Thursday, July 17, 2025
spot_img

USHUNGI WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NA UJUMBE MARIDHAWA

ABBAS MWALIMU

PICHA rasmi za Rais wa Sita wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (napenda nimwite Mama Tanzania, nitasema sababu baadaye) zimetoka, zimeanza kuwekwa katika ofisi mbalimbali.

Kitu kikubwa kilichoamsha maswali kwa watazamaji na wanunuzi wa picha hizo maridhawa ni rangi ya ushungi aliovaa Rais Samia.

Kama Mtanzania niliyebahatika kupata elimu ya diplomasia ningependa kutoa mtazamo wangu kuhusu rangi ya ushungi ambayo hata siku aliyoapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Machi 19, 2021 alivaa ushungi wa rangi hiyo.

Kidiplomasia, rangi nyekundu inamaanisha mamlaka na madaraka aliyo nayo kiongozi kwa mujibu wa Katiba ya nchi husika.

Tukitazama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake yote, inamtaja Rais wa Jamhuri katika ibara ya 33 ambayo inasomeka kama ifuatavyo:
33.-(1) Kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. (2) Rais atakuwa mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Hivyo ushungi wa Rais Samia katika picha, unabainisha kuwa anayeonekana kwenye picha ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Ujumbe huu kwenye ushungi wa Rais Samia unaenda sambamba na ujumbe alioutoa katika hotuba yake ya jumatatu Machi 22, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma wakati wa mazishi ya kitaifa ya Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli aliposema:

“Na wale ambao bado wana mashaka, naomba niwakumbushe kuwa huyu aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa jinsia ni Mwanamke.”

Katika Afrika na duniani kwa ujumla kumekuwa na nadharia potofu inayotokana na baadhi ya tamaduni zetu na mila potofu kuwa majukumu fulani ni kwa ajili ya wanaume tu, jambo linalotokana na mila na tamaduni zilizotengenezwa na sisi wenyewe wanajamii (Gender issue).

Hili lilijionesha hata kwa hotuba za baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi ya kitaifa ya Hayati Rais Dk. Magufuli ambao baadhi ya maneno yao, ukiyasikiliza kwa makini utaona yana ‘gender perspective’ ndiyo maana tulisikia maneno kama ‘tutakushika mkono’ n.k.

Kwa msingi huo, ushungi wa Rais Samia ni ujumbe mahsusi unaotoa tafsiri katika mawanda ya diplomasia ndani na nje ya Tanzania.

Kwa upande mwingine, rangi nyekundu kwa muktadha wa Afrika inamaanisha ardhi ambayo imepiganiwa na Waafrika kuhakikisha haiporwi na wakoloni, walowezi au mabeberu. Rangi hii pia huakisi uanamajumui wa Afrika ‘Pan Africanism’ na Tanzania ni sehemu ya uanamajumui huo.

Rangi nyekundu ipo katika ngao ya Taifa (coat of arms) chini ya Bendera ya Taifa la Tanzania ikiwa na shoka na jembe katikati huku ikiwa imepitiwa na mkuki.

Hivyo basi kwa namna ya pekee ushungi wa Rais Samia unatoa tafsiri kuwa yeye ni mwanamajumui wa Afrika na atapigania na kutetea maslahi ya Tanzania na Afrika ipasavyo kama walivyopigania maslahi ya Taifa hili watangulizi wake, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Amani Abeid Karume, Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Ujumbe huu pia unayaendea mataifa ambayo katika salamu zao za rambirambi yalionesha kuwa, kwa namna fulani yatapata upenyo wa kunufaika na Tanzania chini yake.

Hapa ndipo ninapopata sababu ya kusema kuwa Rais Samia ni Mama Tanzania, mkuu wa nchi, kiongozi, na Amiri Jeshi Mkuu ambaye anatoa ujumbe kwa namna ya kipekee kuwa atalinda na kutetea maslahi ya Tanzania kwa mujibu wa Katiba na kiapo alichoapa.

ABBAS MWALIMU NI MWANADIPLOMASIA NA MCHAMBUZI WA MASUALA YA KISIASA

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya