RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 83
GENGE la watu wanaodaiwa kuwa na utajiri mkubwa jijini Dar es Salaam linadaiwa kuunda mtandao wa kujipatia mamilioni ya fedha kutoka kwa wazazi na walezi wa watoto wanaotafuta shule bora za binafsi kwa ajili ya watoto wao wanaosoma elimu ya sekondari
Inadaiwa mmoja wa viongozi wa genge hilo aliyetajwa kwa jina la Tonny Kabetha ambaye ni mtanznania aliyeishi nje ya nchi kwa miaka mingi kabla ya kurudi nchini na kuanza kujishughulisha na kuwaunganisha vijana wa kitanzania na vyuo vikuu vya nje ya nchi amekuwa pia akitumia maeneo na majengo yasiyokuwa yake kutapeli wazazi na walezi wa wanafunzi.
Kwa mujibu wa watu waliokutana na kadhia ya kutapeliwa na genge hilo, mbali na kujishughulisha na kuwaunganisha wanafunzi wa kitanzania na vyuo vikuu vya nje, pia limekuwa likitangaza katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa linamiliki shule za sekondari katika mikoa mbalimbali nchini huku likikusanya fedha za ada kutoka kwa wazazi na walezi wanaohadaika na matangazo hayo na kuzitia kibindoni.
Inadaiwa genge hilo ambalo mmoja wa washirika wake ni mtumishi wa Serikali mwenye ukwasi wa kutosha halina shule ambazo limekuwa likitangaza kuzimiliki na wala halina maeneo wala majengo linayotangaza kuwa ni shule zake.
“Utapeli sasa umehamia kwenye elimu, hawa watu walitangaza kwenye mitandao ya kijamii na kwenye televisheni kuwa wana shule huko Kibaha Pwani inayoitwa U.A R International Open School kwa ajili ya wanafunzi wa bweni na kutwa. Kwenye matangazo yao wanasema shule hiyo ipo nyuma ya Ofisi za NIDA Kibaha kumbe hakuna shule hapo bali kuna majengo wanayoyatumia kutapeli,” alisema mtoa taarifa.
Mmoja wa wazazi ambaye Februari 21, 2022 alilipa ada ya mwanae, Sh. milioni moja kwenye akaunti ya genge hilo yenye jina la Universities Abroad Link iliyopo Benki ya CRDB amesema alipofika na mwanae kwenye majengo aliyoambiwa kuwa ni ya shule hakukuta mwalimu, kiti wala meza na badala yake alipokelewa na mtu anayemtaja kwa jina moja la Mussa ambaye alimwambia shule hiyo bado haijakamiliki kutengenezwa.
Alisema, Musa baada ya kumuona akiwa na mwanae alianza kuwasiliana na washirika wake kabla ya kumuomba wamtafutie shule nyingine ambayo mtoto wake anaweza kwenda kusoma kwa sababu eneo hilo lililotangazwa siyo shule.
“Nilishtuka nilipofika pale na mwanangu tukiwa na begi lake na godolo sikukuta mwalimu, kiti wala chaki. Kulikuwa na kijana mmoja nadhani ni mshirika wao akaanza kuniuliza ninakotokea nikamwambia kila kitu, nikamuuliza mbona mnatangaza mna shule kumbe hamna shule mpaka tunawalipa na kusafiri kuja huku akaniomba nisubiri.
“Alipoona nimechachamaa akaanza kuwasiliana na wenzake kwenye simu ndipo baadaye akaja kuniomba eti mwanangu wampeleke shule nyingine ya jirani hapo wakati wao wanaendelea kumalizia ukarabati wa hiyo shule waliyotutangazia. Sikuwa na jinsi kwa sababu na hela nilikuwa nimeishawalipa, naona wana mtandao mpana sana na wenye hizi shule za binafsi kwa sababu baada ya kufanya mawasiliano wakatuchukua na mwanangu wakatupeleka shule ya Sekondari Kafurusu hapo akapokelewa nikamuucha hapo lakini mazingira ya hiyo shule siyo mazuri kama ile wanayoitangaza kwenye televisheni na mitandaoni,” alisema.
Alipoulizwa Kabetha kuhusu tuhuma za utapeli anazoelekezewa alisema ni kweli alikuwa na mpango wa kufungua shule lakini alishindwa kuanza kuchukua wanafunzi kwa sababu matengenezo katika baadhi ya majengo yalikuwa hayajakamilika.
Alipoulizwa ni kwanini alitangaza kuwa ana shule wakati hajaisajili na akaenda mbali zaidi kwa kuchukua fedha za watu huku akiwa hata hajakamilisha matengenezo ya majengo ya shule yake alisema yupo Zanzibar kwenye mkutano lakini ifahamike kuwa alinunua eneo Kibaha kwa ajili ya ujenzi wa shule na taratibu za usajili alikuwa ameishazianza kabla ya kukwama. Kuhusu kuchukua fedha za ada alisema malipo hayo hayatambui.
“Shule ipo, nilinunua eneo Kibaha kwa ajili ya kuanzisha shule ni kweli na niliitangaza kwa sababu nilitarajia kuanza kuchukua wanafunzi wa bweni na kutwa lakini wanafunzi walianza kuja kabla ya kukamilika kwa matengenezo. Hao waliokuja tuliwatafutia shule nyingine wakaenda kusoma ingawa nasikia hiyo shule haina walimu wazuri na waliopo ni wachache labda hicho ndicho wazazi wanalalamika kwa sababu ile ya kwangu ni nzuri sana waliyoiona kwenye matangazo.
“Hayo malipo yanayosemwa mimi siyatambui, hakuna mtu aliyenilipa kwa ajili ya mwanae kuja kusoma kwenye shule yangu, kwa sasa nipo Zanzibar kuna mkutano fulani nahudhuria huku lakini nikirudi Dar es Salaam njoo ofisini nikufafanulie vizuri,” alisema Kabetha.
Alipotafutwa Musa kupitia simu yake ya kiganjani na kuulizwa kuhusu shule hiyo, alikata simu mara moja baada ya kusikia swali na alipopigiwa tena na tena simu yake haikupatikana.
Alipoulizwa Mdhibiti Ubora wa Shule za Sekondari wa Mkoa wa Pwani, Agustino Mkumbo alisema huo ni utapeli na wanaojihusisha na genge hilo wanapaswa kufikishwa polisi na kufunguliwa mashtaka.
‘QT nyingi hazijasajiliwa, ni kama tuition center tu. Ila mwenye center hiyo akitaka iwe official wanaohusika ni watu wa elimu ya watu wazima. Lakini kama ni shule ni lazima isijaliwe, shule kabla ya kuanza shughuli zake lazima ikaguliwe sasa huyo anayetangaza kuwa ana shule na anachukua hela za watu hata kama ni sh. 10 tu huyo ni tapeli, ni wa kupelekwa polisi na wao polisi wakikamilisha taratibu zao anapelekwa mahakamani kujibu huo utapeli wake.
“Lakini sisi pia tunaweza kuchukua hatua na moja ya hatua zetu tukimbaini mtu huyo hata kama alikuwa na nia hiyo ya kufungua hiyo shule nasi tunampiga marafuku kabisa kufanya hiyo shughuli. Lakini ninachoweza kusema kwa sasa hilo genge linapaswa kukamatwa na kufikishwa polisi,” alisema Mkumbo.
PANORAMA BLOG INAENDELEA KUFUATILIA NA KURIPOTI SKENDARI HII.