RIPOTA – 0711 46 49 84
MJADALA mpya umeibuka nchini baada ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura kuadhibiwa kutojihusisha na soka milele.
Wambura anatuhumiwa kughushi nyaraka na kuchukua fedha kinyume cha taratibu. Lakini Wambura amepaza sauti akisema kwanza waliomuadhibu hawana mamlaka hayo lakini pia hatua hiyo imefikiwa kwa sababu ya kukemea maovu ndani ya TFF?
Wambura amekaririwa kuwa, alihoji matumizi mabaya ya fedha za TFF.
Kwamba yeye (Wambura) akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya TFF alihoji matumizi mabaya ya shirikisho hilo linalodaiwa kutumia kiasi cha Sh. bilioni 3 kwa muda wa miezi saba kwa ajili ya maendeleo ya soka Tanzania.
Kwamba Wambura hakuridhishwa na matumizi hayo na pia alihoji mwenendo wa utoaji ajira ndani ya TFF baada ya kuwepo madai ya upendeleo katika utoaji ajira na zabuni.
Wambura ametoa madai hayo wakati huu ambapo kuna mijadala inayoendelea katika makundi mbalimbali ya kijamii kuhusu wafanyakazi wengi wa TFF kuajiriwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ‘kishakaji’ bila kufuata taratibu na kanuni za TFF. Inatajwa moja ya ajira hizo ni ya Kaimu Katibu wa TFF, Wilfred Kidao na Afisa Habari wa TFF, Criford Ndimbo.
Wambura anadai kuwa kumteua Wilfred Kidao kuwa Kaimu Katibu wa TFF ni kinyume cha taratibu na kwamba waliostahili ni mmoja kati ya maofisa wa TFF. Kwamba taratibu zinataka afisa aliye ndani ya TFF kukaimu na sio kuteua mtu yoyote ambaye hakuwa afisa wa TFF.