MOSCOW, URUSI
URUSI imeishutumu Ukraine kwa kufanya shambulizi “kubwa” la ndege zisizo na rubani kwenye makao makuu ya Meli zake katika Bahari Nyeusi mji wa bandari wa Crimea wa Sevastopol.
Shambulizi hilo lilianza saa 04:20 kwa saa za huko na kuhusisha ndege tisa zisizo na rubani na saba za baharini, maafisa wa Urusi walisema.
Takriban meli moja ya kivita inasemekana kuharibiwa katika mashambulizi hayo.
Hata hivyo, kraine bado haijathibitisha tukio hilo.
Mikhail Razvozhaev, gavana wa mji huo aliyewekwa na Urusi, alisema jeshi la wanamaji la Urusi limezuia shambulizi hilo.
Mashambulizi hayo ndio yalikuwa “makubwa zaidi” katika jiji hilo tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wa Ukraine mnamo Februari, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilimnukuu gavana huyo akisema.
Alisema kuwa magari yote ya anga yasiyokuwa na rubani (UAV) yamedunguliwa na hakuna “miundombinu ya raia” iliyoharibiwa.
Meli moja imeharibiwa kidogo, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema.
BBC Swahili