RIPOTA PANORAMA
NAIBU Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema Serika itaboresha mazingira ya uwekezaji wa Madini ya Nickel yanayopatikana Wiaya ya Ngara mkoani Kagera ili kuwawezesha wawekezaji kuyaogezea thamani kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.
Aliyasema hayo jana alipotembelea Mradi wa Uwekezaji wa Madini ya Nickel wa Kabanga, uliopo Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera.
“Sisi Serikali tutahakikisha tunawaletea wawekezaji miundombinu ya barabara, reli na umeme ili kuwajengea mazingira rafiki ya uzalishaji lakini kwa upande wao tunataka kuona uwekezaji makini.
“Wachimbe na kuongeza thamani ya madini hayo hapa nchini badala ya kutoa Nickel kama malighafi watoe bidhaa zinazotokana na Nickel,” alisema Nyongo.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha madini hayo muhimu ambayo kwa sasa soko lake duniani limeanza kupanda yanalinufaisha Taifa kwa kiwango kinachostahili.
“Tunataka wawekezaji wachimbe ili tupate kodi, tupate mrabaha lakini pia wananchi wa maeneo haya waweze kupata ajira,” alisema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mradi wa Kabanga Nickel, Meneja Mkazi, Andrew Msola alisema changamoto waliyonayo ni ukosefu wa miundombinu ya barabara, reli na umeme.
Mradi wa Kabanga Nickel ulianza uzalishaji wa Madini ya Nickel zaidi ya miaka 40 iliyopita lakini tangu mwaka 2009 ilisimamisha uzalishaji kutokana na kuporomoka kwa bei ya madini hayo katika Soko la Dunia.