Sunday, June 22, 2025
spot_img

MAJALIWA AWAONYA WATEULE WA RAIS SAMIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

 

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma watimize wajibu wao kama yalivyo matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan anapowateu au kuwapa ajira.

Majaliwa aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na viongozi na watumishi wa Mkoa wa Ruvuma katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba muda mfupi baada ya kuzindua jengo la halmashauri ya wilaya hiyo. 

Alisema Rais Samia anataka kuona watumishi wa umma wakiwatumikia Watanzania hivyo wanapaswa kutoka ofisini kwenda kuwasikiliza kwa sababu hawawezi kuwatumikia wananchi bila kuwasikiliza na kujua changamoto zao. 

Majaliwa aliwataka viongozi na watumishi hao kufanya kazi kwa kulenga matokeo. “Nataka tufanye kazi kwa matokeo, tufuate maelekezo na tuzingatie nidhamu. Tuna fedha za ndani na za Serikali Kuu. Tuzisimamie vizuri na naomba msijiingize kwenye matumizi mabaya ya fedha hizo,” aliwaonya. 

Waziri Mkuu aliwapa mfano wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Irugwa ambaye alipokea Sh. milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita, lakini alizisimamia vizuri akamaliza madarasa, akajenga matundu matano ya vyoo, akaweka mfumo wa maji ya mvua na chenji iliyobakia akapiga lipu mabweni ya wasichana na kujenga mabafu licha ya kuwa shule iko kisiwani na kisiwa kiko mbali kutoka Nansio (makao makuu ya wilaya) na pia kiko mbali kutoka Mwanza ambako mahitaji yote yanafuatwa. 

“Nanyi pia fanyeni hayo hapa Madaba, mtumishi wa umma jitahidi ufanye jambo ambalo wengine limewashinda. Mheshimiwa Rais Samia anatamani kuwa na watumishi wengi wa aina hiyo,” alisema.

Akizungumza kuhusu hoja za CAG, Majaliwa alisema halmashauri hiyo ya ilikuwa na hoja 46 ambapo hoja 28 zimefungwa na hoja 18 bado hazijafungwa na kuagiza hoja 18 zilizobakia zimalizwe.

Kuhusu ujenzi wa hospitali ya halmashauri hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka viongozi na watumishi hao kukamilisha ujenzi kwa viwango alivyoviona na alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Sajidu Mohammed kwa usimamizi mzuri.

Mapema, Waziri Mkuu Majaliwa alikagua ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na kuweka jiwe la msingi. Ujenzi wake umeshatumia Sh. bilioni 2.084.

Akizungumza na wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa anatarajia hatua ya ukamilishaji itazingatia viwango bora.

Naye, Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wana-Madaba Sh. bilioni 14.2 ambazo zimetumika kujenga miradi ya maji, barabara za vijijini, miundombinu ya afya na elimu. 

Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali iwajengee kituo kikubwa cha mabasi na soko kubwa. 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya