Monday, December 23, 2024
spot_img

LA JERRY SILAA LINAIBUA HOJA KUHUSU OGP

ABBAS MWALIMU – 0719 25 84 84

SPIKA wa Bunge, Job Justino Ndugai hivi karibuni aliamuru Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry William Silaa kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma mbalimbali ikiwemo kusema uongo kuwa wabunge hawalipi kodi kutoka kwenye mishahara yao (PAYE) na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Ofisi ya Bunge, tarehe 21 Agosti, 2021 ilieleza kuwa Silaa alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Jumanne ya tarehe 24 Agosti, 2021 saa 7 mchana.

Kanuni ya 4 (1) (a) na (b) ya nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Juni, 2020 inaipa mamlaka Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge kuchunguza mambo yanayohusu maadili ya wabunge yanayopelekwa na Spika, kutokana na kanuni hiyo mbunge huyo anatakiwa kujibu tuhuma zinazomkabili.

Lengo la makala hii si kujadili tuhuma zinazomkabili Silaa kutokana na kudaiwa kushusha hadhi na heshima ya Bunge kwa sababu maelezo yake yalishatolewa ufafanuzi na Bunge lenyewe kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma kupitia kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa kimataifa, tarehe 3 Agosti, 2021 bali tuhuma hizi zinaibua hoja juu ya mpango wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi, yaani Open Government Partnership (OGP) ambao Tanzania ilijiondoa mwaka 2017.

Tukumbuke kuwa Tanzania ilijiunga na mpango huo mwaka 2011, mara tu baada ya kuanzishwa na hivyo kuwa nchi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Afrika Kusini ambayo ilikuwa ya kwanza kusaini makubaliano hayo yanayotaka Serikali kuendesha mambo kwa uwazi bila ya usiri kati yake na wananchi.

OGP inajumuisha nchi zaidi ya 70 duniani ambazo zilisaini mpango huo unaohimiza dhana ya uwazi na ukweli.

Ninafahamu kuwa Tanzania ilijitoa OGP ili kutoa nafasi ya kutumia mpango wa Afrika kujipima kupitia APRM lakini bado ninaona kuna hoja katika OGP hasa kutokana na changamoto iliyomkuta Silaa.
Nasema hivi kwa sababu Silaa ni Mbunge wa Ukonga hivyo huenda maoni yake yanatokana na msukumo wa wanaukonga kutaka kufahamu anacholipwa mbunge wao kwa uwazi.

Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake mbalimbali inaeleza kuwa Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, (kwa niaba ya wananchi,) kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977.

Hivyo hoja hii ya mshahara inaweza kuwa imetoka kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga anaowawakilisha bungeni Dodoma. Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa OGP.

Miongoni mwa malengo ya mpango wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi (OGP) ilikuwa kuifanya Serikali kuwa wazi (kutokuwa na usiri) hadi kwenye mishahara ya viongozi wa kada mbalimbali, hivyo basi licha ya Bunge kufafanua yaliyokuwa yameelezwa na Silaa lakini nadhani bado kuna kundi kubwa la wananchi litakuwa linaamini kuwa labda wabunge kweli hawalipi kodi na labda Silaa anaonewa tu, huu unaweza kuwa mtazamo wa baadhi ya watanzania.

Moses (2016) katika andiko lake ‘Open Government: The Case of Tanzania in Open Government Partnership’, anaeleza kama ifuatavyo na ninamnukuu;

“Any government that wants to call itself open must provide free and accessible public information on taxation, draft and adopted budgets, and actual year- end spending including contract awards. There should be full and open disclosure on government bidding processes, job openings, salaries and benefits, court proceedings and legislation prior to and after passage. Also vital are sharing of key data on economic performance, public health conditions, and fair metrics of student and teacher performance at public schools.” Mwisho wa kunukuu.

Kwa mujibu wa Moses (2016), OGP inagusa mpaka kwenye mishahara, hivyo kwangu ninadhani kujiondoa kwenye mkataba huu wa OGP ndiko kulikoleta changamoto hii na kwa mtazamo wangu ni kwamba kama tungetekeleza OGP huenda shutuma hizi zilizompeleka Silaa mbele ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge zisingekuwepo kwa sababu wananchi ambao kimsingi ndiyo msingi wa mamlaka na madaraka ya Bunge kutokana na ibara ya 8 (1) ya Katiba ambayo inafafanua:

Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii, wangeweza kufahamu ni kiasi gani cha fedha wabunge ambacho wanalipwa kutokana na kodi zao na kiasi gani cha makato ya PAYE kinakatwa kutoka kwenye mishahara yao na hivyo kuondoa minong’ono ambayo imekuwa ikiibuka mitandaoni mara kadhaa.

Kwa mujibu wa Mabala na Mbogela katika ripoti yao ya utafiti iliyopewa jina ‘Evaluating and Shaping Engagement on OGP: A Case Story from Tanzania’ walioufanya kupitia taasisi ya ‘Global Integrity’ wameeleza kuwa Tanzania ilipojiunga na OGP mwaka 2011 ilikuja na Mipango kazi ya Taifa yaani ‘National Action Plans’ kwa kifupi NAPs miwili, mpango kazi wa kwanza ulitekelezwa kati ya mwaka 2012 na mwaka 2013 na mpango kazi wa pili 2014 mpaka 2016.

Katika mipango hiyo Serikali ilijidhatiti kukuza upatikanaji wa taarifa kuhusu shughuli mbalimbali za Serikali na kuchapisha data za sekta zilizopewa kipaumbele ambazo ni afya, elimu na maji.

Kwa mujibu wa Mabala na Mbogela, miongoni mwa maazimio 25 ya mpango wa kwanza, ni mipango miwili tu ambayo ilitekelezwa kwa ukamilifu huku bajeti ya wananchi ikielekezwa kwenye bajeti ya kitaifa tu huku bajeti kwenye ngazi ya Serikali ya Mtaa ikiwa inaelea sehemu ambayo Mabala na Mbogela wanaeleza kuwa ndiko kunakofanyika matumizi makubwa.

Kama ilivyokuwa kwa mpango kazi wa kwanza, mpango kazi wa pili ulikuwa na maazimio matano ambayo ni sheria ya upatikanaji wa taarifa, uwazi katika bajeti, data kupatikana kwa uwazi, uwazi katika ardhi na viwanda vinavyohusisha uchimbaji rasilimali kutoka ardhini.

Tatizo kubwa walilobaini Mabala na Mbogela ni mipango yote miwili kutofanyika kwa njia shirikishi (Participatory), kwa maana ya kwamba kulikuwa na ushirikishwaji mdogo wa wananchi katika utekelezaji wake.

Hivyo basi huenda kutoshirikishwa kwa wananchi kujua taarifa mbalimbali kuhusu wabunge wao nadhani ndiko kulikosabisha hali hii tunayoishuhudia sasa.

Hivyo huenda msukumo kutoka kwa wananchi ndiyo uliosababisha Silaa kuteleza katika hili la mishahara ya wabunge, lakini kuteleza huku ndiko kunakoibua hoja ya kurejea katika Mkataba wa OGP tuliojitoa mwaka 2017 ambao ungetupeleka mpaka kwenye uwazi wa mishahara ya wabunge na makato (PAYE) wanayopata sambamba na viongozi wa kada nyingine walioelezwa kama alivyoeleza Moses (2016).

Hivyo basi si vibaya Bunge likafikiri namna ya kuufanya mkataba wa OGP kurejewa licha ya umuhimu wa APRM.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya