamuita yule mtu wa usalama na kumwambia mbona naiona picha kama ninayoitafuta kwenye lile dust bin?
Naye kwa mshangao akawa anatazama kule nilipokuwa napatazama mimi, nikamuona akipiga hatua za haraka kuelekea mahali pale ilipokuwa ile picha akainama na kuiokota kisha akasema, āDah ni zenyewe mkuu sijui nani kafanya hivi?
USIKOSE SEHEMU YA TATU YA SIMULIZI HII YA KWELI INAYOMUHUSU MWANAMUZIKI TAJIRI NA MWENYE MAFANIKIO MAKUBWA TANZANIA DIAMOND PLATNUMZ