RIPOTA PANORAMA
Wananchi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma wameiomba Serikali isaidie kuwapatia wataalam wa miamba watakaotafiti na kubainisha kiasi cha madini yaliyogundulika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya wilaya jana kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ambaye yuko katika ziara ya kikazi wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala alisema Madini ya Dhahabu yamegundulika katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alitaja baadhi ya maeneo yaliyogundulika kuwa na madini hayo ni pamoja na Nyamtukuza, Kasuga na Muhange lakini haifahamiki kiasi cha madini kilichopo.
“Tunakuomba utusaidie upatikanaji wa wataalamu ili kujua takwimu sahihi za kiasi cha madini kilichopo kwenye maeneo yaliyogundulika,” alisema.
Kanali Ndagala alisema wilaya hiyo ina madini mengi ya chokaa katika Hifadhi ya Pori la Akiba la Moyowosi lakini hayachimbwi kwa sababu sheria za hifadhi haziruhusu.
Akijibu maombi hayo, Naibu Waziri Nyongo alisema Serikali itafanya tafiti mbalimbali za madini nchini kwa kuwatumia wataalamu wa jiolojia kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).
“Tutawaelekeza wataalam wetu wafike hapa Kakonko kufanya utafiti,” alisema Nyongo.
Aidha, aliahidi kulifanyia kazi suala la upatikanaji wa Madini ya Chokaa katika eneo la hifadhi.
Naibu WaziriNyongo anaendelea na ziara yake ambayo itahitimishwa mkoani Kigoma baada ya kuitembelea mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.