Thursday, July 17, 2025
spot_img

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali na haja ya kujitathmini

ABBAS MWALIMU – 0719258484

HABARI kubwa katika vyombo vya habari na mijadala inayoendelea kwenye jamii kwa sasa ni Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere aliyoitoa kwa waandishi wa habari, Alhamisi ya Aprili 8, 2021 jijini Dodoma.

Katika taarifa fupi ya ukaguzi aliyotoa kwa umma kupitia waandishi wa habari, CAG Kichere amebaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na yasiyozingatia bajeti katika wizara, taasisi, wakala na idara kadhaa za Serikali hali ambayo imezua mijadala na maswali mengi kutoka kwa wananchi.

Kwa mujibu wa CAG Kichere ni kwamba ofisi yake ilibaini matumizi yaliyo nje ya bajeti kwa taasisi na wakala kama vile TANROADS, TAWA, TARURA, TIA n.k, sambamba na Wizara za Maliasili na Utalii, Wizara ya Afya na Wizara ya Ujenzi.

Kwa mfano, CAG alisema alibaini matumizi ya Shilingi milioni 172 zilizoidhinishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii kupitia kwa kaimu katibu mkuu wake kwa ajili ya kufadhili tamasha la Kigwangalla Kili Chalenji 2019 kupitia Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) na pia kiasi cha Shilingi milioni 114 kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kiasi cha Shilingi milioni 57 kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), wakati shindano hilo halikuwepo kwenye bajeti za mwaka wa fedha za mamlaka hizo.

Mbali na matumizi hayo kwa mujibu wa CAG Kichere, alibaini pia Kituo cha Utangazaji wa Clouds kililipwa Shilingi milioni 629 na Shirika la Utangazaji (TBC) lilipwa Shilingi milioni 201 kwa ajili ya kuonesha matangazo ya tamasha la urithi huku Kampuni ya Wasafi ikilipwa Shilingi milioni 140 kwa ajili ya kutangaza utalii wa ndani katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Iringa na Dodoma.

Ni wazi kuwa ripoti hii ya CAG imeshtua watu wengi sana na kuzua maswali kadha wa kadha ambayo nadhani yanaweza kujibiwa kwa ufasaha na wahusika.

Binafsi ripoti hii ya CAG inanifanya nidhani kuwa kuna haja kwa Serikali kujenga mfumo imara wa kujitathmini kutokea ndani na kupanua uwajibikaji kwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 8 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba:

(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii; ambapo kifungu (b) kinaeleza kuwa ‘lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi.’

KWA NINI NADHANI HIVI?
Kwa sababu nafikiri kuna changamoto kwenye namna ya kujifanya tathmini kutoka kwenye mfumo uliopo sasa ambapo CAG badala ya kuwa na maamuzi yenye uwezo wa kuathiri moja kwa moja (Sanctioning/enforcing decisions) amekuwa akishauri zaidi jambo linalotoa mwanya kwa baadhi ya watanzania wasio waadilifu kuendelea kutumia ofisi za Serikali vibaya kutokana na kukosekana kwa uwazi kwenye matumizi ya fedha za umma kwa baadhi ya wizara, idara, wakala na taasisi za Serikali na hivyo kurudisha nyuma dhana ya utawala bora.

Tukumbuke kuwa utawala bora ni miongoni mwa viambata vya dira ya maendeleo ya Taifa 2025 na katika kutekeleza hilo Serikali iliunda mpango Taifa wa utawala bora (NFGG) mwaka 1999 ukiwa na lengo la kuleta maisha bora kwa kuangazia maeneo saba muhimu.

Licha ya mpango huo, Ofisi ya CAG ni miongoni mwa taasisi muhimu katika kuleta utawala bora na uwajibikaji nchini. Rejea Mdee na Thorley (2016), Tripp (2012) na Daima Associates (2009)

Tukumbuke pia kuwa Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 14 mwanachama wa ubia wa kuendesha Serikali kwa uwazi (OGP) tangu mwaka 2011 ilipojiunga na baadaye kujitoa mwaka 2015 ambapo Halmashauri ya Mji wa Kigoma tu ndiyo imebaki katika mpango huo wa OGP kama walivyoainisha Juma na Matuku (2019) katika andiko lao -‘Towards Inclusive Open Government in Africa.”

Wakati Tanzania ilipojiunga na OGP iliweza kuja na mpango kazi wa Taifa (National Action Plan) au NAP wa mwaka 2012 mpaka 2016 ambapo katika mpango kazi wa awamu ya kwanza (2012-2013) Serikali ilijidhatiti kuimarisha upatikanaji wa taarifa za utendaji kazi wa Serikali katika nyanja mbalimbali.

Kwa bahati mbaya ni malengo mawili tu kati ya malengo 25 ambayo Serikali ilijidhatiti nayo yalifikiwa.

Mpango kazi wa awamu ya pili (2014-2016) ulijielekeza kwenye sheria ya kupata taarifa (information act), bajeti kuwa wazi (open budget), data kuwa wazi (open data), uwazi katika ardhi na viwanda vya uchimbaji (extractive industry). Rejea Richard Mabala na Kefar Mbogela katika – ‘Evaluating and Shaping Engagement on OGP: A Case Story from Tanzania.’

Lakini kutokana na changamoto mbalimbali, mwaka 2015 Tanzania ilijitoa katika mkataba wa OGP na kubaki kwenye mpango wa hiyari wa Nchi za Umoja wa Afrika kujipima kwa vigezo vya utawala bora, yaani APRM, mpango ambao kwa mujibu wa Razzano na Gruzd (2015) katika andiko lao –‘A Next Generation Peer Review: What Does the Open Government Partnership have to offer’- wanasema una michakato mingi na migumu kutelezeka.

Hivyo basi, kwa mtazamo wangu nadhani hali hii ya Ofisi ya CAG kubakia kuwa mhimili pekee madhubuti wa kujipima kutokea ndani imesababisha kupungua kwa wigo wa mifumo ya kujifanyia tathmini hali inayosababisha CAG kubaini changamoto nyingi katika matumizi ya fedha za walipa kodi.

NINI KIFANYIKE?
Nafikiri sasa kuna haja ya kuipandisha hadhi Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa mamlaka kamili, yaani; Controller and Audit General Authority (CAGA).

Kwa nini nasema hivi? Kwa sababu kwa mtazamo wangu naamini ikiwa mamlaka kamili (Authority) itakuwa na uwezo wa kimaamuzi (ability to enforce sanctions) yatakayosababisha baadhi ya watu kuwajibishwa moja kwa moja kwa mujibu sheria itakayokuwa ikiongoza ‘mamlaka’ hiyo badala ya kuishia kushauri ‘mamlaka’ tu.

Kwa maoni yangu, CAG akikosa nguvu za moja kwa moja za kuathiri ama (sanctions) kisheria, nadhani bado changamoto zitazidi kuwa kubwa na hivyo msukumo unaweza kupungua zaidi katika utawala bora na uwajibikaji wa Serikali kwa maana ya kwamba baadhi ya watumishi wa umma wataendelea kutokuwa waadilifu kwa nchi na wananchi na hivyo kushindwa kuwaletea ustawi wananchi huku likiwa ndiyo lengo kuu la Serikali kwa mujibu wa Katiba.

Hili liligusiwa pia na Razanno na Gruzd (2015) walipoeleza kwa lugha ya Kingereza kwamba, “…the lack of tough sanctions may mean that the political reputational incentive is not significant enough to warrant change”

Tumeona mafanikio kadhaa kwa TAKUKURU tangu ilipokuwa taasisi inayojitegemea na hata Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa sana hivyo CAGA nayo itafanikiwa bila shaka.

Mbali na Ofisi ya CAG kuwa ‘mamlaka’ kamili nadhani pia kuna haja ya kutazama upya mfumo wetu wa kutathmini uwazi (transparency), uwajibikaji (accountability), kupambana na rushwa (jambo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza TAKUKURU), kuwawezesha wananchi kushiriki katika maamuzi sambamba na kuhanikiza utumiaji wa teknolojia kuimarisha utawala bora kama vile kuhakikisha miamala yote inafanyika kwa njia za kielekroniki kupitia simu ya kiganjani ili kuondoa mianya ya rushwa na ubadhilifu.?

Katika kufikia azma hizi nadhani kuna haja ya kuwa na mfumo wa kujitathmini wa Serikali ambao unaweza kuitwa –‘Tanzania Accountability and Participation Independent Review Mechanism au TAPIRM.’

Kwa maoni yangu nafikiri hii ‘mechanism’ ingekuwa sehemu ya CAGA katika kufanya tathmini ni kwa kiwango gani wananchi wa kawaida wanatambua wajibu wao kwa wale waliowachagua na walioteuliwa kwa lengo la kuwahudumia kwa sababu kwa mfano, tafiti zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawana imani na Serikali za mitaa (local governments) kutokana na kuhofia kutosikilizwa.

Hili liliainishwa katika utafiti uliofanywa na Anna Mdee na Lisa Thorley na kuchapishwa mwezi Oktoba, 2016 uliokuwa na kichwa cha utafiti, ‘Good governance, local government, accountability and service delivery in Tanzania: Exploring the context for creating a local governance performance index.’ ambapo katika utafiti wao wamebaini kama ifuatavyo:

‘Citizens are also less likely to engage with their LGAs as there is a perception their concerns will not be heard or taken seriously.’ (Mdee na Thorley, 2016:12).

Huenda hii ya kukosa imani ndiyo sababu wananchi hubeba mabango pindi waonapo ama kusikia ziara ya Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu katika eneo lao hali iliyopelekea Rais Samia kuwaonya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi ambao watabainika kuzuia haki hiyo ya wananchi.

Hivyo basi kwa mtazamo wangu naamini ipo haja ya kuwa na ‘mechanism’ yetu wenyewe ya kutathmini uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini yaani (TAPIRM) itakayokuwa ndani ya CAGA ili wananchi washiriki kufanya maamuzi na kupanua wigo wa utawala bora baada ya kuwa tumejitoa OGP.

Kimsingi ninaamini kuwa kuna haja ya sisi kama watanzania kujitathmini na kwa Serikali kuipandisha hadhi Ofisi ya CAG kuwa mamlaka inayojitegemea yaani CAGA itakayokuwa na uwezo wa kuathiri (enforcing decisions/sanctions) kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaohusika na matumizi mabaya ya fedha za umma na ambayo itakuwa na tawi la kupima uwajibikaji (TAPIRM) kwa kuwashirikisha wananchi ili tufikie azma ya dira ya Taifa 2025.

Kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Abbas Mwalim

Facebook|Instagram|Twitter.
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya