RIPOTA PANORAMA
WATU watatu waliokuwa wakishikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jana walifikishwa kortin wakituhumiwa kufanya mkusanyiko usiokuwa halali.
Watuhumiwa hao ambao wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.
Walisomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita aliyedai mahakama hapo kuwa wanaunganishwa na wenzao 28 walioshtakiwa wiki iliyopita.
Wakili Mwita alidai mahakamani kuwa washtakiwa walifanya mkusanyiko usio halali maeneo ya Mkwajuni, Kinondoni mwezi uliopita. Kwamba walitenda kosa hilo, Februari 16, kinyume cha sheria wakiwa na nia ya kufanya uvunjifu wa amani na kusababisha taharuki, hata hivyo walikana shtaka hilo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika hivyo kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine na Hakimu Mwambapa alitoa masharti ya dhamana kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini dhamana ya maandishi ya Sh. milioni 1.5. Washtakiwa wote walipata dhamana. Kesi hiyo itatajwa Machi 8, mwaka huu.