Nahodha wa zamani wa Arsenal, ambaye hivi sasa ni meneja wa klabu ya soka ya Cristal palace, Patrick Viera, ameelezea kufurahishwa kwake na mchango wa mshambuliaji mwenye asili ya Afrika, Wilfried Zaha, baada ya mshambuliaji huyo kukiongoza kikosi chake kuibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Wolves katikati ya wiki hii.
Zaha, ambaye mkataba wake anakodolewa macho na vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya, mkataba wake unaelekea ukingoni na mazungumzo juu ya mkataba mpya yameendelea kuwa siri kubwa baina yake na waajiri wake hao, huku kukiwa na tetesi za kuwa bado hakuna makubaliano ambayo yameweza kufikiwa hadi sasa.
Hata hivyo, suala hilo halikumzuia mshambuliaji huyo kuonyesha kandanda safi na kuhusika na magoli yote mawili yaliyofungwa na Palace, ambao walikuwa wametangulia kufungwa na Wolves, ambao walipata bao lao kupitia Adama Traore.
Shuti la mpira wa adhabu lililopigwa na Ruben Neves dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza, liligonga mwamba wa kushoto wa goli la Palace huku kipa wao akiwa amesimama kama nguzo, na hivyo kunusurika kwenda mapumziko wakiwa na mzigo wa mabao 2-0 na huenda na idadi hiyo ndogo ya mabao iliwapa hamasa Palace ambao walirejea kipindi cha pili kwa nguvu na kusawazisha kisha kupata bao la ushindi.
Matokeo hayo yanawafanya palace kukwea hadi nafasi ya 10, wakiwa wamejikusanyia pointi 13 baada ya michezo 10 huku Wolves wakibaki katika nafasi ya 17 kwa alama 9 wakiwa na idadi sawa ya michezo.
Akiongea na wanahabari baada ya mechi hiyo, Viera amesema amefurahishwa na wachezaji wake kutimiza majukumu yao ambayo ni kucheza mpira, huku akisema masuala ya mikataba yana watu wake wa kuyashughulikia na anatarajia Zaha ataendelea kuonyesha kiwango bora na kuisaidia timu wakati suala lake linafanyiwa kazi.