RIPOTA MAALUMU
IMEELEZWA kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amekubali kumpokea na kumrejeshea uanachama wa chama hicho, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hayo yameelezwa na mmoja wa watu waliopata kuwa karibu na Zitto, David Kafulila katika andiko lake ambalo limesambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika andiko lake hilo, Kafulila ameeleza kuwa Mbowe na Zitto walikutana jijini Nairobi nchini Kenya ambako walifanya mazungumzo ya kina ambapo Mbowe alimpa Zitto masharti ya kurejea Chadema ambayo aliyakubali kabla ya kufikia makubaliano ya kumaliza tofauti zao.
Mbowe aliingia kwenye mgogoro na Zitto alipotangaza nia ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema na mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho kabla ya wazee wa Chadema kuingilia kati na Zitto akatimuliwa.
Kafulila ameandika akimtaja Zitto kuwa mwanasiasa machachari asiyetabirika, asiyeaminika na asiyepaswa kutegemewa ambaye ameamua kujiunga na siasa za kianaharakati kama zile zinazofanywa na Chadema baada ya kutotimia kwa matarajio aliyokuwa nayo ya kuwa mmoja wa wanasiasa wa upinzani kuteuliwa kuwa kiongozi mwandamizi wa Serikali.
Kwamba katika mazungumzo ya wawili hao huko Nairobi wengine waliokuwepo ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.
“Najua kwamba hitaji lake yeye ilikuwa ninyi mkubali aingize ACT kwenye UKAWA lakini Mbowe ukakataa kwa sababu zinazojulikana ambazo hazitofautiani na zilizomfanya akamkatalie Lowassa kuileta ACT katika ushirika wa UKAWA mwaka 2015.
“Ulijenga hoja kwamba ACT inakufa kwa kuondoka akina Kitila Mkumbo hivyo ni bora yeye Zitto arejee Chadema peke yake na iwapo ana wafuasi wake, watamfuata.
“Hakuwa na jinsi, ilibidi akubaliane na hilo. Najua mlikubaliana kimsingi kwenye hilo ila bado mkajipa muda wa kuonana tena na kukamilisha mazungumzo ikiwa ni pamoja na ratiba ya utekelezaji wa hilo,” linasomeka andiko la Kafulila.
Anaandika zaidi kuwa Mbowe anafurahia kurejea kwa Zitto kwa sababu amemzidi katika siasa za kiuanaharakati. Kwamba hivi sasa Zitto amekuwa akitoa maneno makali dhidi ya Serikali ambayo yeye (Mbowe) anaogopa kuyasema dhidi ya Serikali na Rais wa nchi.
“Nilicheka sana kumwona kwenye mitandao akiwahamasisha wabunge na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wasaini ‘petition’ ambayo sijui alikuwa anaiandaa yeye ili kukulazimisha wewe na viongozi wenzako wa juu wa Chadema muitishe kikao cha kamati kuu na kufanya uamuzi mzito (ambayo pia angewaambia yeye uamuzi gani mfanye) na akaahidi eti yeye na chama chake kitawaunga mkono.
“Hii haijapata kutokea. Kiongozi wa juu kabisa wa chama A anahamasisha viongozi wa chama B waasi dhidi ya uongozi wao na kulazimisha kikao ili wafanye kikao na kufanya maamuzi yanayopendekezwa na kiongozi huyo kwa ahadi kwamba atawaunga mkono.
“Si aitishe kamati kuu yake afanye hayo maamuzi magumu halafu aombe chama chenu kimuunge mkono? Ajabu hata kukusindikiza tu polisi hajaenda,” inasomeza sehemu nyingine ya andishi la Kafulila.
Anaandika Zaidi; “Utakuwa unajua kwamba katikati ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015, alikutana na watuhumiwa ufisadi wa Escrow kujadili njia za kumdhibiti Kafulila asirudi bungeni kwa sababu aliapa kufa na watuhumiwa hao.
“Lakini baada ya kuhakikisha Kafulila ameshindwa uchaguzi Kigoma Kusini na yeye akarudi bungeni kwa msaada wa rafiki zake wa ndani ya CCM, akaanza kuwasha moto tena akitaka mafisadi wa Escrow wakamatwe. Yote anapiga mkwara ili wamwite wampe kitu anyamaze.”
Aidha, Kafulila ameandika kuwa akielezea jinsi Zitto alivyotoa taarifa zisizo sahihi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu fedha zilizotumiwa na ACT Wazalendo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Zitto alisema kwa msajili wa vyama kuwa chama chake kilitumia jumla ya Shilingi milioni 600 na kidogo kwenye uchaguzi wa mwaka 2015. Sasa nenda kwa aliyekuwa Mweka Hazina wa ACT Taifa akupe ripoti kamili ya fedha. Chama kilitumia milioni 72 kwenye kampeni za urais nilizosimamia mimi.
“Lakini kwenye kampeni za ubunge alizosimamia yeye, chama kilitumia bilioni 1, milioni 144,” anazidi kuandika.
Sehemu nyingine ya andiko lake inayodai chuki ya Zitto dhidi ya Serikali inasomeka hivi; “Leo anakuambia anamchukia Rais Magufuli. Si yeye aliyebaki bungeni wakati nyinyi mnatoka na kususia hotuba ya Rais ya kuzindua Bunge?
“Si yeye aliyemsifia Rais kwa hotuba yake na kusema imesheheni ilani ya ACT kwa asilimia 60? Si yeye aliyemsifia wakati akimtumbua Prof. Muhongo (Sospeter) kwenye ripoti za Makinikia? Si yeye aliyewananga mlipopinga sheria ya madini kwa hati ya dharura?… anamchukia Rais Magufuli kimkakati. Mfano: Alipobaki bungeni na kuhudhuria kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Dodoma, alikuwa amepigwa changa la macho na marafiki zake wa ndani ya CCM kuwa Magufuli (Rais) angewateua watu wake fulani toka ACT kuwa wabunge mwanzoni kabisa mwa utawala wake.
“Lakini alipomchukia Magufuli (Rais) mwanzoni kabisa na kuanzisha Operesheni Linda Demokrasia ni baada ya uteuzi wa wabunge kukwama kisha akaenda kuangalia kwenye orodha ya kamati za bunge akakuta amepangwa kwenye kamati ya huduma za jamii na siyo hesabu za Serikali na rafiki yake mmoja akamwambia eti ni maelekezo ya Rais.
“Lakini pia marafiki zake waliokuwa wanaongoza mashirika ya umma na kumpa hela wakatumbuliwa. Alipomsifia sana Rais Magufuli, wakati wa kupelekwa sheria za madini kwa hati ya dharura na hatimaye akamsifia sana kule Kigoma alikofanya ziara Rais ni kwa sababu alikuwa ameahidiwa na wapambe wake kwamba Rais akirudi tu Dar, anamteua kumrithi Muhongo uwaziri wa Nishati na Madini.”