WAKATI mashabiki wa Simba wakijiuliza kuliko kwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Nelson Okwa kutocheza kwenye kikosi cha sasa, mwenyewe amevunja ukimya na kuanika kinachomfanya asitumike tofauti na ilivyokuwa enzi za kocha Zoran Maki.
Okwa, raia wa Nigeria alisajiliwa chini ya Zoran aliyetimkia Al Ittihad ya Misri alikuwa akitumika katika kikosi cha timu hiyo, lakini tangu Juma Mgunda apewe timu jamaa amekosa nafasi na mwenyewe ameliambia Mwanaspoti sababu za kutoonekana uwanjani.
Mnigeria huyo alisema kukosekana kwake kunatokana na mabadiliko ya benchi ya ufundi, huku akikiri kuwa hata mastaa wanaopata nafasi kwa sasa wana ubora hivyo anapambana kumshawishi Mgunda.
Okwa aliyesajiliwa kutoka Rivers United alisema ni kweli kama mchezaji hafurahii; “Nilipata nafasi nikiwa chini ya Zoran Maki wakati huo kuna wachezaji pia walikuwa hawapati nafasi na sasa chini ya kocha mpya wanacheza mfano mzuri ni Mzamiru Yassin, Joash Onyango wengine hivyo naamini utafika muda nitacheza na nitaonyesha uwezo mkubwa.”
“Pia kila kocha ana aina ya wachezaji anaowataka kuna anaependa mchezaji anayekimbia sana, anayejua kukokota mipira na kutoa pasi, anayejua zaidi kufunga hivyo naamini hao waliopata nafasi wana sifa za kocha aliyopo lakini hainikatishi tamaa nitapambana ili niweze kupata nafasi ya kucheza.”
Akizungumzia mechi ya Jumapili, Okwa alitoa nafasi kubwa kwa Simba kuibuka na ushindi kutokana na namna timu hiyo ilivyo na muendelezo mzuri wa kupata matokeo kwenye kila mchezo na mabadiliko ya ubora wa mchezaji mmoja mmoja.
“Simba itaibuka na ushindi, nawaheshimu wapinzani wetu (Yanga), lakini kwa sasa sisi ni bora kuanzia ndani hadi mashindano ya kimataifa. Angalia matokeo yetu tuliyoyapata hivi karibuni pia ukiangalia mchezaji mmoja mmoja kumekuwa na ongezeko la utimamu wa mwili,” alisema Okwa na kuongeza;
“Tunataka kuendeleza furaha za mashabiki zetu na huu ni mchezo ambao umekuwa ukiumiza hisia zao sana tofauti na mechi nyingine kutokana na utani wao wa jadi, tumekosa matokeo mchezo wa mwisho dhidi yao hatuwezi kurudia makosa.”
Okwa ni miongoni mwa wachezaji waliong’ara na kuwa gumzo wakati wanasajiliwa Simba kutokana na rekodi zake