RIPOTA PANORAMA – 0711 46 49 84
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu (TFF), jana liligawa mamilioni ya Shilingi kwa wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali vya habari za michezo waliohudhuria mkutano uliotishwa na Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia.
Taarifa za kuwepo kwa mgawo huo wa fedha zimetolewa na baadhi ya wahariri waliohudhuria mkutano huo uliofanyika jana asubuhi katika Hoteli ya Sea Scape jijini Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa zaidi wa wahariri 30 walihudhuria mkutano huo na kila mhariri aligawiwa Sh. laki moja (100,000) na kwamba mgao huo uliwafikia pia wapiga picha waliokuwepo. Imedaiwa kuwa zaidi ya Sh. milioni nne ziligawiwa kwa wahariri na wapiga picha.
Taarifa zimeeleza kuwa fedha hizo ziligawiwa na afisa mmoja wa TFF wa kitengo cha uhasibu kwa utaratibu wa wahariri na wapiga picha kuorodhesha majina yao, lakini haikufahamika mara moja lengo la mgawo huo.
Haya yamebainika wakati Rais wa TFF, Karia akieleza shirikisho hilo liko katika mpango wa kubana matumizi na kupambana na ufisadi huku akifananisha mwenendo wa utendaji wake na ule wa Rais Dk. John Magufuli katika kupambana na matumizi yasiyo ya lazima na kupambana na ufisadi.
Katika mkutano wake wa jana, pamoja na mambo mengine, alisema ndani ya miezi saba, TFF imetumia Sh. bilioni 3,752,001,171.00 huku sehemu kubwa ya matumizi hayo ikielekezwa kwenye usimamizi wa ligi mbalimbali na kuandaa timu za Taifa ambako zimetumika Sh. bilioni 2,409,150,732 ambazo ni sawa na asilimia 64 ya matumizi yote.
Alisema asilimia 36 ya fedha zilizobaki ilitumika kulipia madeni ya TFF, mishahara ya wafanyakazi, kusaidia mikoa katika maeneo ya miundo mbinu, kuwajengea uwezo wafanyakazi na kuendesha mafunzo mbalimbali.
Aidha Rais Karia alieleza kuwa shirikisho limepunguza mishahara ya wafanyakazi kutoka Sh. milioni 85 mpaka Sh. milioni 50 baada ya kupunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 44 mpaka 21 waliobaki sasa huku kukiwa na wale wa kujitolea.
Haijafahamika kiasi hicho kilichogawiwa jana kwa wahariri kilitolewa katika fungu gani.