Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya St. Anne Marie Academy, Profesa Gradius Ndyetabula anayedaiwa kutiwa mbaroni kwa makosa ya wizi wa mtihani wa darasa la saba. |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi ya St. Anne Marie Academy, iliyopo Mbezi Kimara – kwa Msuguli, jijini Dar es Salaam, Profesa Gradius Ndyetabula anadaiwa kutiwa mbaroni wiki iliyopita akituhumiwa kwa makosa ya wizi ya mitihani ya darasa la saba.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka vyanzo vyake vya habari pamoja na watu walio karibu na Prof. Ndyetabula zimedai kuwa amewekwa korokoroni katika Kituo Kikuu cha Polisi (central) Dar es Salaam akiwa pamoja na walimu wenzake zaidi ya kumi kutoka shule mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam wanaotuhumiwa pamoja naye kutenda makosa hayo ya wizi,
Inadaiwa kuwa, Prof. Ndyetabulaalikamatwa baada ya wana usalama kuliona jina lake katika simu ya kiganjani ya kinara wa wizi wa mitihani ya Taifa ya darasa la nne na la saba, likiwa kwenye mtandao wa wakuu wa shule waliokuwa wakiwasiliana na mtu huyo ambaye simu yake imekuwa ikipokea miamala ya fedha zinazodhaniwa kuwa ni za malipo ya mitihani ya wizi wanayonunua baadhi ya walimu wakuu na wamiliki wa shule kutoka kwake kwa lengo la kupandisha ufaulu wa shule zao.
“Ni kweli amekamatwa, alikamatwa tangu jumatatu ya wiki iliyopita, aliingia kwenye mtego wa wanausalama wanaopambana na wizi wa mitihani ya Taifa. Walimpigia simu wakijifanya ni wazazi wanaotaka kupeleka wanafunzi kujiunga na shule yake, alipotoka hadi mapokezi wakamuweka chini ya ulinzi.
“Walikwenda pale shuleni, wakaomba kuonana na mwalimu mkuu, alipojitokeza mapokezi wakamuonyesha vitambulisho, likaja gari lao wakambeba wakaondoka naye. Anatuhumiwa kwa wizi wa mtihani wa Taifa wa darasa la saba, kusambaza au kuwa na mtihani wa Taifa kinyume cha taratibu,” alidai mtoa habari wetu aliye karibu na familia ya Prof. Ndyetabula.
Taarifa zaidi zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedai kuwa mtaalamu mmoja wa elimu ambaye jina lake halijafahamika na ambaye anafanya kazi katika moja ya taasisi binafsi za elimu ambayo kazi yake ni kusambaza mitihani ya darasa la nne na la saba kwenye shule mbalimbali, wakati akitekeleza jukumu lake hilo, pia alikuwa na mitihani yake ya wizi mkononi ambayo alikuwa akiwauzia walimu wakuu wa shule na wamiliki waliokuwa wakihitaji.
Inadaiwa, mtu huyo aliiuza mitihani hiyo kwa baadhi ya walimu wakuu wa shule binafsi lakini kwa shule za Serikali alimtumia mtu anayetajwa kwa jina la FBI ambaye hufundisha muda wa ziada katika baadhi ya shule za Serikali za jijini Dar es Salaam lakini haifahamiki hasa ni mwajiriwa wa wapi, kumuuzia mitihani yake hiyo ya wizi.
“Kuna mwalimu mmoja ambaye ni mtaalamu wa taasisi moja, Non Govermental School Orgnisation, akiwa mtaaluma wa hiyo taasisi ambayo kazi yake ni kusambaza mitihani kwenye mashule hasa ya darasa la nne na la saba ambayo ni madarasa ya mitihani. Sasa inasemekana alikuwa na mitihani yake ya wizi pia mkononi aliyokuwa akiwauzia watu tofauti tofauti wakiweno hao wakuu wa shule binafsi na za Serikali.
“Huku za Serikali alitumiwa mtu anayefahamika kwa jina la FBI ambaye huyu FBI hufundisha baadhi ya shule za Serikali za mjini lakini muda wa ziada, haifahamiki hasa kama ni mwajiriwa wa kampuni gani au shule gani . Huyu jamaa amekuwa akitumiwa na baadhi ya shule kuwasambazia mitihani ya kujipima kabla ya mitihani ya Taifa na huku simu yake ikitumika kukusanya pesa za mauzo ya mitihani ya wizi anayowauzia walimu na wamiliki wa shule. Na huo ndio mwanzo wa kukamatwa kwa profesa,” alidai mtoa taarifa wetu.
Tanzania PANORAMA imemtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo kuzungumzia kukamatwa kwa Prof. Ndyetabula ambaye simu yake ya mkononi ilipoita ilipokelewa na msaidizi wake aliyeeleza kuwa yupo kwenye kikao mkoani Morogoro.
“Mimi ni msaidizi wake, Kamanda yeye yupo kwenye kikao hapa Mkoa wa Morogoro, kikao hiki kinaanza asubuhi na kinamalizika saa 12 jioni hivyo labda mtafute muda huo wa kuanzia saa 12 lakini hata hivyo huyo mtu hayupo Central kwa sababu hilo suala haliwahusu polisi bali vyombo vingine vya usalama,” alisema.
Alipoelezwa kuwa Tanzania PANORAMA inazo taarifa kutoka kwa watu walio karibu na familia ya Prof Ndyetabula kuwa amekamatwa tangu wiki iliyopita na anazuiliwa korokoroni ya kituo hicho, alisema majukumu ya ukamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ameachiwa Kamishna Kupa hivyo atafutwe yeye anaweza kulizungumzia hilo.
Alipotafutwa Kamishna Kupa na kuulizwa alisema suala hilo aulizwe moja kwa moja Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (ZCO) Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele ambaye licha ya kutafutwa muda mrefu, simu yake iliita bila kupokelewa.
Vyanzo vya habari vya Tanzania PANORAMA vimedai kuwa Prof. Ndyetabula ambaye ilikuwa afikishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jumatatu, wiki hii sasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo leo.