Wednesday, December 25, 2024
spot_img

NYUMA YA MLANGO WA BUNGE: – SIASA NI MAJUNGU, CHUKI NA FITINA

NA CHARLES MULLINDA

NILIPATA hamu ya kuonana na kuzungumza na Japhet Sagasii. Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria ambaye kabla ya kuteuliwa na Rais kushika wadhifa huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, baada ya kupata taarifa kuwa ni miongoni mwa watendaji wa Serikali aliyekumbana na adha za wanasiasa zilizomlazimisha kuondoka katika utumishi wa Bunge

Nilimpigia simu kumueleza nia yangu. Awali alisita kukutana nami lakini baada ya ushawishi mkubwa alikubali ombi langu na kunipa miadi. Nilipokutana naye sikupata tabu kubaini kuwa ni mmoja wa watendaji wazuri na makini wa Serikali lakini asiyependa kufikiwa na vyombo vya habari.

Nywele zake kadhaa nyeupe kichwani na mikunjo ya hapa na pale usoni mwake vilinidhihirishia utu uzima wake ndani ya utumishi wa umma na kunishawishi kuamini kuwa kwa mara nyingine nimekutana na mtu mwenye hekima na busara.

Baada tu ya kunikaribisha ofisini kwake na kusalimiana, kabla sijamuuliza swali lolote alitangulia kunipa maneno ya kunisifu kwa kufanikiwa kumshawishi hadi akakubali kukutana na mimi. Huku akijiweka sasa katika sofa alilokaa, akaniambia yuko tayari kujibu maswali yangu.

Nilianza kwa kumuuliza sababu zilizomuondoa katika utumishi wa Bunge naye bila kumung’unya maneno aliniambia ni fitna, majungu na kufanya kazi na wanasiasa wasiojiamini na wasiojua wanachokifanya.

“Sikupenda kuondoka katika utumishi wangu wa awali, niliondolewa na fitna, majungu na kufanya kazi na wanasiasa wasiojiamini na wasiojua wanachokifanya. Ukiingia ndani ya milango ya Bunge utaona wanasiasa waungwana, wenye haiba za kuvutia, lakini nyuma ya milango hiyo kuna wanasiasa wapika majungu, wenye chuki na mabingwa wa fitina.

“Nilikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge na kwa nafasi hiyo nilikuwa pia mmoja wa makatibu wa Bunge. Shughuli zangu zilikuwa pamoja na kuwapangia wabunge sehemu za kukaa.

“Safari ya kuja katika ofisi hii niliyopo sasa ilianza siku niliyoletewa ‘kimemo’ cha Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi kilichokuwa kimeelekezwa kwa Dk. Thomas Kashillilah ambaye wakati huo alikuwa akikaimu wadhifa wa Katibu wa Bunge.

“Chenge alikuwa ameondolewa kwenye uwaziri hivyo alilazimika kuhama alipokuwa akikaa, katika ‘kinoti’ hicho alikuwa akiomba atafutiwe sehemu ya kukaa na aliomba iwe upande wa kulia wa Spika.

“Ilikuwa mwishoni mwa kikao cha Bunge la mwezi wa nne, hivyo Dk. Kashillilah alinielekeza kufanya kazi hiyo ili katika Bunge la Bajeti la mwezi wa sita, Chenge awe na sehemu nyingine ya kukaa. Sikumbuki ilikuwa tarehe ngapi ila nakumbuka ilikuwa Jumatatu, siku ya ‘Briefing,’ kikao cha Bunge ilikuwa kianze saa nne asubuhi.

“Kabla ya kuanza kwa kikao nilimchukua Chenge kwenda kumuonyesha nafasi yake kwa sababu tulishaitafuta. Nilimkuta akiwa na ama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru au Ali Ameir Mohamed, nikamuomba tuongozane kwenda ndani ya Ukumbi wa Bunge.

“Njiani, tulikutana na Basil Mramba na Anne Abdalah ambaye alimtania kuwa amefufuka, yeye alimjibu kwa mkato ‘acha tu mama yangu.’ Nikiwa na mtumishi mwenzangu wa Bunge, Mariam tulimwonyesha sehemu yake iliyokuwa karibu na kiti cha Rose Kiligini na Abdalah Mtutula, akasema hapo hapamfai.

“Tukampeleka alipokuwa akikaa James Wanyancha kabla hajateuliwa kuwa Naibu Waziri, kiti hicho kilikuwa karibu na korido na jirani na Stephen Galinoma na Naibu Spika, Anne Makinda, alikikagua kwa kukizungusha akakikubali. Akaomba chuma cha jina lake kiwekwe hapo, tukakubaliana. Ilikuwa majira ya saa 3.30 asubuhi, tukatoka nje ya ukumbi na kuachana salama.

“Baadaye kikao cha Bunge cha siku hiyo kiliendelea vizuri, lakini wakati wa mapumziko ya mchana tetesi za kuwekwa ungaunga wenye uchawi bungeni zikaanza kusambaa na mimi zikanifikia jioni nikiwa baa ya polisi jamii, huku nikitajwa kuhusika. Yalikuwa mambo ya ajabu na huo ndiyo ukawa mwanzo wa safari yangu kuondoka katika utumishi wa taasisi hiyo.”

Baada ya maelezo hayo alinyamaza na kuniangalia usoni, nikamhoji kisa kizima kilikuwaje.

Alieleza kuwa siku hiyo saa tisa alasiri alipanga kwenda kijijini kwake Mvumi lakini uvivu ulimkamata akaahirisha safari hiyo, akabaki akichapa kazi ofisini.

Alisema Saa 12 jioni alikwenda baa ya polisi jamii kula nyama na bia kadhaa ndipo alipofuatwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Dodoma na kumhusisha na tuhuma hizo za kishirikina bungeni. Kwa maneno yake mwenyewe alieleza;

“Baada ya kutoka ofisini majira ya saa 12.00 hivi jioni, nilikwenda baa ya polisi jamii kula nyama na bia kadhaa. Nikiwa hapo nilipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Dodoma akiomba kuniona, nilimruhusu na kumuelekeza nilipokuwa.

“Aliungana na mimi muda mfupi tu baada ya kuwasiliana na kunieleza kuna uvumi bungeni wa kufanyika vitendo vya kishirikina na mimi nimehusishwa. Kwamba usiku wa manane, kamera za ndani ya Ukumbi wa Bunge zimetunasa mimi na Chenge tukimwaga ungaunga wa kichawi kwenye viti vitatu.

“Nilishangaa, nikakataa, nikamweleza ukweli wangu kuwa kweli mimi, Mariam na Chenge tuliingia bungeni lakini ilikuwa saa tatu asubuhi si usiku wa manane, tena chini ya maelekezo ya maandishi ya Kaimu Katibu wa Bunge.

“Mpelelezi yule alinihoji kama nilipita kwenye kiti cha Spika wa Bunge, Samuel Sitta nikakataa, akataka kujua kama nilifika kwenye kiti cha Naibu Spika, Makinda nikakubali. Kwa Dk. Harrison Mwakyembe nikasema no.

“Kisha akataka kujua nahusika vipi na kuugua kwa Dk. Mwakyembe, hapo nikamshangaa zaidi kwa sababu jambo hilo niliona ni upuuzi. Hili nitalieleza baadaye, tuendelee na hili.

“Baada ya kuridhika na majibu yangu alinieleza kuwa Spika alimtuma msaidizi wake kwenda kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kutoa taarifa za watu kunaswa na kamera zilizo ndani ya Ukumbi wa Bunge wakifanya vitendo vya kishirikina ukumbini humo usiku wa manane na kumtaka afanye uchunguzi.

“Alinieleza kuwa ingawa hawaamini uchawi walilazimika kuendesha uchunguzi huo kutokana na madai na maombi ya Spika hivyo yeye aliagizwa kuanza kutuchunguza wote tuliotajwa.

“Niliitwa kituo cha polisi siku ya Ijumaa nikatoa maelezo ya mdomo na Jumatatu niliandika maelezo yangu kwa maandishi. Walifanya uchunguzi wao ikabainika tuhuma hizo si za kweli lakini tukabaki kusubiri tamko la Spika kama alivyokuwa ameahidi kuhusu jambo hilo.

“Kwa sababu nilikuwepo katika Ofisi za Bunge, nilijua kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Spika aliitisha Kamati ya Huduma za Bunge na Kamati ya Uongozi ili wamshauri kuhusu jambo hilo. Inawezekana alifanya hivyo kwa sababu alikuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida kwa sababu kikanuni huwezi kuita kamati hizo mbili kukushauri kwa wakati mmoja.

“Kwa wadhifa wangu nilihudhuria kikao kile, ajabu alipoingia tu na kuniona alisema hataki kuniona katika kikao chake, akanifukuza. Wabunge wanamuogopa Spika, hakuna aliyehoji kwa nini nafukuzwa wakati mimi ndiye ninayepaswa kutunza kumbukumbu za vikao vya Bunge. Nilidokezwa baadaye kuwa walijadili namna nzuri ya kuliwasilisha jambo hilo bungeni ili lisilete maswali zaidi kutokana na kauli ya mwanzo ya Spika.

“Jukumu la kuandaa tamko la kusafisha hali ya hewa bungeni kutokana na kauli mbaya zilizotolewa awali zikutuhumu watu kwa uchawi walipewa Dk. Willbroad Slaa, George Simbachawene na Wilson Masilingi na jukumu la kulisoma akapewa Naibu Spika, Makinda ili Spika awe pembeni na jambo hilo kwani lingeweza kumgeukia.

“Makinda akafanya kazi ya kulitaarifu Bunge kuwa mjadala wa ushirikina bungeni umefikia tamati bila kujua kuwa anatoa tamko batili kwa sababu huwezi kusema mwisho wa mjadala wakati haujajadiliwa bungeni, hoja haijatolewa na haijaungwa mkono.

“Kuanzia hapo mimi na Spika tukawa paka na chui, hakutaka kuniona kwa karibu hata nilipokuwa nikimsogelea kwa makusudi. Baadaye niliondoka bungeni na namshukuru Rais alinileta hapa nilipo sasa.”

Baada ya maelezo haya nilimuuliza kuhusu sakata la kuugua kwa Dk. Mwakyembe na kuhusishwa na ushirikiana naye alikuwa na haya ya kunieleza:

“Spika kwa kipindi nilichokaa naye niligundua kuwa ni mtu mwenye kutoa kauli pasipo kuzifanyia kazi sawasawa. Kwa kiongozi wa ngazi yake, kabla ya kutamka jambo zito kama hilo, tena bungeni alipaswa kuwa anajiridhisha kwanza na anachokizungumza.

“Dk. Mwakyembe hakuugua, suala hilo halipo na ninaweza kueleza mahali popote hivyo. Kama ni kumuwekea uchawi kama tulivyotuhumiwa sijui tuliwekaje manake wiki hiyo ya kusomwa hotuba ya bajeti siku zote alikuwepo.

“Ila napenda jamii ielewe wazi kuwa Dk. Mwakyembe hakuugua kama ilivyotangazwa bungeni wala hakukuwa na ushirikina. Nasema hivi kwa uhakika kabisa kwa sababu mimi ndiye niliyetuhumiwa na nilikutana naye mlangoni wakati akitoka nje ya Ukumbi wa Bunge.

“Ilikuwa hivi; siku ya Alhamisi baada ya Waziri wa Fedha wa wakati huo, Zakia Meghji kusoma hotuba yake, Dk. Mwakyembe alishatoka nje ya Ukumbi wa Bunge, mimi nilikutana naye mlangoni nikamuuliza kulikoni? Akasema hajisikii vizuri lakini haumwi bali ni kwa sababu ya uchovu wa pombe.

“Yeye mwenyewe alinieleza kuwa siku ya Alhamisi alikunywa pombe nyingi na kwa muda mrefu hadi karibu na alfajiri. Asubuhi ya Alhamisi pamoja na uchovu wa pombe alikuja bungeni kwa sababu alikuwa na hamu ya kusikia hotuba ya bajeti. Akiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge akajisikia vibaya na kwa sababu alikuwa anayumba akamuomba Mbunge Mwambalaswa amshike mkono ili amsaidie kutoka nje asije akaanguka.

“Alikwenda Zahanati ya Bunge ambako alichunguzwa na kweli akagundulika ni uchovu na kutokula. Hapo walimpa ‘Glucose’ wakamlaza na kumzungushia pazia la kijani ili apumzike. Waliokwenda kumuona walimkuta katika hali hiyo lakini alikuwa anawaambia kabisa kuwa haumwi bali uchovu. Ajabu bungeni ikatangazwa hivyo na bwana mkubwa. Ni mambo ambayo sitayasahau katika maisha yangu kwa sababu yaliniumiza sana.”

Nilimuuliza pia tathimini yake kuhusu mwenendo wa Bunge la tisa kwa muda aliolitumikia, akasema uongozi wa Bunge lililopita umelipeleka Taifa pabaya.

“Bunge limekuwa sehemu ya watu kushughulikiana kwa sababu ya tofauti zao za ajabu ajabu tu, Bunge limekuwa sehemu ya watu wenye nguvu ndani ya taasisi hiyo kuwaumiza wengine, Bunge limegeuka kuwa sehemu ya wanasiasa kujitafutia umaarufu, Bunge limegeuka kuwa sehemu ya baadhi ya wanasiasa kuwachafua wenzao. Kwa mtazamo wangu mimi Bunge hili lililopita halikuwa na kiongozi makini na ndiyo maana liliiyumbisha nchi.

“Mimi si mnafiki nasema kutoka moyoni kile ninachokiamini. Bunge linaipeleka nchi pabaya na mimi nilipokuwa bungeni nilikuwa namkosoa waziwazi Spika kila alipokuwa akichukua maamuzi ambayo yangeweza kuyumbisha Bunge au Taifa.

“Nilimpinga alipotaka kubadilisha ‘order paper,’ alikasirika kweli, lakini nilifanya hivyo kumsaidia yeye. Nilikuwa na Damian Foka akapiga simu akitaka tubadili ‘order paper.’ Badala ya kuanza na kipindi cha maswali na majibu tuanze na kanuni za Bunge, nikasema hapana. Foka akampigia kumueleza kuwa si utaatibu, akafoka akasema yeye ndiyo Spika tufuate anachosema.

“Nikapuuza tu, sikubadili ‘order paper’ hiyo lakini nikamwambia Foka tukutane mapema asubuhi ili tujue tunafanya nini. Asubuhi tukakubaliana na Foka kuwa ili tusiingie kwenye malumbano na Spika, tuandae ‘supplementary paper.’ Spika alipofika na kukuta ‘order paper’ iko vile vile akafura kwa hasira, akaapa kuwa atanifuta kazi.

“Wakati naingia ukumbini nilikutana na Naibu Spika Makinda, akaniambia ninaitwa na Spika, aliponiona tu akaanza kufoka, mimi nikawa namtizama tu baadaye akanyamaza. Akaniuliza kwa nini nimenyamaza sikumjibu lolote, nikamwambia namsubiri amalize kufoka. Akatulia, nikampa ‘supplementary paper’ ikiwa inasomeka shughuli zitaanza kwa kuwasilisha hati mezani, akatulia.

“Nikatumia nafasi hiyo kumuonya kuwa anatakiwa kuwa makini sana na maamuzi yake kwa sababu yeye ndiyo mtu wa kwanza katika Bunge anayetakiwa kulinda Kanuni za Bunge, vinginevyo Bunge litamshinda, ataliharibu.”

Ingawa Sagasii alionekana kuchoka kutoa maelezo niliona niumie wasaa zaidi kidogo kujua zaidi mambo yanayomfanya awe na mtazamo huo kuhusu Bunge. Nilimuuliza jambo jingine linalomfanya aamini kuwa Bunge la tisa halikuwa na kiongozi makini na liliiyumbisha nchi. Naye bila kusita aliendelea kunieleza:

“Huwezi kuwa na Bunge la aina hii, kama hili lililopita katika nchi yenye watu maskini kama hii licha ya utajiri ilionao kisha ukasema una Bunge makini na lenye meno. Huwezi kuwa na Bunge la matajiri linalotetea maslahi ya watu maskini, sijui kama ninaeleweka?” haraka niliitikia kuwa ninamuelewa, akaendelea:

“Ubunge sasa ni biashara si uwakilishi, ubunge ni sawa na utukufu ambao matajiri wanaukimbilia. Nimesema mwanzo ndani ya milango ya Bunge kuna wanasiasa waungwana kwa kuwatizama sura zao lakini wakiwa nyuma ya milango ya Bunge ni wanasiasa wa ajabu kabisa.

“Bunge hili liliitikisa Serikali hadi Baraza la Mawaziri likavunjwa kwa sababu tu ya manufaa ya wanasiasa fulani. Watu walichafuka sana wakati wa Bunge hili lakini mimi ninakwambia si wachafu kiasi hicho, ni majungu, fitna na chuki tu. Bunge hili limetumia kiasi kikubwa mno cha fedha ambazo hazilingani na kazi lilizofanya. Sitaki bwana, nisije nikaanzisha malumbano na watu.

“Lakini lilifika hapo kwa sababu ya kukosa uongozi makini. Na hili nalisema sana kwa sababu nililipigania sana nikiwa mmoja wa watendaji pale. Nimemsaidia sana Spika kuruka vihunzi vinginevyo watu wa aina ya Dk. Slaa wangeshamshughulikia au kumuumbua.

“Kuna wakati alimtaka Katibu wa Bunge ampeleke Dk. Slaa kwa DCI baada ya kuiondoa hoja yake moja alipoona imekaliwa. Spika akakasirika ile mbaya ndiyo akatoa hilo agizo. Nimekuwa bungeni muda mrefu kuna wabunge ambao hupaswa kucheza nao kitoto kwa sababu ukikosea tu wanakuvua nguo. Dk. Slaa ana jeshi nyuma yule
hata anapowasilisha hoja zake hakurupuki, ana jeshi la wanasheria nyuma yake. Sisi tuliokaa bungeni muda mrefu tunamjua.

“Spika bila kujua anataka kuanzisha mapambano na mtu wa aina gani na madhara yake ni nini, pasipo hata kutaka ushauri kutoka kwa watendaji wake akatoa agizo hilo. Mimi nikaiona hatari ile nikamwambia Katibu wa Bunge tunatumia mamlaka yapi kumpeleka Dk. Slaa kwa DCI? Ikichunguzwa ikaonekana hoja za Dk. Slaa ni za kweli Spika yuko tayari kusimama mahakamani? Na hata ikionekana hoja hizo za Dk. Slaa ni sahihi halafu na yeye akajua akadai fidia, Spika yuko tayari kulipa fidia hiyo?

“Kwa sababu hapo hakukuwa na uhusiano kati ya Katibu wa Bunge na DCI hivyo nilikuwa nahoji mamlaka yetu. Pale tusingesimama kidete Dk. Slaa alikuwa anammaliza Spika kirahisi kabisa. Na tatizo ni kutokujua kwake kama Spika anapaswa kufanya nini.

“Siku nyingine akaja anaeleza kuwa wabunge Michael Lazier na Molel anawasimamisha ubunge kwa sababu ya tuhuma zilizokuwa zinawakabili, nikamwambia hapana mzee, wewe Spika huna mamlaka hayo. Wakati wote nilikuwa nahakikisha namshauri vizuri, sikumwacha aingie kwenye mtego wowote na nilikuwa wazi kabisa kwake, sasa sijui alikuwa anachukuliaje ushauri huo, nadhani alikuwa na mawazo kuwa namdharau.

“Sasa nikumalizie na hili. Siku ile Rais anatoa hotuba kisha Spika akasimama na kumwambia anapaswa kuwa mkali kidogo alikosea mno. Nisiseme sana ila kikawaida anayetakiwa kutoa neno la shukrani baada ya Rais kuzungumza ni Waziri Mkuu si Spika. Tafuta mabingwa wa mambo ya kibunge watakwambia hili. Mimi nimemaliza.”

Nilisimama kumshukuru kwa kutoa muda wake kuzungumza nami na kuagana naye nikimtakia mafanikio katika shughuli zake. Kisha nikaondoka ofisini kwake huku nikiwa na msongo mkubwa wa mawazo kuhusu Bunge na wabunge wetu.

MAHOJIANO HAYA YALICHAPISHWA KATIKA JARIDA LA UMOJA – OKTOBA 2010

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya