Nasib Abdul (Diamond Platinumz) |
HAMEES SUBA
NASIB Abdul, a.k.a Diamond Platinumz ni kijana mwenye mafanikio makubwa sana hapa nchini kupitia muziki. Jina lake si tu ni maarufu Tanzania na Afrika Mashariki bali Afrika nzima na sehemu kadhaa duniani. Safari yake ya mafanikio ina mambo mengi magumu na mepesi, mazuri na mabaya, ya kusifiwa na ya kukosolewa, yaliyo wazi na yasiyo wazi lakini hivi ndivyo mimi ninavyomjua. ‘Tu-shee’ pamoja.
Novemba 2009
Majira ya saa tisa alasiri nikiwa ndani ya chumba cha habari (News Room) cha Gazeti la Kiu ya Jibu nikimalizia majukumu yangu simu yangu iliita lakini niliipuza kwa dakika kadhaa hadi ikakata, ilirudia kuita mara ya pili na ya tatu ndipo nikashawishika kuinyanyua na kutazama kioo chake ili kujua aliyekuwa akipiga simu hiyo ni nani.
Sikuipuuza kwa sababu ya dharau bali nilifanya hivyo nikijua kwamba nilikuwa na muda mfupi sana kumalizia kazi niliyokuwa nikiifanya ili niwe huru kuzungumza na mtu yeyote kwenye simu.
Nilipoinyanyua niliona jina la Chipsi likimweka kwenye kioo cha simu yangu na kumtambua mtu aliyekuwa akinipigia. Alikuwa ni rafiki na mtu wangu wa karibu sana ambaye asubuhi nilikuwa naye ofisini lakini baadaye tuliachana kwa sababu kila mmoja alikuwa na majukumu yake.
Jina kamili la Chips ni Gideon Chipungahelo, Chipsi ni ufupisho wa Chipungahelo. Alikuwa Rais wa Shindano la Urembo la Miss Tourism Beauty Peugeant (Miss Utalii). Licha ya kuwa nilishaweka msimamo wa kutopokea simu ya mtu yeyote mpaka nitakapomaliza kiporo changu cha kazi lakini kwa kutambua umuhimu wa Chipsi ilinilazimu kupokea simu hiyo na kumsikiliza.
“Dadi mambo vipi?” alinisalimia baada ya kupokea simu. “Poa tu Dadi, mambo yakoje?” nilimjibu kwa bashasha. Tulizoea kuitana Dadi siku zote na mpaka sasa tunapokutana ndivyo tunavyoitana.
“Mambo yako poa leo unatoka saa ngapi maana yule jamaa yetu wa Kahama anataka kuonana na sisi kuna ishu yake inahitaji msaada wako,” alisema Chipsi.
Nilishamfahamu mtu aliyekuwa akimzungumzia kwani siku chache zilizopita tulikuwa naye, alikuwa akimzungumzia mtu aliyefahamika kwa majina ya Msafiri Peter maarufu kwa jina la Papaa Misifa. Huyu ndiye aliyekuwa Promota wa awali wa Diamond Platinumz.
Kujuana kwetu na mtu huyu kulitokana na shindano la Miss Tourism, yeye alikuwa promota wa matamasha mbalimbali ya burudani. Mbali na kazi yangu ya uandishi wa habari, katika Management ya Miss Tourism nilikuwa mratibu (Coordinator) wa mashindano hayo na mkuu wa taarifa za Miss Tourism (Chief of Information). Kwa hiyo Papaa Misifa tulijuana naye wakati alipoomba leseni ya kuandaa shindano la Miss Tourism katika mji wa Kahama.
“Nina dakika chache tu Dadi ili niweze kutoka ofisini, wewe uko wapi kwani?” nilimuuliza. “Mimi niko hapa Keys Hotel nakusubiri ili twende tukamsikilize jamaa,” alisema Chipsi.
Keys Hotel ilikuwa jirani sana na ofisi yetu ambayo ilikuwa katika jengo la Ushirika lililopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam. Hoteli hii kwa takribani miaka saba ndiyo tuliyokuwa tukiitumia kwa chakula cha mchana na kupata vinywaji wakati wa jioni.
“Sawa, basi acha nimalizie hiki kimeo fastafasta halafu nakufuata twende tukamsikilize,” nilimjibu na kukata simu.
Baada ya kama dakika thelathini na tano hivi tulikutana na kuanza safari ya kwenda kwa Papaa Misifa, tulikuwa ndani ya gari aina ya Pajero ‘Short Chases’ yenye rangi nyeusi na mimi ndiye nilikuwa dereva. Tuliuacha Mtaa wa Lumumba na kuingia barabara ya Morogoro hadi Magomeni Mapipa ambapo tulichukua Barabara ya Kawawa hadi eneo la Morocco Hoteli (Magomeni Kanisani) na kukata kushoto kuingia Barabara ya Tandale.
Kwa mwendo wa takribani nusu saa tukawa tumefika nje ya nyumba aliyokuwa akiishi Papaa Misifa. Alikuwa akiishi kwenye nyumba ya ghorofa lakini si ghorofa kama zile za Oysterbay na Mikocheni bali ghorofa la Tandale.
Nasema hivi nikimaanisha kwamba kwa mtazamo tu halikuwa na ubora unaostahili, lilionekana kutokuwa na uhakiki wa bodi za usajili wa makandarasi na mainjinia za hapa nchini, yaani CRB na ERB lakini lilikuwa ni ghorofa. Hata hivyo, kutokana na uchakavu wa nyumba nyingi za maeneo hayo zililifanya ghorofa lile kuonekana lenye thamani kama yale ya Oysterbay na Masaki.
Tulishuka kwenye gari kisha Chipsi akampigia simu Papaa Misifa na kumtaarifu kwamba tuko nje chini ya ghorofa anapoishi. Sauti ya Papaa Misifa ilisikika kutokea ghorofani ikisema, “Ni huku wakubwa.”
Ilitulazimu kunyanyua nyuso zetu upande ule sauti ilipotoka na kumtazama. Akatuelekeza kwa ishara ya mkono upande zilipokuwa ngazi za kupandia juu alipokuwa nasi bila kupoteza muda tulielekea kwenye ngazi zile na kupiga hatua za haraka haraka kumfuata.
Hatimaye tukamfikia, akatukaribisha mpaka ndani sebuleni ambapo tuliwakuta vijana kama wanne hivi. Wa kwanza tulipishana naye mlangoni akitoka baada ya sisi kuruhusiwa kuingia ndani, wawili walikuwa wamesimama pembeni ya spika kubwa zilizokuwa zikiungurumisha muziki mnene sebuleni hapo.
Kijana wa nne alikuwa ameketi chini kwenye zulia mithili ya waumini wa kiislamu wanapokuwa msikitini, pembeni yake kulikuwa na redio kubwa iliyokuwa ikipiga muziki kwa sauti ya taratibu lakini mkito wake ulikuwa ni wa kutetema sana.
Kijana aliyekuwa kwenye zulia alionekana mtulivu sana na mwenye dalili za hofu kutokana na ugeni ulioingia. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kutusalimia akidhihirisha nidhamu yake, alisalimia kwa heshima kubwa na unyenyekevu wa hali ya juu huku akiwa ametazama chini akisuguasugua mguu mmoja kwenye lile zulia.
Upande wa kushoto alikuwepo mwanamke mmoja wa makamo amesimama kwa heshima pia.
Mimi nilikaa kwenye kochi lililokuwa likimtazama kijana huyo, Chipsi yeye alisimama kwa kitambo kwa kuwa alikuwa akiongea na mtu kwenye simu kabla ya kukaa. Baada ya Chipsi kumaliza kuongea na simu Papaa Misifa alianza kututambulisha.
“Jamani hawa ndiyo mabosi zangu niliokuwa nikiwasubiri,” Papaa Misifa aliwaambia wale watu waliokuwemo mle ndani.
Jina bosi halikutumika kwa maana ya kuwa sisi ndiyo tulimwajiri Papaa Misifa bali ilikuwa ni namna ya sisi kwa sisi kupeana heshima zetu tunapokutana.
Papa Misifa akanigeukia na kusema; “Tajiri hawa vijana wawili waliosimama pembeni upande wa kushoto ni wadogo zangu. Yule kule anaitwa Boni (sasa hivi ni marehemu), huyu hapa anaitwa Kesi.”
Kwa utambulisho zaidi ni kwamba vijana hawa ndiyo wale wanaoonekana kwenye video ya wimbo wa kwanza kumpatia mafanikio Diamond Platinumz uitwao Nenda Kamwambie.
Nilitingisha kichwa kama ishara ya kumwelewa utambulisho wake huo halafu nikasindikiza na neno hili; “Nafurahi kuwafahamu.”
Papaa Misifa akageuka upande wa pili na kuendelea kutoa utambulisho: “Huyu aliyekaa chini mbele yako anaitwa Nasibu lakini jina la kisanii anaitwa Diamond (wakati huo jina Platinumz halikuwepo). Ndiye aliyenifanya niwaite hapa leo, ni msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva), anahitaji msaada wangu kama Promota ili nimsimamie kazi zake kwa kuwa hana uwezo kifedha na yule mama mnayemuona amesimama pale ni mama yake mzazi.”
Chipsi alishamaliza kuongea na simu na papo hapo aliingilia maongezi kwa kuuliza: “Anataka kufadhiliwa anaweza kuimba au longolongo tupu” Chipsi ni mtu anayependa masikhara sana na kama hujamzoea unaweza kugombana naye sekunde chache sana unapokutana naye na kuanziasha mjadala fualani. Nilibaki kimya, sikutaka kutia neno kwa haraka, niliacha kwanza wenzangu wajadili ili nipate pa kuanzia.
“Mwambie aimbe tumsikilize,” Chipsi alisema. Papaa Misifa akamgeukia Diamond na kumwambia: “Umesikia wakubwa wanavyosema, achia mistari wakusikie ili wajue uwezo wako.”
Dogo (Diamond) akajitutumua na kujiweka sawa pale kwenye zulia, bila kukawiza akaachia mistari. Aliimbia wimbo wa kwanza, wa pili na wa tatu, nyimbo zote zikiwa kwenye mahadhi ya Bongo Fleva. Chipsi akamuuliza: “Una staili nyingine au ni hiyo hiyo Bongo Fleva?”
Diamond akasema; “Ninayo.” Papo hapo akaanza kuchana mistari kwa staili ya Hip-Hop. Chipsi akacheka sana na kutingisha kichwa kisha akasema; “dogo anajau au unasemaje dadi?”
Sikutia neno! Papaa Misifa akanigeukia na kusema; “Tajiri mbona upo kimya hujatoa maoni yako mpaka sasa wakati wewe ndiye tunayekutegemea.”
Nilimsogelea Papaa Misifa na kumnong’oneza jambo sikioni kisha tukatoka na kuwaacha wenzetu wote pale sebuleni. Tukiwa nje juu ghorofani nikamwambia maneno haya; “Nimekutoa hapa nje ili tuliweke sawa hili jambo, mwambie yule mama aondoke tumsikilize huyu dogo akiwa peke yake kuna vitu si vema kumchana dogo mbele ya mzazi wake halafu kumbuka kuwa kumfadhili mtu ni pesa inatumika kwa hiyo ni lazima tumsikilize kwa umakini na kumshauri kwa umakini bila ya kuwepo huruma ya mzazi, mama ana nafasi yake wakati mwingine si kwa leo, ushauri wangu ni huo.”
Papaa Misifa alikubaliana na ushauri wangu ndipo tukarejea ndani pale sebuleni tulipowaacha wenzetu. Nyumbani kwa Papaa Misifa hadi nyumbani kwa kina Diamond hapakuwa na umbali mkubwa kwa hiyo walikuwa ni kama majirani. Papaa Misifa alifanikiwa kumtoa mama Diamond (Sanura Kasim ‘Sandra’) pale ndani bila yeye kujua alitolewa kwa makusudi gani. Mama Diamond aliniaga kwa kunipungia mkono na mimi nikampungia kisha kikao chetu kikaendelea.
“Ukweli mimi bado sijaridhika na nyimbo ulizoimba sio kwamba ni mbaya ila kuna kitu bado sijakiona cha kunishawishi kuamini kama kweli wewe unafaa kufadhiliwa na Papaa Misifa, una nyimbo nyingine tofauti na ulizoimba?” nilimwambia Diamond naye bila kusita alisema “Ninazo.” Nikamwambia: “Twende kazi.”
Akaimba wimbo wa kwanza nadhani ulikuwa unaitwa Mama, kama haukuitwa hivyo basi ulikuwa na ujumbe uliomuhusu mama. Baada ya hapo akaimba nyimbo nyingine mbili (kwa sasa sizikumbiki).
Baada ya kuimba nyimbo hizo nilibaini vitu vingi kwa Diamond, kwanza alikuwa na kipaji cha muziki na dhamira ya kweli ya kupambania ndoto yake, jambo la pili hakuwa mtu wa kukata tamaa na jambo la tatu alitanguliza nidhamu kuliko kitu chochote katika kuhakikisha anatimiza malengo yake. Haya mambo matatu nitakuja kuyafafanua zaidi mbeleni.
Basi, baada ya kufanya kile tulichotaka kukisikia kutoka kwake nilijikuta nikimwambia Papaa Misifa: “Mchukue dogo anafaa sana.” Chipsi alipiga makofi akipongeza ushauri wangu kwa kuwa yeye alishamtanguliza kwenye mikono ya Papaa Misifa kabla yangu.
Papaa Misifa alitushukuru lakini alituomba kurudi tena kesho yake kwa ajili ya kusikiliza demo ya nenda kamwambie ambayo ilikuwa ikifanyiwa kazi kwa Bob Junior, Sharobaro Records. Tukakubalina kuja kuisikiliza kwa ajili ya kutoa ushauri mwingine kabla haijafanyiwa ‘mixing’ na kusambazwa kwenye vituo vya radio.
USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA PILI, Alhamis Oktoba 27.