MOURENE MALLYA
CHINA siyo Taifa lililopiga hatua kubwa katika mchezo wa Kun-fu pekee, bali kuna mengi ya kujifunza katika Taifa hilo kubwa na lenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani kiasi cha kulinyima usingizi Taifa la Marekani ambalo kwa miongo kadhaa sasa ndilo kinara wa uchumi duniani.
Hivi karibuni, nilipata wasaa wa kubadilishana mawazo na mchina mmoja kuhusu mambo ya maendeleo. Katika mazungumzo yetu, kijana mmoja alijiunga nasi na alimuuliza, “unaongeleaje tofauti ya maendeleo kati ya China na Tanzania, wapi kwa mtazamo wako pameendelea?”
Hili swali lilinishtua kwa sababu hata mtoto wa miaka mitano anajua uchumi wa China hauwezi kulinganishwa na uchumi wa Tanzania hata kwa theluthi moja na kufanya hivyo ni kama kumlinganisha simba na paka wakati ni wazi kuwa simba ndio mfalme wa nyika.
Nilisikia aibu kama mtanzania kwa swali aliloulizwa mchina yule mbele yangu lakini nikakumbuka kuuliza sio ujinga.
Mchina bila kusita alijibu kuwa China ipo mbali sana kiuchumi. Akatoa mfano rahisi wa gari moshi. Alisema, “China unaweza kusafiri kwa saa zisizozidi mbili ukitumia treni kutoka Dar es Salaam mpaka Arusha,” aliendelea kusifu miundombinu ya Taifa lake, huduma za kijamii, bidhaa na mambo kadha wa kadha. Hii ilipendeza sana kusikiliza.
Nilivutiwa sana na simulizi zake lakini alinivutia zaidi aliposema kuna baadhi ya mambo Tanzania inaweza kujifunza kutoka China. Kama mtanzania, nikatega sikio kwa utayari wa kupokea mafunzo yatakayoniwezesha kuijenga nchi niipendayo.
Jambo la kwanza alizungumzia sheria zenye adhabu kali. Alisema makosa ya uhujumu uchumi na rushwa yana adhabu kubwa sana China na haijalishi muhusika ni nani. Hata mtuhumiwa akiwa Rais wa nchi, adhabu yake ni ile ile wanayopewa wengine.
Akatoa mfano wa Ling Jinhua ambaye alikuwa msaidizi wa karibu wa Rais wa zamani wa China, Hu Jintao na Jaji wa Mahakama Kuu ya China, Huang Songyou walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu ya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Hii ilinipa picha kuwa Serikali ya China haina mchezo katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi. Hakuna kumuhamisha mtu wizara wala kumfanya ajiuzuru kwa hiari kutokana na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi bali mtu anafunguliwa mashtaka na kupewa adhabu kali endapo atakutwa na hatia. China kila mtu anapata kipato halali.
Tanzania tunaweza kuanzisha sheria kali kama hizi. Makosa mengi ya jinai na madai yamekuwa na adhabu lakini si kali za kuzuia watu kutotenda maovu, mfano kosa la mauaji kwa Tanzania adhabu yake ni kifo lakini hii adhabu haitolewi na ikitolewa ni kwa nadra na utekelezaji wake ni mgumu hivyo watu wanaendelea kuua wakijua hakuna kunyongwa.
Laiti adhabu ya kunyongwa ingekuwa inatekelezwa watu wangeacha kutenda makosa ya mauaji kwa sababu ya woga. China na Iran, kosa la kukutwa na dawa za kulevya adhabu yake ni kifo na kosa la kujihusisha na rushwa adhabu yake ni kufungwa maisha.
Tanzania tungeweka sheria ngumu kama hizi haina shaka mambo yangebadilika, watu wangepunguza matamanio ya mafanikio batili ya haraka katika maisha na kujitoa kufanya kazi kwa bidii ili kupata kipato cha halali na kukuza uchumi wa Taifa.
Rushwa na dawa za kulevya havitozwi kodi. Tutajadili zaidi huko tuendako tuone tunawezaje kutumia adhabu kali kulinda uchumi wa Taifa.
Katika mazungumzo yale, jambo lingine lililonivutia kwa wachina ni sheria ya kuzaa mtoto mmoja pia imesaidia sana uchumi wa China. Taifa la China lina idadi kubwa sana ya watu na iliwalazimu kuweka sheria ya kuzaa mtoto mmoja kudhibiti idadi ya watu ili kuboresha maisha.
Hii iliiongezea nguvu Serikali katika kutoa huduma nzuri na bora za kijamii. Miundombinu, elimu, makazi na malazi ya wananchi yameboreshwa kwa sababu ya kudhibiti ongezeko kubwa la watu ambalo haliendani na ukuaji wa uchumi.
Mpaka mwaka 2015, takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha muda wa kuishi (life expectancy) ya Wachina ni miaka 76. Hii inatokana na upatikanaji mzuri wa mahitaji muhimu kama chakula, afya, elimu, kazi na mengineyo yanayosababisha wananchi kufurahia maisha yao.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba mtizamo wangu huu umekuwa ukipata upinzani kwa baadhi ya watu na wengine wamekuwa wakinishutumu kwamba napendelea upande fulani ambao ni Serikali.
Leo ninapojadili hoja ya umuhimu wa kukaza sheria zetu kwa makosa makubwa na njia muafaka tunazopaswa kufuata kama Taifa kukuza uchumi wetu, ninataka ieleweke kwamba mimi ni mtanzania nisiyekuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa lakini ninaye amini katika utawala bora wa kisheria.
Kiongozi yeyote anayefuata misingi ya haki kisheria ni kiongozi wangu na si vinginevyo, nieleweke hivyo.
Pili, ninaamini kuwa mtegemea cha nduguye hufa masikini, hii inamaanisha kitu unachoweza kufanya wewe kama mtanzania fanya katika nafasi yako vinginevyo utaishia maisha ya malalamiko.
Kabla hujasema Tanzania utanifanyia nini, wewe jiongeze katika nafasi yako na ujiulize utaifanyia nini Tanzania kama nchi yako.
Matatizo mengine utatuzi wake upo katika mikono yako wewe na mimi; mfano, ongezeko la watu. Hili ni jambo ambalo mimi na wewe tunaweza kufanya uamuzi sahihi wa kuzaa watoto tunaoweza kuwalea na kuwapa maisha bora wakati huo huo tukijijengea maisha bora ya baadaye baada ya kustaafu ili tusiwe tegemezi na kuwasababishia watoto msongo wa mawazo ya kutulea. Manufaa ya uamuzi huu yanaweza kuonekana mpaka katika kukuza uchumi wa nchi.
Kingine kilichonifikirisha katika mazungumzo yale ni mapinduzi ya kilimo ambayo yamekuwa mkombozi mkubwa kwa Taifa la China kwa kusaidia uchumi wao wa viwanda. Hakuna bidhaa ambayo mtu utaitaka, utaikosa China.
Viwanda vikubwa vipo China na nchi nyingi zilizoendelea zimewekeza katika viwanda China na zinanufaika sana. Mpaka sasa Marekani inaongoza kiuchumi duniani ikifuatiwa kwa karibu sana na China lakini halitakuwa jambo la ajabu ndani ya muda mfupi China ikiongoza kiuchumi duniani.
Ni muhimu kujifunza na kutafiti mbinu mbalimbali za kilimo walizotumia wachina na hasa kilimo cha umwagiliaji na viwanda ili na sisi kama Taifa tunufaike na ujuzi wao.
Kwa sasa tunasema Tanzania ni ya viwanda lakini kazi ya ziada inahitajika kufanya tafiti za aina ya viwanda, bidhaa za kuzalisha, malighafi na masoko ya hizo bidhaa. Hii itaepusha kuwa na viwanda vingi vyenye bidhaa za aina moja au duni zisizokidhi mahitaji na kushindwa kupambana katika masoko ya kimataifa.
Lakini kikubwa kilichonifurahisha katika simulizi za mchina huyo ni miundombinu ya nchi. Nikitafakari foleni za barabarani katika Mkoa wa Dar es Salaam na muda tunaopoteza ambao ungetumika katika mambo mengine ya kimaendeleo napata simanzi.
Anapotokea mtu anapayuka kuponda jitihada kubwa za Serikali za ujenzi wa miundombinu, maneno yake yanakaharahisha bila kujali kama watanzania tunamsikiliza au lah kwa sababu masikio hayana pamba za kuyazuia yasisikie.
Hata hivyo kwa upande wa Serikali, miundombinu yetu inajengwa kukidhi mahitaji ya sasa na wataalamu wanasahau ya mbeleni. Mfano rahisi ni Barabara ya Mwendokasi kipande cha Jangwani. Mvua zilizonyesha wiki chache zilizopita zilileta balaa na kwa siku moja hiyo usafiri katika eneo hilo la Mkoa wa Dar es Salaam ulighubikwa na giza.
Tujiulize swali dogo, wakati wajenzi wanajenga ile barabara wakiwemo wahandisi wetu, walisahau tatizo la mafuriko katika eneo la Jangwani?
Mimi sio mtaalamu wa barabara lakini naamini kuna kitu kilipaswa kufanywa na wahandisi wetu waliohusika katika ujenzi wa barabara hiyo ili kukabiliana na tatizo hilo kwa sababu ni wajibu wao kuepusha maafa makubwa kama yaliyotokea kwa kutumia utalaamu wao.
Funzo lingine kutoka China nililolipata katika mazungumzo yale linawahusu wanasiasa. Wanasiasa ni lazima wabadilike, wasitumie shida zetu watanzania kutufumba macho kwa ahadi feki.
Wapo wanasiasa ambao tangu walipopigiwa kura na kuchaguliwa hawajawahi kurudi majimboni mwao. Walitudanganya barabara, maji safi, majengo mazuri ya shule, hospitali na kadhalika lakini mpaka leo hakuna kitu.
Lakini mwisho, mchina yule alisema maneno yaliyonibariki sana. Alisema wachina hawajali siasa hata kidogo, wao wanachotaka ni maisha bora na wao wako tayari kutoa ushirikiano kwa yeyote atakaewapa maendeleo na maisha bora.
Huu ndio ukomavu wa akili. Tazama siasa chafu zinavyotuvuruga Tanzania na kutufanya tusahau maendeleo tuliyofikia. Wanasiasa baadhi wana ndimi chafu, waongo, wasengenyaji, wanalamba matapishi yao, wameuweka kando utamaduni wa kiafrika na kitanzania na sasa wanagombana hadi na wasiokuwa na kauli; lakini kibaya zaidi ni kuwa mfano mbaya kwa kukosa heshima na adabu kwa viongozi wa Taifa letu.
Hebu tutizame nchi ya Kenya, Taifa jirani ambalo siasa inatumiwa kama chombo cha kugawa watu kwa ukabila! Je wanasiasa wenye ndimi chafu na wachochea ukabila wanataka na sisi tufike huko kwa jirani zetu?
Ushabiki wa siasa sio kama ushabiki wa mpira maana siasa ni maisha yako na mpira ni burudani. Wanasiasa hawana budi kuwa na maamuzi sahihi kwa niaba ya wananchi tulio wengi maana dhamana waliyopewa ni kubwa na watadaiwa na Mungu.
Tujifunze kutoka mataifa yaliyoendelea na tufanye maamuzi sahihi yanayozingatia sheria na haki za kila mtanzania. Watanzania tunataka maendeleo, hatutaki siasa za matusi na kutugawa.
Ninaamini tukizingatia sheria na haki za kila mtanzania, ipo siku na sisi uchumi wetu unaweza kukua kwa zaidi ya asilimia saba kwa mwaka. Kama binti wa kitanzania naruhusiwa kuiwazia mema nchi yangu, Nisihukumiwe; ni mawazo yangu tu.
MOURENE MALLYA NI MWANASHERIA KITAALUMA